ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 22, 2012

Wizara yakamata makopo 8000 ya ARVs bandia




WALIOHUSIKA KUCHUKULIWA HATUA, WAATHIRIKA WASEMA SERIKALI INACHEZA NA MAISHA YA WATU
Mwandishi Wetu
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii, imekiri kuwapo kwa dawa feki za Kupunguza Makali ya Ukimwi (ARVs) kwenye mzunguko na tayari imekwishakamata zaidi ya makopo 8000 ya dawa hizo.Pia imesema kuwa inafanya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama ili kubaini wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Vilevile, Wizara imesema hatua nyingine itakayochukuliwa ni kufuatilia uondoaji wa dawa hizo bandia katika vituo vya huduma kwa kushirikiana na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Bohari ya Dawa (MSD).

Kauli hiyo ya Serikali inatokana na  kuchapishwa kwa habari na gazeti hili jana iliyofichua kuwapo kwa dawa za ARVs ambazo hazina ubora zikiendelea kupewa wagonjwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Regina Kikuli, ilieleza kuwa hadi kufikia Septemba 4, mwaka huu,  makopo 8,008 ya toleo namba  OC.01.85 ya dawa hizo yalikuwa yamezuiwa.

Taarifa hiyo ilitaja hatua nyingine inayoendelea kuchukuliwa na Serikali kuwa ni kuhakikisha jitihada zinafanyika kuendelea kuwapo kwa dawa za ARVs kwenye vituo vyote vya matibabu baada ya dawa hiyo bandia kuondolewa.

Hata hivyo, Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema katika taarifa hiyo kuwa dawa zilizobainika kuwa na matatizo ni kidogo na kwamba huduma za utoaji wa dawa hiyo utaendelea kama kawaida

.

“Toleo hilo la dawa ambalo limebainika kuwa na matatizo, halitaathiri utaratibu wa kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwa ni kiasi kidogo ukilinganisha na dawa zilizopo na pia zenye matatizo zimeondolewa katika mzunguko,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

“Kiasi hicho kingeweza kutumika kwa watumiaji 8,000 kwa mwezi tu kati ya takriban watumiaji 400,000 nchi nzima.”

Wataalamu waeleza madhara

Mtaalamu wa dawa kutoka Hospitali ya Amana, Dk Charles Lymo aliliambia Mwananchi jana kuwa kazi ya ARVs ni kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi, hivyo endapo mgonjwa atameza dawa feki, vijidudu vya ugonjwa huo vitaendelea kuushambulia mwili na kuudhoofisha.

“Virusi vya Ukimwi vinapoingia kwenye mwili wa binadamu, vina tabia ya kujibadilisha na kuwa kama chembe hai nyeupe ndipo zinapoanza kushambulia mwili,” alisema.

Alisema mgonjwa anapomeza vidonge vya ARVs huwa chakula cha virusi ambavyo vikishiba hulala.

"Virus ni sawa na mtoto kazi yake ni kula na  kulala na ndiyo maana mgonjwa anatakiwa ameze hivyo vidonge kila baada ya saa 12,”alisema mtalaamu huyo.

Dk Lymo alisema kuwa vidonge bandia huvifanya virusi kukosa chakula na hivyo kuamua kushambulia mwili.

“Kumeza dawa bandia ni sawa na kutoa unga wa ngano kwa virusi wakati siyo chakula chake. Kwa hiyo watakuwa wanashambulia tu na kuzaliana,” alisema Dk Lymo.

Kwa upande wake, Dk Mlangwa Mguta kutoka katika hospitali hiyo, alisema kwa kutumia dawa hizo bandia virusi hivyo vitaendelea kuwa sugu kwenye mwili wa binadamu.

“Lakini pia kwa kawaida hivi vidonge vina madhara na vikiwa feki ndiyo yanaongezeka kabisa,” anasema Dk Mguta.

Kwa upande wa Dk Alex Mwita, kutoka Taasisi ya Utafiti wa Tiba (Nimri), alisema kuwa kwa kuwa kazi ya ARVs ni kupunguza makali ya ugonjwa huo, dawa ikiwa bandia  mgonjwa anaweza kupunguza siku zake za kuishi kutokana na virusi kumdhoofisha.

“Dawa zikiwa bandia maana yake viambata muhimu havipo, ina maana hiyo dawa haiwezi kufanya kazi iliyokusudiwa,” alisema Dk Mwita.  
    
Wanaotumia ARVs

Rogers Stephen aliliambia Mwananchi kuwa habari ya kuwapo dawa bandia za ARVs nchini imemshtua na kwamba Serikali inapaswa kuchukua hatua haraka.

Alisema kuwa amekuwa akitumia dawa hizo kwa zaidi ya miaka 10 sasa tangu akiamini kuwa ni salama.

Stephen alisema kuwapo kwa vidonge bandia sokoni ni sawa na Serikali kuchezea maisha ya watu.

“Haya ni maisha ya watu, naona kama Serikali inataka kucheza na maisha yetu kwa sababu tulikuwa tunajua kuwa hizi dawa ni salama kabisa,” alisema Stephen.

Alisema kutokana na unyeti wa suala hili wakipata uthibitisho wa kisayansi kwamba kuna dawa hizo sokoni, watatafuta njia ya kufikisha malalamiko yao serikalini.

Mwanamke mwingine ambaye hakutaja jina lake ambaye anaishi ya virusi vya Ukimwi alisema amekaa na virusi vya Ukimwi kwa miaka 18 na Januari mwaka huu ndiyo alianza kutumia ARVs akiamini kuwa vitamsaidia.

“Sasa kama watu wanaotutengenezea hizo dawa wanatuletea vitu feki wanataka kutuua ama vipi? Hii ni sawa na mtu anakupa chakula anakwambia kitakupa afya kumbe kaweka sumu,” alisema mwanamke huyo.

Alisema kutokana na unyeti wa dawa hizo inatakiwa kuwapo na udhibiti wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa dawa zinazoingia sokoni ni salama.

Jana gazeti hili lilichapisha habari iliyokuwa ikieleza kuwa maelfu ya watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi ambao kwa sasa wanatumia ARVs nchini wapo hatarini kufupisha maisha yao baada ya kubainika kuwa toleo mojawapo la dawa hizo la Machi, 2011 ni bandia.

Uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha kuwa dawa hizo zilizosambaa katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mara zilianza kusambazwa tangu Mei mwaka huu na hadi sasa bado zipo sokoni, jambo lililoilazimu Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) kuagiza zirudishwe Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Tayari TFDA imetoa waraka ambao umesambazwa kwenda kwa waganga wakuu wa mikoa yote nchini kuwaagiza kuondoa dawa hizo kwenye mzunguko mara moja.

Mwananchi

No comments: