ANGALIA LIVE NEWS
Friday, August 17, 2012
MADAI YA ZITO NDUNGAI ALIPUKA ASEMA ANAUTUMIA VIBAYA UKUMBI WA BUNGE ADAI ANALIFANYA TAIFA LIAMINI UWONGO WAKE
NAIBU Spika wa Bunge, Bw. Job Ndugai, amemshukia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), baada ya kushindwa kuwataja kwa majina viongozi wa Serikali aliodai wanahusika kuficha mabilioni ya fedha katika Benki za Uswisi.
Akizungumza na Majira nje ya ukumbi wa Bunge, mjini Dodoma jana, Bw. Ndugai alisema baadhi ya wabunge wanautumia vibaya ukumbi wa Bunge kwa kutoa tuhuma nzito bila kuzifanyia utafiti.
Alisema hali hiyo inalifanya Taifa liamini uongo huo ambapo hivi sasa Bunge linaangalia uwezekano wa kuzifanyia marekebisho kanuni zake ili kuwabana wabunge wenye tabia ya kuzungumza uongo na kupakazia wengine bila kuwa na ushahidi.
Aliongeza kuwa, Bw. Kabwe katika katika hotuba yake kama Msemaji wa Kambi ya Upinzani kupitia Wizara ya Fedha, alisema viongozi wa Serikali wamechota mabilioni ya fedha na kuyaficha katika Benki ya Uswisi huku akisita kuwataja kwa majina hivyo kusababisha Taifa kubaki njia panda.
“Kumezuka tabia ya baadhi ya wabunge kutumia vibaya ukumbi wa bunge na kutoa taarifa ambazo hawakuzifanyia utafiti wa kutosha hivyo kusababisha maswali mengi kwa wananchi.
“Mbunge anasimama na kusema kuna mabilioni ambayo yamechotwa na kufichwa katika Benki za Uswisi na viongozi wa Serikali lakini hawataji kwa majina au kiasi halisi cha fedha hizo...amezichota wapi, huku ni kujenga utamaduni wa kutuhumu, tabia hii imeanza kujengeka hapa nchini jambo ambalo zi zuri hata kidogo,” alisema Bw. Ndugai.
Hata hivyo, wakati Bw. Kabwe akiwasilisha hotuba yake bungeni, alisema kama kama Serikali itashindwa kuwataja kwa majina viongozi hao pamoja na wafanyabiashara wakubwa ambao wameficha fedha hizo, kambi hiyo itawataja.
Bw. Ndugai alidai kushangazwa na msimamo wa Bw. Kabwe na kusisitiza kuwa, kwanini asiwataje kwa majina pale pale kama si kutumia vibaya ukumbi wa Bunge kulingana na kinga zilizopo.
“Kama kweli Bw. Kabwe alikuwa na nia njema ya kile alichokisema kwanini hakuwataja moja kwa moja, mbele ya safari kuna umuhimu wa kupitia upya kanuni.
“Kitendo cha baadhi ya wabunge kuleta taarifa za uongo ambazo utafiti wake si mzuri, kinavunja heshima ya Bunge kwa kupakazia watu ili kuchafua upande mwingine uwe chama tawala au upinzani waonekane tofauti kwenye jamii,” alisema Bw. Ndugai.
Aliongeza kuwa ni vyema wabunge kama kuna jambo ambalo halijafanyiwa uchunguzi wa kina likaachwa badala ya kulizungumzia ndani ya Bunge.
“Huwezi kuitaka Serikali ijishughulishe na mambo ambayo haiyajui, yeye ndiye ameyaleta sasa kwanini asiyaseme badala ya kutaka maelezo,” alisema Bw. Ndugai.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment