Rose Itono na Kassim Mahege
HATIMAYE Jeshi la Polisi mkoani Kinondoni, limeandika barua kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kuomba kibali cha kufukua mwili wa marehemu, Ntimaruki Khenzidyo, ambao ulitolewa Hospitali ya Mwananyamala na kusafirishwa Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, John Mtalimbo, alisema taratibu za kuandika barua hiyo zimefanyika wakisubiri majibu kutoka kwa hakimu.
Alisema baada ya Mahakama kutoa kibali cha kufua mwili huo, ndugu wa marehemu wataondoka kwenda Handeni ambapo watashirikiana na polisi wa huko kufanya kazi hiyo.
Aliongeza kuwa, kazi hiyo itafanywa kwa kushirikisha ndugu waliozika mwili wa mtu ambaye si ndugu yao na mwili uliopaswa kuzikwa Tanga, umesafirishwa na mazishi yamefanyika juzi.
“Mwili wa marehemu aliyezikwa Tanga haukuibiwa bali ni makosa ya uhakiki hivyo jamii ielewe wazi kuwa taratibu zote za kisheria kwa ajili ya kuutoa zilifuatwa,” alisema.
Kamanda Mtalimbo alisema jeshi hilo linategemea gari iliyopeleka maiti kwa ajili ya mazishi mkoani Tanga, ndilo litarudi na jeneza la maiti iliyozikwa kimakosa.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala Dkt. Sofinius Ngonyani, alisema taratibu za kawaida kuhusu utoaji maiti mochari, zilifuatwa ambapo askari, ndugu wa marehemu na madaktari walikuwepo wakati uchunguzi ukifanyika.
“Nasikitika kusikia vyombo vya habari vimeandika maiti imeibiwa ukweli ni kwamba haijaibiwa bali ndugu walijichanganya kwenye uhakiki,” alisema Dkt. Ngonyaini.
Alisema siku ya tukio, hospitali hiyo ilipokea maiti mbili tu za ajali zilizotokea Tegeta na Kawe ambapo marehemu wote majina yao hayakuweza kutambulika.
Aliongeza kuwa, mwili wa marehemu Khenzidyo ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Ulinzi ya Group 7, ulifikishwa hospitalini hapo na wafanyakazi wenzake ambao walikuwa hawamfahamu mwenzao kwa majina.
“Utaratibu wa kufahamu jina la marehemu ulifanyika muda mfupi baada ya bosi wake kufika hospitalini na kumtambua ambapo siku ya kuchukua maiti ndugu wa marehemu walikuwepo hospitalini na taratibu zote zilifuatwa,” alisema.
Awali taarifa zilizoandikwa katika vyombo vya habari zilidai kuwa, hospitali hiyo imeingia katika kashfa ya mwili wa marehemu Ntimaruki kupotea mochari katika mazingira ya kutatanisha.
Majira
No comments:
Post a Comment