ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 23, 2012

Bashe, Kigwangalah wapigwa panga CCM

SEKRETARIETI YADAIWA KUPENDEKEZA WAKATWE,VURUGU ZA NZEGA ZAWAPONZA,WABUNGE,MAWAZIRI SASA RUKSA KUWANIA UONGOZI
Waandishi Wetu
MAKALI ya panga la Sekretarieti ya CCM, yameanza kuonekana baada ya majina ya wagombea wa nafasi ya Halmashuari Kuu (Nec) ya chama hicho kupitia Wilaya ya Nzega, Mbunge wa Jimbo hilo,  Dk Hamis Kigwangalah na Mjumbe wa Mkutano Mkuu, Hussein Bashe kukatwa.

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka Dodoma zinaeleza kuwa Sekretarieti ya CCM iliyoketi hivi karibuni, kupitia majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho ikiwa chini ya Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama iliamua kuyaondoa majina ya Kigwangalah na Bashe kwa madai kuwa wamekiabisha chama hicho.


Habari nyingine kutoka mjini humo zinaeleza kuwa Sekretarieti ya CCM pia imepitisha majina matatu ya watakaowania nafasi ya umakamu mwenyekiti wa UVCCM, Tanzania Bara.

Wanaotajwa kupitishwa ni pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dodoma, ambaye pia ni Wakili wa Kujitegemea Anthony Mavunde, Paul Makonda na Mboni Mhita.

Bashe na Kigwangalah waliingia katika mvutano wakati wakichukua fomu ambapo kulitokea malumbano baina yao wakiwa katika Ofisi za CCM, mjini Nzega na kusababisha kutoleana bastola.

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani Tabora lilieleza kuwa linaishikilia bastola ya Mbunge Kigwangalah na kwamba, wanafanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

Mbali ya tukio hilo kufikishwa polisi, Kamati ya Siasa ya CCM wilayani Nzega iliketi na kutoa mapendekezo kadhaa, ambayo yalimbana Kigwangalah, ambaye aliibuka na kueleza kuwa hana imani na viongozi hao, akiwatuhumu kuwa wanampendelea Bashe.

Uamuzi wa kuenguliwa kwa makada hao wa CCM katika kinyang’anyiro hicho, ambao ulikuwa umeenea miongoni mwa baadhi ya wafuasi wa chama hicho wilayani Nzega, unadaiwa kuchukuliwa na sekretarieti ya chama hicho kwa maelezo kuwa kitendo walichokifanya kinakiabisha chama hicho.

Habari zinadokeza kuwa, wakati wakijadili hoja hiyo, wajumbe wa sekretarieti hiyo wakiwamo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na John Chiligati walikwenda mbali zaidi kumbana Bashe wakieleza kuwa hana msaada kwa chama hicho, ingawa anaendesha chombo cha habari.

Hii itakuwa mara ya nne kwa Bashe kuondolewa jina lake katika kinyang’anyiro cha kusaka uongozi ndani ya chama hicho.

Mwaka 2007 wakati akigombea ujumbe wa Nec Taifa, jina lake liliondolewa na baadaye wakati akigombea uenyekiti wa UVCCM, ambapo uchaguzi huo ulifutwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na kuamriwa nafasi hiyo igombewe na watu kutoka Zanzibar.

Katika mwaka 2010 wakati akiwania kiti cha ubunge kupitia chama hicho Jimbo la Nzega, jina lake lilikatwa kwa madai kuwa siyo raia.

Nape
Nape alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kuwa Sekretarieti hiyo haina uwezo wa kuengua majina ya wagombea.

“Sekretarieti haina mamlaka ya kuengua majina ya wagombea,” alisema Nape huku akisisitiza kuwa kama ikifanya hivyo, basi ni kinyume na Katiba ya CCM.

Dk Kigwangalah, Bashe
Hata hivyo, kwa upande wake Mbunge Dk Kigwangalah alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kuwa hata yeye anazisikia taarifa hizo, lakini hajapata taarifa rasmi.

“Siwezi kuthibitisha wala kukanusha kwa sababu mimi siyo mjumbe wa kikao kilichoketi na kufanya uamuzi, labda uwaulize waliokuwepo katika kikao hicho,” alisema Kigwangalah na kuongeza:

“…Sidhani kama nitakatwa, kwa sababu mimi nina uwezo mkubwa wa kuwa mjumbe wa Nec, hata viongozi wangu wanajua uwezo wangu.”

Alipoulizwa hatua atakazozichukua iwapo atapewa taarifa rasmi kuwa ameenguliwa kugombea nafasi hiyo alisema: “Unajua, huwezi kuzungumza habari za mto wakati bado hujauvuka.”

Bashe alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alisema kuwa, hana taarifa za jina lake kufutwa.

