ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, September 25, 2012
Kwenye mapenzi kuna virusi, unapaswa kujua ‘kuskani na kudiliti’-2
BUSARA, hekima na moyo imara ni vipengele vikuu vitakavyokuwezesha kuvuka changamoto mbalimbali kwenye mapenzi. Fikiria kwamba hata barabara iliyochongwa vema na wahandisi waliobobea, bado milima na mabonde vitakuwepo.
Kama ndivyo, basi inashindikana vipi kutokea kwa hali isiyoeleweka kwenye mapenzi? Ni mambo ya kawaida mno, kwa hiyo busara na hekima view ndani yako. Vilevile moyo imara ukupe nguvu ya kuvuka changamoto za hapa na pale.
Unatakiwa uwe mwepesi kukubali matokeo. Inapotokea umejikuta upo kwenye uhusiano na mtu mbaya, basi ikupe sababu ya kuona kwamba ni bahati kukutana naye ili akupe elimu ya uhusiano. Utajuaje kasoro za kimapenzi kwa mtu wa ovyo ikiwa hujakutana naye?
Hapa simaanishi kwamba watu wawe wanajaribu mapenzi kwa lengo la kuonja tamu na chungu kwenye mapenzi. Namaanisha kuwa wakati mwingine mtu mbaya humfanya mwathirika awe na mapenzi mazuri kwa mpenzi wake anayefuata.
Unaweza kumchezea ‘faulo’ mwenzi wako. Ukawa kichwa ngumu hata pale anapokuwa anakuelekeza usahihi wa namna ya kuishi kimapenzi. Huyo anakuwa na kiburi kwa sababu hajawahi kukutana na mapenzi ya Jengua. Vuta kumbukumbu ya namna Jengua alivyokuwa anaishi na mke wake kwenye mchezo wa Kidedea.
Aina ya watu kama Jengua (yule wa kwenye maigizo) ni vizuri wakawepo kwa sababu wanasaidia kutoa masomo mazuri. Wengine ni kama Tomaso, eti kila kitu mpaka waone ndiyo waamini. Wanapotendwa, hukumbuka mambo matamu ya mpenzi aliyemletea kiburi.
Unakuwa kiburi kwa mwenzi wako, baada ya kuachana unakwenda kukutana na Jengua. Anakutenda inavyotakiwa mpaka unakoma. Sasa ndiyo unakumbuka yale yote uliyokuwa unamfanyia mpenzi aliyekupenda, kukujali na kukunyenyekea.
Mapenzi ni akili na utulivu. Usithubutu kuwa kama ndugu yangu Yohana, kwa tamaa yake ya kutaka kumiliki wanawake wawili, wakamuumiza kichwa. Walipogundua kichwa chake kimefeli, wakamchezesha sindimba. Ngoma inapigwa huku na kule hajui aende wapi.
Kama wanaambiana vile, mwanamke huyu analianzisha kivyake, eti anamhitaji haraka, mwingine naye anamtaka. Wote wanamfuata kijiweni, kila mmoja anataka aondoke naye. Yohana kajaziwa watu na wapenzi wake. Naye hajui aende wapi, akatae wapi.
Mwisho Yohana akawa mwendawazimu. Akipita barabarani anazungumza peke yake, wanawake wamemfanya awe mwehu. Hii siyo simulizi ya kufikirika, ni tukio ambalo lilimtokea ndugu yangu kwa tamaa ya kutaka kumiliki mabibi wawili kwa wakati mmoja.
Kuna mtu hana hamu. Anaishi kwa tabu kwa sababu ya mateso anayopewa na mpenzi wake. Sasa jiulize, ikiwa mpenzi mmoja anaumiza kichwa namna hiyo, inakuaje ukiwa na wengi? Ikae akilini kwako kwamba kadiri wapenzi wanavyoongezeka na matatizo nayo hukuandama.
Sasa basi, unapoona mwenzi wako anakutesa, usikimbilie kujirundikia wapenzi. Wapo wanaamini kuwa ukiwa na wengi ni vizuri. Eti, mmoja akikutibua, utakwenda kujiliwaza kwa mwingine. Waliofuata kanuni hiyo, wote wamefeli. Mwenzi wako akikuudhi tafuta suluhu, ukiona umechoka, vunja uhusiano kabla ya kuanzisha mwingine.
Wakati unachukua uamuzi huo, hakikisha akili yako haisumbuliwi na mawazo. Usithubutu kulia kwa maana machozi hayakupi ufumbuzi. Badala ya kujuta, wewe furahia pumzi yako. Usimuwaze tena yeye, bali mtafakari mtarajiwa wako. Tumaini kwa mazuri.
Wakati unatafakari kuhusu mtarajiwa wako, zingatia kwamba inawezekana umepangiwa kukutana na mwenzi ambaye siyo sahihi ili ujue utamu wa ngoma. Kwamba utakapokutana na mpenzi bora, umheshimu, umtunze na kumthamini kwa kiwango kinachotakiwa.
Unajuta nini? Mpenzi bora ni zawadi kutoka kwa Mungu. Dunia yetu ilivyo chafu, inakuwa ngumu mno kupata mwenzi sahihi. Wengi wameharibiwa na sukari inayonakshi ardhi ya dunia, ndiyo watu wazuri kwenye mapenzi ni wa kuokoteza. Kazi sana.
Maisha yanakwenda mbio sana, kwa hiyo utapoteza muda wako bure kukaa umejiinamia kwa ajili ya mpenzi asiyekufaa. Usilie, bali mshukuru Mungu kwamba sasa umejifunza kitu kwa maisha yako yajayo. Tuliza akili halafu jipange kumpa furaha mwenzi wako ajaye.
Ni maisha yako, ukifeli maana yake ni hasara yako mwenyewe. Utashindwa kufanya kazi zako vizuri kwa sababu ya kulilia mapenzi. Ni sawa una haki ya kuumia kwa sababu umetendwa lakini hiyo haiwezi kuwa dawa. Piga moyo konde halafu tazama mbele. Maisha yanakudai.
Siku zote unatakiwa kujua namna ya ‘kuskan na kudiliti’, virusi ni vingi na vipo katika sura nyingi kwenye mapenzi. Hakikisha unakuwa mwangalifu.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment