Salma Said, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imewataka viongozi wa serikali za mitaa kujiepusha kuwa chanzo cha migogoro mbali mbali inayotokana visiwani Zanzibar kwani inahatarisha amani na usalama.
Kauli hiyo imetolewa jana na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad wakati wa semina maalum kwa ajili ya Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Masheha na Madiwani kuhusu uhusiano baina ya viongozi wa kisiasa na utendaji katika serikali za mitaa Zanzibar huko Wesha, Mkoa wa Kusini Pemba.
Kauli hiyo imekuja kufuatia Madiwani kulalamika mbele ya Rais na Maalim kwamba baadhi ya masheha wamekuwa wakitumia nafasi zao vibaya kwa kuwanyima wananchi wenye haki ya kupata vitambulisho vya mzanzibari mkaazi huku lawama kubwa ikielekezwa kwa wakuu wa mikoa na wilaya wenye mamlaka ya kuwateuwa masheha hao.
Semina hiyo imefunguliwa na Dk Shein lakini alimpa nafasi ya kuongea Maalim Seif ambapo alizitaka Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya kuzitangia uwezo wa mtu badala ya itikadi au chama cha siasa anachotoka wakati wa kupendekeza majina ya watu wanaotakiwa kuteuliwa kuwa Masheha.
Alisema yapo malalamiko mengi kuwa Masheha wote wanatoka chama kimoja, jambo ambalo huwafanya baadhi ya wananchi hapa Zanzibar kuhisi kuna ubaguzi dhana ambayo haifai wakati huu wa serikali yenye muundo wa umoja wa kitaifa.
Maalim Seif alisema ili kuondoa dhana hiyo mbaya Kamati za Ulinzi na Usalama ambazo ndizo zenye jukumu la kupendekeza majina ya Masheha zinapaswa kufanya uadilifu na kuzingatia uwezo wa mtu kiutendaji katika kutumikia wananchi.
“Malalamiko hayo ni kweli yapo, inasemwa hata nafasi za ajira ya kupuliza dawa za kuulia mbu wa malaria majumbani hupewi hadi uwe unatoka chama fulani”, alisema Maalim Seif.
Alieleza kuwa Sheha anatakiwa awe mtu anayeheshimika miongoni mwa jamii na wananchi anaowaongoza lazima wawe hawana shaka na uadilifu wake.
Maalim Seif alisema hayo, baada ya Madiwani kutoka Wadi mbali mbali kisiwani Pemba kulalamika juu ya kuwepo ubaguzi katika uteuzi wa Masheha na Kamati zao za wajumbe 10, hali ambayo inachangia kuporomoka utendaji na ushirikiano kati yao na Madiwani.
Akijibu hoja za Madiwani hao Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba, Meja Mstaafu, Juma Kassim Tindwa alisema kuwa Wakuu wa Mikoa hufanya uteuzi wa Masheha baada ya kupewa majina matatu yanayopendekezwa na Kamati za Ulinzi na Usalama katika Mikoa yao.
Alisema kuwa hakuna upendeleo wowote unaofanywa katika kupata viongozi hao wa serikali za mitaa, kwa vile kamati hizo za ulinzi na usalama haziainishi watu waliopendekezwa wanatoka chama gani cha siasa.
Akifungua semina hiyo Dk Shein pamoja na mambo mengine amewataka viongozi hao kutojihusisha na migogoro ya aina yoyote ikiwemo ile ya ardhi kwani inaathiri maendeleo ya kilimo, utalii na makaazi ya watu na wakati mwengine huathiri hata amani na usalama katika maeneo yao.
Alisema migogoro hii inavuruga ustawi wa uchumi pia, kutokana na ukosefu wa maadili pamoja na kutokuzingatia sheria ziliopo kwa baadhi ya watendaji matokeo yake ni kuwanyima haki zao wananchi wanaostahiki na kupelekea kunungunika.
“Katika yatakayozungumzwa hapa ni suala la ardhi, jambo lenye kuleta utata na migogoro katika jamii Unguja na Pemba na pia ijulikane kuwa tatizo hili si la Zanzibar pekee bali ni la nchi nyingi duniani”,alisisitiza Dk. Shein.
Dk Shein alieleza kuwa katika mfumo wa utawala wa nchi, viongozi wa Serikali za Mitaa wakiwemo Masheha na Madiwani wana jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba misihgi ya utawala bora inatekelezwa.
“Kama nilivyosema kule Unguja, nyie hapa ndio mlioko mashinani na mti wenye shina bovu hauwezi kusimama. Kwa kuzingatia haya, tumeamua kuendesha semina hii maalum kwenu ili kukupeni na nyinyi maelekezo na fursa kamili katika kujadili utawala bora”,alisema Dk.Shein.
Dk Shein alisema kuwa Utawala Bora ni kiini cha ustawi wan chi, amani na utulivu wake na kusisitiza kuwa malengo yote ya nchi yakiwemo uchumi na huduma za jamii yanalenga katika kuleta Utawala Bora kwa wananchi.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa katika awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa, suala la utawala bora lina umuhimu wa pekee.
Aliwaeleza Masheha na Madiwani wametakiwa kuwa uhusiano mkubwa katika kutunza amani na usalama ndani ya shehia zao. Aidha wameelezwa kuwa ulinzi unaotolewa na vyombo vya dola au Polisi Jamii ambao unawapa usalama wananchi utafanikiwa tu kwa mashirikiano yao na wahusika wengine.
Viongozi hao pia, wametakiwa lazima watambue kwamba utekelezaji wa mipango ya maendeleo unaofanywa na Serikali kwa kupitia kwenye Idara na Wizara zake huwa unatekelezwa katika shehia, zikiwemo upelekaji huduma za afya, elimu, maji na nyenginezo.
Pia viongozi hao aliwataka watambue jukumu jengine kubwa kwao ni kuchangia katika kuendeleza utalii nchini ambao unazidi kuwa tegemeo kubwa la uchumi sekta ambayo pia, imekuwa ikikua vyema kisiwani Pemba.
Wamesisitizwa kuzingatia suala zima la utunzaji wa mazingira na usafi katika shehia zao na kuwaleza kuwa ni lazima yawe ni miongoni mwa majukumu yao makubwa.
Aliwaeleza viongozi hao kuwa ukuaji wa majaa na utupaji ovyo wa taka unaendelea katika shehia hasa Wilaya zenye watu wengi kama vile Wete, Chake, Mkoani na Micheweni wakati Madiwani na Masheha wapo.
Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa kutokana na mafanikio ambayo kila mmoja atahusika nayo ikiwa ni pamoja na kuelewa misingi ya uongozi, utawala bora, maadili, uwajibikaji na umuhimu wake katika utkelezaji wa majukumu waliyokabidhiwa.
Semina hiyo ni mfululizo wa semina maalum za viongozi na watendaji wakuu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambazo tayari zimeshafanyika ikiwemo ile ya viongozi wa Serikali za Mitaa iliyofanyika Juni 26, mwaka huu kwa upande wa Unguja na leo ni zamu ya Pemba.
Semina hiyo iliyodhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) imelenga katika kutoa maelekezo ya mambo tofauti ya uongozi na kiutendaji, ardhi na migogoro yake utawala bora, mazingira, maadili, uchumi na utalii kwa wote, usimamizi wa fedha na ununuzi wa vifaa na nyenzo.
Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Matifa (UNDP) nchini Bi Njeri Kamau alisema kuwa Shirika hilo litaendelea kuiunga mkono Zazibar katika shughuli zake za maendeleo zikiwemo uendelezaji na uimarishaji wa Serikali za Mitaa kwa kutambua umuhimu wake katika maendeleo ya nchi.
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa semina hiyo pia, ina lengo la kuleta maelewao mazuri kati ya viongozi wa Serikali na wale wa Serikali za Mitaa na kuwataka kujenga maelewano mazuri.
Akitoa mada katika semina hiyo, Afisa Mwandamizi kutoa Serikali za Mitaa, Abrahamai Haji Mnoga alitilia mkazo na kueleza kuwa Sheha hana mamlaka juu ya ardhi na kitendo cha kujihusisha na mauzo ya ardhi za serikali ni matumizi mabaya ya madaraka aliyopewa.
Alisema kuwa taasisi inayohusika na ardhi za serikali ipo nayo ni Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati na kueleza kuwa wajibu wa sheha ni kulinda mali za Serikali na sio kujifanya wadhibiti wa mali hizo kinyume na sheria.
|
No comments:
Post a Comment