Mbali na Bashe na Kigwangalah, sekretarieti hiyo pia inadaiwa kukata majina ya makada wengine waliokuwa wakiwania nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho kutokana na kukumbwa na kashfa mbalimbali.

Tayari uchaguzi huo ndani ya CCM umegubikwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa baadhi ya makada wakidai kuwa kuchezewa faulo, huku majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali yakijadiliwa na kikao cha Nec mjini Dodoma.

Mmoja wa makada hao ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono anayegombea nafasi ya uenyekiti Jumuiya ya Wazazi Taifa, ambaye jina lake linadaiwa kukatwa katika ngazi ya mkoa na kuonya kuwa kama hiyo itafanyika basi patachimbika.

Kada mwingine ambaye ameunyooshea kidole uchaguzi huo ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye juzi alikaririwa akisema kuwa chaguzi zinazoendelea ndani ya CCM, zimevurugika kwa kuwa mafisadi wameingilia na kuweka watu wao kwa lengo la kulinda masilahi yao.

Alisema kuwa watu waliojitokeza kugombea ni mapandikizi na vibaraka wa mafisadi hao.

"Hivi karibuni tumepata aibu kubwa ndani ya chama chetu, wakati  chaguzi zetu zikiendelea, viongozi wamepitisha vipaza sauti vya mafisadi, kazi yao kubwa ni kulinda masilahi ya mabwana zao na kuwafurahisha," alisema Sitta.

Kujirundikia vyeo ruksa
Katika hatua nyingine, mkakati wa CCM wa kuondokana na baadhi ya wanachama wake na kujirundikia vyeo umeonekana kugonga ukuta baada ya chama hicho kueleza kuwa, busara zinahitajika zaidi kuliko uhalisia ili mkakati huo uweze kufanya kazi.

Hali hiyo ya imekuja wakati ambapo chama hicho kupitia vikao vyake vya juu, kiliwahi kutangaza kuwa watu wenye nafasi nyingine wakiwemo wabunge, madiwani na mawaziri, hawataruhusiwa kugombea nafasi zaidi za uongozi ndani ya chama.

Akionyesha kuwa chama kimebadili msimamo huo ulio kwenye Katiba yake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alitoa ufafanuzi mbele ya waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuhusu wabunge na mawaziri kugombea nafasi za ujumbe wa Nec, huku wakiwa wana shughuli zingine.

“Ni kweli, tulipanga kufanya hivyo na hilo siyo geni, lakini kumbukeni nia ya chama chochote ni kushinda na kushika dola hivyo tukisema kwamba tukate majina ya kila mtu hatutakuwa tumetenda haki, tunaweza kujiangusha sisi,’’ alisema Nape.

Alisema kuwa wako watu ambao ni muhimu kwa chama na kuwa, kuwaondoa katika nafasi zao inaweza kuwa ni tatizo kwa CCM na wananchi wanaowazunguka.

Katibu huyo alisema kuwa kwa namna yoyote, wako mawaziri na wabunge watahitajika  kuteuliwa na kugombea kutokana na umuhimu wao ndani ya chama na kuwa CCM haiwezi kuwatema.
Akitoa mfano alisema kuwa Dann Makanga aliyehama kutoka chama cha UDP na kujiunga na CCM, aliteuliwa kwa wakati huohuo kuwa mgombea na alishinda, uamuzi ulioonyesha kwamba asingeteuliwa kungekuwa na madhara.
Mpango wa CCM kuzuia wanachama wake kujirundikia vyeo, ulilenga kuwazuia kugombea nafasi zaidi baadhi ya watumishi wa Serikali, wanaokuwa na majukumu ya kila siku, ili kutoa nafasi kwa wajumbe wengine kukitumikia chama hicho kwa uaminifu na uadilifu.
Kuhusu uamuzi wa kukatwa majina, Nape alisema kuwa CCM haina kigugumizi na hilo akitolea mfano wa waliokuwa wagombea wa Uenyekiti wa Mkoa wa Mara, Chambili na Gachuma, aliosema majina yao wote yalikatwa na kutangaza nafasi hizo upya.
Akizungumzia ratiba ya vikao vinavyoendelea kiongozi huyo alisema kikao cha Kamati ya Maadili juzi hakikumaliza shughuli zilizopangwa kufanyika, hivyo kuendelea jana asubuhi.
Alisema hali hiyo ililazimu kikao cha Kamati Kuu (CC) kilichopangwa kufanyika jana asubuhi kisogezwe hadi jana jioni.
Kikao cha CC kinatarajia kukamilika leo kabla ya kupisha kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, kitakachofanyika kwa siku mbili kuanzia kesho na kutoa mapendekezo ya mwisho, kabla ya kufanya uteuzi wa wagombea.

Mwananchi

No comments: