ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 22, 2012

Sitta aikoromea CCM



  *Inatia aibu kuachia ufisadi kujichimbia
  *Akerwa na �zomeazomea� ya wapinzani

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatia aibu kutokana na kujiimarisha kwa kikundi cha wasiokuwa waadilifu, wanaokifanya kizomewe na kukosolewa na wapinzani.
Sitta amesema hali hiyo imeathiri mashiko ya CCM kwa umma, na kukwamisha jitihada za serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ustawishaji huduma za jamii nchini.
Ameyasema hayo jana, wakati akizungumza katika mahafari ya 11 ya Shule ya Msingi ya Mchapuo wa Kiingereza ya Kwema na kuzinduliwa kwa Shule ya Sekondari ya Kwema Modern, zote zipo wilayani Kahama, mkoa wa Shinyanga.
Sitta alisema ukiukwaji wa maadili kwa baadhi ya wana-CCM wakiwa sehemu ya utawala wa nchi, kunaweza kukirithisha kizazi kipya hivyo kuondoa matumaini ya kuwa na taifa linalopiga hatua za maendeleo.

Kwa hali hiyo, Sitta aliihimiza jumuiya ya shule za Kwema, kuwekeza katika kuwaelimisha na kuwawezesha wanafunzi, kutambua na kuyaishi maadili mema, wakiwa tegemea la taifa kwa siku sijazo.
“Mnaweza kusoma kufikia hatua ya vyuo vikuu, elimu inaweza kutumika kulistawisha taifa, lakini ikipatikana kwa mtu mwenye hulka ya wizi, ubadhirifu na aina nyingine za ufisadi inakuwa balaa kwa jamii,” alisema.
Sitta alisema CCM ina wajibu mpana wa kuhakikisha vitendo viovu vinavyochochea kukiathiri, vinadhibitiwa kwa njia tofauti, ikiwemo kuwachagua viongozi bora.
“Hali ilivyo sasa inaifanya CCM kuwa chama cha aibu kwa sababu baadhi ya viongozi wenzetu hawana maadili,” alisema.
Sitta alisema viongozi wenye hulka ya ufisadi ndani ya CCM, wamejenga mtandao wa wale aliowaita kuwa ‘vipaza sauti vya mafisadi’, wakiwatetea na kutetea maslahi yao (mafisadi) bila kujali athari zake kwa jamii.
Alisema watu wa aina hiyo, wanafanana na wachekeshaji wa Mfalme katika historia ya mataifa ya Uingereza na Ufaransa, ambapo kazi yao ilikuwa kuwapiga ‘vijembe’ waliopingana na Wafalme katika nchi hizo.
“Watu hao wanapata riziki yao kutokana na ukibaraka wao, wa kuimba na kumpamba anayewalipa hata kama wanachokitetea kinaiathiri jamii,” alisema.
AHOFIA MAFISADI KUITEKA SHINYANGA
Sitta alisema kuna fununu kwamba kikundi cha mafisadi, kimejidhatiti kupandikiza viongozi watakaosimamia matakwa yao na kuwajengea mazingira ya kuendeleza mitandao ya kuhujumu uchumi na rasilimali za nchi.
Aliukejeli mkakati huo na kusema, watekelezaji wake wanafikiri kwa kutumia matumbo badala ya akili kama ilivyo kwa binadamu wa kawaida.
“Watu hawa hawafikiri kwa kutumia akili, wanatumia matumbo yao na mengine ni makubwa yanakaribia kupasuka…hawawezi kuwa kielelezo cha CCM inayotakiwa kwa Watanzania,” alisema.
Mkoa wa Shinyanga hivi sasa unaongozwa na Mwenyekiti wake, Khamis Mgeja, ambaye hivi karibuni, alimpongeza Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbroad Slaa, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ‘kumuumbua’ Sitta.
Dk Slaa alimjibu Sitta baada ya Waziri huyo kusema, akiwa mkoani Kagera, kuwa CCM ina hazina ya viongozi tofauti na Chadema, inayomtegemea zaidi Dk Slaa.
“Inasikitisha na kutisha sana mtu anapokuwa kibaraka wa mafisadi, lakini zaidi ya hapo akajitokeza hadharani na kujisifia kwa hilo,” alisema.
Aliongeza, “ukiwa na viongozi wa aina hiyo, hauwezi ukawakuta watu wanaounga mkono mambo mazuri kama tunayoyaona katika shule hizi.”
AUSHUKIA MGODI WA BUZWAGI
Sitta alisema Kahama ni eneo lenye umuhimu wa pekee katika Nyanja tofauti za kijamii, kutokana na kufikiwa kwa urahisi na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Alisema lakini inashangaza kuona umeme wa uhakika unaotoka kwenye gridi ya Taifa, umeishia kwenye mgodi wa Buzwagi, huku ukiliacha eneo kubwa la Kahama kutokuwa na umeme wa uhakika.
“Hali hii ni kashfa kubwa sana, lakini tunapozungumza hivyo, wanajitokeza wengine wananuna kwa sababu hawataki kutenda haki kwa wananchi,” alisema.
Aliongeza, “hii ni aibu na aibu ni aibu tu hata ukiwa unaifanya wewe mwenyewe, kwa maana wengine watasema ninailaumu serikali…tufike mahali ukweli ubaki kuwa ukweli.”
LEMBELI: TUVUTIE WANAFUNZI KUTOKA NJE
Naye Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli, alisema wakati umefika kwa Tanzania kuhamasisha wanafunzi kutoka nje, waje kusomea hapa nchini.
Alisema hivi sasa kuna shule zinazotoa elimu bora, ikiwemo Kwame aliyomtaka Sitta kuitangaza katika nchi za EAC.
KWEMA: TUNATAKA KUWA CHUO KIKUU
Naibu Mkurugenzi wa shule za Kwame, Pauline Mathayo, alisema pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo, uongozi wa shule hizo umeazimia kujikita katika uboreshaji wa elimu hadi kufikia Chuo Kikuu.
“Lengo letu ni kuendelea kuboresha kiwango cha elimu mwaka hadi mwaka, hatimaye tufikie kuwa na Chuo Kikuu,” alisema.


 
CHANZO: NIPASHE

No comments: