JESHI
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaa, limeshindwa kujibu madai ya
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo, Josephati Gwajima, ya kulitaka
liwakamate watu waliohusika kumteka na kumtesa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, Dk. Ulimboka.
Hatua
hiyo inakuja siku chache baada ya jeshi hilo, kumkamata na kumfikisha
mahakamani raia wa Kenya Joshua Mhindi (21), akidaiwa kuhusika na tukio
hilo, madai ambayo mchungaji Gwajima, alihoji ni kwa nini watuhumiwa
waliotajwa moja kwa moja na Dk. Ulimboka mwenyewe hawakamatwi na
kuhojiwa.
Kamanda
wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari
juu ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo wiki iliyopita, alilihusisha kanisa
la Ufufuo na Uzima akidai Mulundi ni muumini wao, jambo ambalo
lilipingwa vikali na mchungaji Gwajima na kuanika mkasa mzima.
Hata
hivyo jana katika mkutano wake na vyombo vya habari, Kova alikwepa
kabisa kuzungumzia madai ya mchungaji Gwajima na badala yake akadai kuwa
jeshi hilo halina haja ya kuingia kwenye malumbano na viongozi wa dini.
Kova alifafanua kuwa kwa sasa suala la Mhindi na mlalamikaji Dk. Ulimboka, halizungumziki nje ya utaratibu wa mahakama.
“Ni
kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujadili jambo
ambalo liko mahakamani kama ilivyo katika shauri hili,” alisema Kova.
Kuhusu
madai ya mchungaji Gwajima kuwa mtuhumiwa ni kichaa au mwendawazimu,
Kova alisema kuwa kisheria ni suala ambalo daktari ndiye mwenye uwezo wa
kumpima kitaalamu.
Alibainisha
kuwa hata kichaa au mwendawazimu anamilikiwa na sheria ambapo kama
akifanya makosa ya jinai, anashughulikiwa kama mhalifu mwingine.
Vile
vile alisema jeshi hilo haliwezi kuingia katika mtengo wa malumbano na
taasisi za dini iwe ni ya Kikristu au Kiislamu ama madhehebu mengine.
Kova
alisema jeshi hilo lina wajibu wa kudumisha amani ili viongozi wa dini
na waumini wao wawe huru bila hofu katika kufanya ibada zao usiku na
mchana.
Mchungaji
Gwajima katika mkutano wake juzi, alisisitiza kuwa analishangaa jeshi
hilo kwani mtu wa kwanza ambaye alipaswa kukamatwa na kuhojiwa kutokana
na tukio ni Afisa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ahmed
Msangi, ambaye alitajwa na Dk. Ulimboka.
1 comment:
Nina imani hata wasipokamatwa Damu ya Ulimboka bado inalia lazima wakutane na nguvu za Mungu, neno linasema kila unachopanda utavuna, wao walimwaga damu na yao itamwagika pia
Post a Comment