ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 25, 2012

Kikwete awashukia wapinzani wa CCM *Adai wanaokiombea kife watakufa wao *Hatima ya wagombea kujulikana kesho


Na Pendo Mtibuche, Dodoma

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Jakaya Kikwete, amesema kamwe chama hicho hakitakufa na wanaokiombea kife, watakufa wao na kukiacha kikiwa hai.


Rais Kikwete aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akifungua Kikao cha Kamati Kuu (CC) na kuongeza kuwa kikao cha Kamati ya Maadili kilichomalizika jana saa tisa usiku, kilikuwa na jukumu la kupitia majina mengi ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.

“Dhamira yetu ni kutenda haki kwa wagombea wote walioomba nafasi husika ambao walikuwa wanafikia 5,000, hivyo wajumbe wa Kamati ya Maadili wametumia muda mwingi kuyachambua,” alisema Rais Kikwete.


Aliongeza kuwa, kikao hicho kimeweza kufanya mabadiliko tofauti na yale yaliyotoka mikoani kwa kupitia majina ya waliopitishwa kugombea Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kutoka mikoani wengi wao wakiwa wasomi.

“Tumejaribu kujihoji wenyewe kwanini huyu kapewa alama hii na yule kanyimwa ndio maana nasema kasi haikuwa ndogo kupitia jina moja moja na kutoa mapendekezo,” alisema.

Rais Kikwete alisema madadiliko ya utoaji alama kwa wagombea yatarahisisha uteuzi wa majina katika kikao cha NEC ambacho kinatarajiwa kufanyika kesho.

“Kikao cha kamati ya maadili kilikuwa kikubwa zaidi kilichohitaji umakini mkubwa, lengo ni kupitia majina kwa usahihi lakini kikao cha NEC natarajia kitakuwa chepesi na kitaisha mapema,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, kikao cha NEC kitakuwa na kujumu la kupitisha majina ya wagombea wanaofaa.

Majira

No comments: