Jeneza lake lakutwa kanisani
Tukio hilo la kutisha linalohusishwa na imani za kishirikina linadaiwa kuwa ni la pili kutokea katika vijiji vya Mwabasabi naNyehunge katika muda usiozidi mwezi mmoja.
Akithibitisha jana kuwepo kwa tukio hilo kijijini hapo, Afisa mtendaji wa kata ya Nyehunge vilipo vijiji hivyo, Daud Nomoromo ameutaja mwili wa mtoto huyo kuwa ni Seleman Chupwa, aliyekuwa na umri wa miaka miwli na miezi 6 uliopatikana jana asubuhi ukiwa umetupwa barabarani njia panda katika kijiji jirani cha Nyehunge.
Aliongeza kuwa baada ya kuonekana hapo ndipo zoezi la utambuzi lilipofanyika na baada ya kutambuliwa ilibainika ulikuwa umefukuliwa toka katika kitongoji cha Makeja kijiji cha Mwabasabi na kisha kusafirishwa na kutupwa katika kijiji jirani cha Nyehunge huku jeneza lake likiwekwa na kutelekezwa ndani ya kanisa hilo.
Alisema kutokana na kuwepo kwa matukio ya kutisha tayari imeamriwa kufanyika mkutano mkuu utakaovishirikisha vijiji viwili jirani vya Mwabasabi na Nyehunge kujadili mustakabali wake ikiwemo kuendesha zoezi la mchakato wa kuwabaini ili kurejesha hali ya amani na utulivu.
Nomoromo ameongeza kuwa jumla ya matukio matano ya ufukuaji makaburi yametokea katika vijiji hivyo kwa nyakati tofauti ndani ya mwaka mmoja hata hivyo miwili kati yake ndiyo waliyofanikiwa kuitoa miili makaburini ambapo mwezi uliopita mwishoni mwili wa mtoto mwingie wa kike ulifukuliwa na kupatikana katika shimo la majitaka.
Mwenyeikiti wa kijiji cha Nyehunge, Charles Elkana na Afisa mtendaji wa kijiji hicho, Christian Kululetela, walioratibu zoezi la uokotaji mwili huo na kisha kuuzika kwa mara ya pili kwa kushirikiana wanakijiji wa vijiji vyote viwili wamedai kuwa hali hiyo ikiruhusiwa inaweza kuhatarisha utulivu na amani.
Wamedai kuwa pamoja na mkutano huo utakaofanyika siku ya Agosti 24, kwa kushirikisha vijiji viwili kuitafuta dawa ya tatizo hilo, ulinzi wa jadi sungusungu utashirikishwa kwa nguvu na kasi mpya ili kuhakikisha kila mwanajamii anashiriki kikamilifu kuwasaka na kuwatambua wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Mara baada ya kufanyika utambuzi wanakijiji wakishirikiana na uongozi wa vijiji vyote viwili na askari wa kituo cha polisi cha Nyehunge mwili huo ulizikwa upya kwa kutumia jeneza lililokutwa ndani ya jengo la kanisa.
Mtoto huyo anadaiwa kabla ya kufikwa na kifo alitoweka nyumbani kwao na kurejea saa 4 usiku na kisha kushikwa na ugonjwa wa ghafla ambapo siku iliyofuata alifariki njiani akipelekwa katika hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema na mwili wake kuzikwa Julai mosi, mwaka huu.
Pamoja na Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, kutopatikana kuzungumzia tukio hilo lakini Mkuu wa Polisi wilaya ya Sengerema Prudenciana Protas amethbitisha kutokea kwa tukio hilo la kufukuliwa na kisha baada ya kutambuliwa kuzikwa upya na wanakijiji na kuwa uchunguzi unafanyika kuwabaini waliohusika.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment