ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 8, 2012

MAPENZI NI AFYA, NENDA VIZURI YAKUONGEZEE SIKU ZA KUISHI -3

UNAHITAJI kujua thamani na umuhimu wa mapenzi. Hupaswi kwenda mbio, matokeo yake huwa ni mabaya. Siku zote kaa ukitambua kwamba mapenzi yanaweza kukufanya uishi maisha marefu, vilevile yakikuendea ndivyo sivyo, yatafupisha siku zako za kuishi.
Mada hii ina lengo la kukufanya uyaelewe mapenzi. Si kukimbilia kuacha pale kunapotokea tofauti za hapa na pale na mwenzi wako wa maisha. Uvumilivu unahitajika, amini kwamba utamu wote unaoyazunguka ‘malavidavi’ kuna ugumu mkubwa.

Ni sehemu ya tatu. Hapa tunazungumzia elimu zaidi inayoweza kukukomboa wewe kwa kuheshimu hisia za mwenzako na wakati huohuo ukawa unajali za kwako. Kwa pamoja ndipo utaweza kufanikiwa kuwa na moyo tulivu katika nyakati zote. Ukiwa na moyo tulivu ndivyo unavyoweza kuongeza siku za kuishi.
Ukiheshimu hisia za mwenzi wako na ukawa unajali za kwako, itakusaidia kukufanya uwe na tumaini chanya wakati wote. Wakati wa matatizo, hasa kipindi ambacho hampo kwenye maelewano mazuri, utabaki na imani kwamba yote yatakwisha.
Penda kuamini kuwa ‘hili nalo litapita’ kwamba wakati ambao mwenzi wako amenuna, hataki kuzungumza na wewe, unachopaswa kufanya ni kuheshimu hisia zake na uamini kwamba mwisho atatulia na uhusiano wenu utaendelea kwa maelewano makubwa.
Ni ukweli ulio wazi kuwa hakuna kitu kinachouma sana siku zote kama kupenda sehemu ambayo unaamini utapenda kama upendavyo wewe. Vilevile kingine kinachotesa moyo ni kumpenda mtu halafu asijue au kuheshimu thamani ya penzi lako kwake.
Maisha ni fumbo zito, kwa hiyo hutokea kukutana na mtu ambaye siyo sahihi. Inawezekana pia ni mipango ya Mungu kwa mwanadamu kutumbukia kwa mtu ambaye siyo sahihi. Inaweza ikawa pia majaribu ya Shetani. Unajua Shetani ni msumbufu sana.
Wakati mwingine, hali ya kukutana na mtu ambaye siyo sahihi, imesababisha matokeo chanya, kwamba mtu anapoachana na yule aliyemtesa, anaweza kuwa makini mno kwenye uhusiano wake wa baadaye. Haya tumeyaona sana.
Asimuliaye mvua, imemnyeshea. Kutokana na uzoefu huo, siku akiona mawingu atakuwa makini kutafuta hifadhi. Vivyo hivyo, aliyeteseka (kwa kutendwa) au aliyeachwa (baada ya kumtenda mwenzake), ni wajenzi wazuri wa uhusiano.
Hii ni kwa sababu wanajua athari iliyo kinyume chake. Wapo ambao hawakubali kufanya mchezo kama wa mwanzo. Ila wapo vichwa ngumu ambao maumivu yaliyopita hawayazingatii. Hawakosekani, ndiyo maana nakutaka wewe ucheze salama. Mapenzi ni matamu.
Naomba nimalizie mada hii kama nilivyoanza kwa kukutaka uchanganue mambo inavyotakiwa, kadiri unavyoyafanya maisha yako kuwa na majanga, ndivyo na umri wako unavyoufupisha. Hii ikupe changamoto ya kuchagua jema kati ya mambo mawili. Kuongeza siku za kuishi au kuzipunguza.
Mantiki hapa ni namna ya kuyatumia mapenzi ili kupata umri kulingana na namna utakavyokadiriwa na Mwenyezi Mungu. Vilevile, ni jinsi unavyokwenda kinyume nayo, matokeo yake yakakufanya umri wako upungue. Nimefafanua vizuri, tazama na mifano katika eneo unaloishi.

www.globalpublishers.info

No comments: