ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 25, 2012

Mama Salma Kikwete katika mkutano wa wake wa viongozi wa Afrika, New York, Marekani


 Mama Salma Kikwete akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe Mwanaidi Sinare Maajar, Balozi wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa Mhe. Amina Salum Ali na Mshauri wa Rais  mambo ya Diplomasia Balozi Liberata Mulamula kabla ya kuhudhuria mkutano wa  African First Ladies Roundtable jijini New York, Marekani, leo
 Mama Salma Kikwete akibadilishana mawazo na   Bibi Katalin Bogyay Balozi wa  Hungary UNESCO na amebobea katika diplomasia ya utamaduni  na mtetezi mkubwa wa masuala yahusuyo  fursa sawa ya elimu kwa mtoto wa kike.
Na  Mwandishi Maalum
 Mke wa Rais  Mama Salma Kikwete , amesema tekinolojia  ya mawasiliano ya simu za mkononi,   kama ikitumiwa vema,  inaweza kuwa chombo muhimu katika  kuchagiza na kuwaletea maendeleo ya haraka   wanawake na wasichana  hususani  wale  wa vijijini.
Mama Kikwete ameyasema hayo, wakati alipokuwa akitoa mchango  wake katika  majadiliano ya  kwanza na  ya  aina yake.

Kwa habari na picha zaidi bofya read more

Majadiliano  yaliyowaleta meza moja,  baadhi ya wake wa marais,  wakurugenzi wa  makampuni,wahadhiri na wanadiplomasia, kujadiliana na kubadilishana  mawazo  na mbinu zitakazoweza kuwahamasisha watoto wa kike kuchangamkia masomo ya Sayansi,  Tekinolojia, Uhadinsi na Hesabu ( STEM)
 Majadiliano hayo  ambayo yalifunguliwa na Bi. Anitta Kalinde,  Waziri wa Masuala ya Jinsia kutoka Malawi kwa niaba ya Rais wa Malawi.Yamefanyika siku ya jumatatu katika ukumbi wa mikutano wa  jengo la  Credit Suisse, Jijini New York.
Aidha Majadiliano hayo , yalilenga pia kuwachagiza viongozi hao kutumia  nafasi    walizo nazo,  uelewa wao na uwezo walionao  katika  kuwasaidia wanafunzi wa kike  kung’amua mapema  vipaji vyao na hivyo kupata fursa ya  kuvitumia  vipaji hivyo kufikia malengo, matarajio na ndoto zao kuhusu maisha yao ya baadaye.  
Kupitia teknolojia ya simu za mkononi, Mama Salma  amebainisha kwamba kwa nchi za Afrika ikiwao  Tanzania, siyo tu kwamba ni tekinolojia rahisi ya mawasiliano lakini inawawezesha wanawake,   kubuni na kuanzisha miradi ya kiuchumi kwa kuwa mawasiliano hayo yanawapa fursha ya kupata habari na kubadilishana mawazo na makundi mbalimbali ya jamii.
 “ Ninawashukuru kwa kunialika katika   majadiliano haya, lakini kilichonifurahisha zaidi ni mada yenyewe.   Tunahitaji kukusanya nguvu zetu, uwezo wetu na maarifa yetu kuwasaidia wanawake na wasichana wa vijijini kunufaika na tekinolojia rahisi zilizopo kujiletea maendeleo yao na kuondokana na umaskini”. Akasema Mama Salma
Na kuongeza,  tekinolijia hiyo ya simu za mkononi ni mfano mmoja tu lakini zipo teknolojia nyingi na rahisi ambazo kwazo zinaweza kuwanufaisha wanawake na wasichana  ikiwa watapewa na kuwezeshwa  kujifunza masomo ya sayansi, hesabu, uhandisi na tekinolijia.
Na  kwa sababu hiyo, Mke wa Rais amesema,  ili wanawake na wasichana wanaweze kunufaika na teknolijia zilizopo kunahitajika  ushirikiano na ubadilishanaji wa mawazo na uzoefu wa namna bora ya kuwasaidia.
“Wito wangu kwetu sote tuliokusanyika hapa, ni  huu,  tujenge mitandao, tubadilishane uzoefu,  na utaalamu wa kuwasaidia wanawake na watoto wa kike na kwa upande mwingine kuwapa fursa wanawake na wasichana nao kutembeleana na kujufunza  baina yao”. Akasisitiza.
Aidha amesema kwa kutambua umuhimu wa wasichana  kupata elimu, ikiwamo  maarifa na ujuzi mbalimbali.  Yeye  binafsi kupitia  taasisi  yake ya wanawake na Maendeleo  ( WAMA) imekuwa mstari  katika kuwasaidia watoto wa kike kufikia malengo yao.
Akatumia nafasi hiyo,  kuwakaribisha   wajumbe wenzie   kutembelea Tanzania na kujionea jitihada mbalimbali zinazofanywa  na Serikali na WAMA katika  kusukuma mbele maendeleo ya wanawake na watoto wa kike.
Katika maajadiliano hayo, baadhi ya  washiriki   akiwamo  Bibi Savanna Maziya ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa   Kundi la Makapuni ya Bunengi ( Bunengi Group of Companies), na mwanzilishi wa majadiliano hayo,  wameonyesha nia ya kuja Tanzania  kutambua maeneo ya ushirikiano hususani katika eneo hilo la kuwasaidia na kuwawezesha  watoto wa kike  kumudu masomo ya STEM.
Tayari  Bibi Savanna  kupitia Kampuni yake ameanza kuwasaidia wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu kumudu na kuyakabili masomo ya sayansi katika baadhi ya  shule nchini  Marekani,  na tayari ameanza kuona mafaniko makubwa kwa watoto hao kufanya vizuri
Aidha  Dkt, Herta von Stiegel,   Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa   Kampuni ya Ariya Capital Group Limited yeyé, na  ambaye tayari kampuzi yake imeanza kuwekeza nchini Tanzania  katika uvunaji wa umeme wa upepo. Anasema kwa kadri hali ya mabadiliko ya dunia  yanavyoendelea, Afrika  inabaki kuwa ndilo bara  lenye  raslimali nyingi zikiwamo za ardhi, madini  na nguvu kazi kubwa.
Akasema  wakati idadi ya watu ikipungua katika nchi zilizoendelea, idadi ya watu inaongezeka  barani afrika   na kwa sababu hiyo akashauri kwamba  idadi ya watu inayoongezeka barani afrika inapaswa kutumika si tu kama nguvu kazi, bali yenyewe  iwezeshwe ili ichukue nafasi ya kuendesha uchumi na maendeleo ya  nchi zao.
 Dkt. Stiegel amesema huu ni wakati muafaka pia kwa makapuni ya kibiashara kutafuta fursa za uwekezaji  nchini Tanzania, nchi ambayo ameitaka kama yenye vivutio vingi vya uwekezaji.
 Mama Salma Kikwete akihudhuria mkutano huo
 Baadhi ya washiriki


 Mama Salma Kikwete akipokea vipeperushi katika mkutano huo
 Mama Kikwete akisalimiana na baadhi ya washiriki
 Picha ya pamoja





SIMU ZA MKONONI ZINAWEZA KUWAKOMBOA
 WANAWAKE KIUCHUMI - SALMA KIKWETE

No comments: