Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA), Fadhili Manongi |
Kifaa kilichokufa kugharimu Mil.40/-
Rada ya kuongozea ndege kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere imeharibika na sasa itailazimu Serikali kutumia Sh.milioni 40/- kwa ajili ya kuagiza kifaa cha mfumo wa kusambaza umeme kilichopata hitilafu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA), Fadhili Manongi, alithibitisha rada hiyo kutokufanya kazi na kueleza kuwa kifaa kinachoitwa Power Supply Unit kimeharibika.
Kifaa hicho ambacho ni sehemu ya vifaa vinavyosaidia shughuli za kuongoza ndege ,kimezimwa kutokana na hitilafu zilizojitokeza.
Rada hiyo ni ile ambayo ilinunuliwa kwa Dola za kimarekani milioni 40 na Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Silaha ya BAE Systems ya Uingereza na imekuwa haifanyi kazi tangu Agosti 3, mwaka huu baada ya kutokea hitilafu katika kifaa cha kuingizia umeme katika rada hiyo.
Ununuzi wa Rada hiyo ulizua mjadala mkali na kusababisha wabunge mara kwa mara kuhoji gharama kubwa za ununuzi wake.
Sakata hilo lilimfanya aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Clare Short wakati wa Serikali ya Waziri Mkuu Tony Blair, kujiuzulu akipinga Uingereza kuiuzia nchi maskini kama Tanzania rada hiyo kwa bei kubwa.
Kashfa hiyo kwa muda mrefu pia imekuwa ikitajwa kumhusisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Andrew Chenge, ambaye pia aliwahi kukutwa na kiasi cha Sh. 1.2 bilioni, kisiwani Jersey, ambazo Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza, ilikuwa ikichunguza kama zilikuwa na uhusiano na biashara hiyo.
Manongi aliwaambia waandishi wa habari kuwa ni wiki ya tatu sasa kifaa hicho hakifanyi kazi ambapo wahandisi na wataalamu walibaini tatizo hilo wakati wakifanya ukaguzi wao.
Hata hivyo, Manongi alisema hakuna madhara yoyote yaliyotokea kutokana na kifaa hicho kuharibika kwani marubani hawajaeleza matatizo yaliyotokea tangu kuharibika kwa kifaa hicho.
Alisema baada ya kutokea kwa tatizo hilo waliamua kuzima mtambo huo na kuwasiliana na Kampuni ya Uingereza ili kuwapa kifaa hicho.
Manongi alisema kifaa hicho kitagharimu Sh milioni 40 na kinaagizwa kwa oda maalumu, kitendo kitakachosababisha kutumia muda kidogo kukipata. "Sio kwamba ukiagiza unakikuta kipo tayari wanapokea oda kwenye kampuni ambayo iliyotuuzia rada hiyo hatujajua kitatumia muda gani kuwasili nchini," alisema.
Alisema badala ya kusubiri kifaa hicho kitoke Uingereza, Jumatatu watakipeleka kifaa kilichoharibika nchini Afrika Kusini ili kifanyiwe matengenezo kwa ajili ya kuendelea na shughuli zake.
Alisema uamuzi wa kukipeleka Afrika Kusini ni njia mbadala ya kusubiri kifaa kipya kwa kuwa Uingereza wanatoa kifaa kipya.
Alisema kampuni hiyo ya BAE tayari imeshaanza mchakato wa kukitafuta kipuri hicho.
Alisema kuzimwa kwa mtambo kama huo ni kawaida kwani wahandishi hulazimika kupanda katika antena kwa ajili ya kuweka mafuta mazito.
Manongi alisema pamoja na kuharibika kwa kifaa hicho ambacho ni muhimu bado huduma za usafiri wa anga zinaendelea vizuri na waongoza ndege wanaendelea kutumia taratibu nyingine.
Alisema wamejipanga kuhakikisha hakuna madhara yoyote yatakayotokea kwa kuwa njia mbadala ya mawasiliano katika kuendesha ndege hizo pamoja na redio call zinatumika.
Akizungumzia kuhusu usalama wa anga alisema tangu kuharibika kwa kifaa hicho usalama wa watu unaangaliwa ndio maana mpaka sasa hakuna matatizo yaliyotokea.
"Sio mara ya kwanza kuharibika tumekuwa tukibadilisha vipuri katika mtambo huo kwani ni mara nyingi hivyo ni jambo la kawaida kufanya matengenezo na isitoshe rada hiyo kwa sasa inafikisha miaka 12 tangu iliponunuliwa mwaka 2000," alisema.
Alisema suala la huduma ya anga halitegemei rada peke yake na kwamba kuna njia mbalimbali ambazo zinawezesha huduma hiyo kuendelea.
Aidha alisema hatua nyingine walioifanya ni kutoa taarifa kwa wadau wa usafiri wa anga kote duniani juu ya kuzimwa kwa mtambo huo.
Alisema suala la usafiri wa anga nchini linapewa kipaumbele cha pekee kulingana na taratibu za Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICOA).
Tayari Serikali imeshapokea Pauni milioni 29 za malipo ya fidia kwa Serikali ya Tanzania na imekubaliwa fedha hizo zitumike kununua vitabu na madawati kwa shule za msingi na sekondari nchini.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment