ANGALIA LIVE NEWS
Friday, July 13, 2012
Ndoa ya Slaa njia panda
WAKILI WAKE ASEMA HAKUNA ZUIO LA MAHAKAMA, JAJI KUSIKILIZA KESI AGOSTI 14
Tausi Ally na James Magai
MAHAKAMA Kuu imepanga kuanza kusikiliza kesi ya kupinga ndoa ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na mchumba wake Josephine Mushumbusi Agosti 14, mwaka huu.Slaa na Mushumbusi walitarajia kufunga ndoa katika Kanisa Katoliki Julai 21, mwaka huu, lakini Rose Kamili, anayedai kuwa ni mke wa Dk Slaa, amefungua kesi kuipinga na kudai fidia ya Sh550 milioni.Jana, Jaji Lawrance Kaduli akitaja kesi hiyo namba 4 ya mwaka 2012, alisema Dk Slaa na Mushumbusi wanatakiwa kujibu pingamizi hilo la ndoa kwa njia ya maandishi kabla ya Julai 30, mwaka huu.
Pia alimtaka Kamili kupitia wakili wake, Joseph Thadayo kama watakuwa na majibu yoyote wayasajili Agosti 7, mwaka huu na baada ya taratibu hizo Agosti 14, mwaka huu atasikiliza kesi hiyo.
Kitendo cha kesi hiyo kupangiwa tarehe ya mbele, siku 22 baada ya siku iliyopangwa kwa ajili ya kufunga ndoa, kinaiweka ndoa ya wawili hao njia panda na kuacha maswali mengi iwapo itafungwa au la.Mutakyimilwa Philemon ambaye ni wakili wa Dk Slaa alipoulizwa nje ya mahakama kuhusu mchakato huo wa kisheria kama utazuia ndoa hiyo kufungwa, alijibu:
“Hakuna amri ya mahakama ya kuzuia ndoa. Kwa hiyo itategemea busara tu. Lakini, sitaki kuzungumza kama ndoa ipo au haipo, hilo ni jambo la mahakamani.”
Madai ya Kamili
Katika kesi hiyo, Kamili ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), anaiomba mahakama kusimamisha ndoa hiyo.
Pia anaiomba mahakama iamuru Dk Slaa amlipe Sh50 milioni kama fidia ya fedha alizotumia kujihudumia pasipo matunzo ya mumewe.
Mbunge huyo pia anaiomba mahakama iamuru Mushumbusi amlipe Sh500 milioni kama fidia ya maumivu aliyoyapata kutokana na kitendo chake cha kuingilia ndoa yao.
Katika hati hiyo ya madai, mbunge huyo anadai kuwa ndoa inayotarajiwa kufungwa kati ya Dk Slaa na Mushumbusi ni batili kwa sababu kuna ndoa nyingine halali na inayoendelea kuishi, kati yake na mumewe huyo iliyofungwa mwaka 1985.
Alidai baada ya kufungwa kwa ndoa hiyo, Juni 18, mwaka 1987 walifanikiwa kupata mtoto wa kike anayeitwa Emiliana Muchu na baadaye Septemba 23, mwaka 1988 walipata mtoto mwingine wa kiume, Linus Amsi.
Anadai kuwa katika uhusiano wao, Slaa akiwa ni Padri alifanya taratibu zilizomwondosha katika nafasi hiyo ya upadri na kuanza maisha ya familia.
Baada ya taratibu hizo, anadai kuwa jamii ya Watanzania iliwatambua kama mume na mke, na hata kumbukumbu za hati za kimataifa kama za kusafiria ziliwatambua kuwa wanandoa.
Kamili aliendelea kudai katika maelezo hayo kuwa, yeye na Slaa waliishi maisha ya ndoa yenye amani, yaliyowawezesha kupata mali kadhaa walizomiliki kwa pamoja ikiwamo nyumba iliyopo kwenye kiwanja namba 609 kitalu E, nyumba ya makazi iliyopo katika Kijiji cha Gongali, Karatu na vifaa mbalimbali vya nyumbani.
Hati ya mashtaka imeendelea kueleza kuwa, uhusiano kati ya Slaa na Kamili, ulianza kuharibika mwaka 2009, baada ya Slaa kuwa na uhusiano na mwanamke mwingine kinyume cha sheria.
"Tangu mwaka 2009, Slaa akaitelekeza familia yake kwa kutoipatia huduma," imeeleza hati hiyo.
Kamili anaiomba mahakama iamuru kuwa yeye na Slaa bado ni mke na mume na kwamba, Mushumbusi aliingilia ndoa yao, hivyo mahakama izuie ndoa inayotarajiwa kufungwa Julai 21, mwaka.
Kamili pia amewasilisha hati hiyo ya mashtaka kwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.
Kamili amemweleza Kadinali Pengo ambaye pia anaongoza Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kuwa moja ya Parokia za Dar es Salaam zina taarifa ya ndoa hiyo.
Nakala ya madai hayo pia imewasilishwa kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Msajili wa Ndoa na kwa Askofu wa Jimbo la Mbulu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Yaani am so proud of her...wanawake afrika tumezidi kuonewa hii itakuwa fundisho kubwa sana kwa jamii yetu ya kitanzania!mama Kamili good for you gombea haki yako!
Post a Comment