ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 25, 2012

Zanzibar yachaguliwa kuwa makao makuu ya kamisheni ya Afrika Mashariki

 Picha juu na chini ni Wajumbe wa kamisheni ya kiswahili kutoka nchi tano za Afrika Mashariki waliopo Zanzibar katika kikao chao cha siku tatu kinachofanyika katika ukumbi wa Eacrotanal Visiwani Zanzibar.  
Salma Said, Zanzibar

KAMISHENI ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imekubaliana kuwa makao makuu ya kamisheni hiyo yawepo Zanzibar.

Uamuzi huyo umeafikiwa jana na wajumbe wa mkutano huo kutoka hizo za Afrika Mashariki ikiwmeo Burundi, Uganda, Kenya, Tanzania na Rwanda kwa sauti moja wamekubaliana kwamba makao makuu hayo yawepo Eacrotanal Mjini Unguja.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mkutano huo, Mkurugenzi  wa Utamaduni, Wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Hermas  Mwansoko, alisema kamisheni hiyo itaanzishwa rasmi wakati wowote kuanzia sasa baada ya wajumbe hao kukubaliana.


Awali wajumbe wa mkutano huo kutoka nchi tano za Afrika walitembelea majengo ya kituo  cha zamani cha utamaduni cha Eacrotanal ambapo kwa kiasi kikubwa waliridhishwa na majengo hayo na kutangaza kuwa makamo makuu hayo yatahitaji watendaji wakuu  na wafanyakazi wengine wa kamisheni itakayoanzishwa, akiwemo katibu mtendaji na manaibu wake wawili.


Pamoja na mambo mengine wajumbe wa mkutano huo watajadili uendeshaji wa kamisheni na njia zitakazotumika ili kuleta faida katika ukuzaji wa lugha ya kiswahili katika nchi husika.

Akizungumzia lengo la mkutano huo wa siku tatu Profesa Mwansoko alisema na kurejesha mashirikiano ya awali katika sekta ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ambapo zamani nchi hizo zilikuwa zikishirikiana sana.

Alisema wanachama wa EAC kuanzisha kamisheni hiyo ni kukuza matumizi ya Kiswahili katika uendeshaji  wa shughuli za jumuiya pamoja na za Bunge la jumuiya ya EAC ambapo hivi sasa bunge hilo linaendesha shughuli zake kwa kutumia lugha za Kiingereza kama lugha rasmi.

Mwansoko alisema kufunguliwa rasmi kwa ofisi za makao makuu ya kamisheni hiyo hapa Zanzibar kutatanguliwa na marekebisho ya majengo yaliyokuwa yanatumiwa na Eacrotanal.

Aidha alisema kabla ya taasisi hiyo kusitisha shughuli zake mwaka 1995 na majengo kuwekwa chini ya uangalizi wa shirika la Unesco na Tanzania.

Professa Mwansoko aliwaambia waandishi wa habari kwamba miongoni mwa watakaokuwa watendaji wa kamisheni itakayoanzishwa ni pamoja na watafiti wa Kiswahili na wataalamu wengine kutoka mabaraza ya Kiswahili ya nchi zote wanachama wa EAC.


Professa Mwansoko alisema kuwa kuanzishwa kwa kamisheni ya lugha ya kiswahili inatoa fursa nyingi kwa wananchi wa nchi zinazounda jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba kama fursa hiyo utatumika vizuri itaweza kuwaunganisha wananchi wa nchi hizo. Akizungumzia changamoto zinazowakabili katika ukuzaji wa lugha ya kiswahili katika jumuiya ya Afrika Mashariki,.

Akizitaja changamoto hizo ni pamoja na kuwa kuwa na uchache wa wataalamu ambapo alisema wataalamu waliopo wa lugha ya Kiswahili zaidi ni kutoka Tanzania na Kenya.

“Tuna uhaba wa wataalamu kwa sababu wataalamu wa lugha ya Kiswahili wengi wanatoka Tanzania na Kenya ingawa wapo waliosomea fani hiyo hadi kufikia kiwango cha kuwa wanafalsafa kutoka Rwanda lakini nasema walio wengi ni kutoka nchi mbili” alisema Professa.

Changamoto nyengine Professa alisema ni kupatikana kwa vifaa vya kisasa vya kufundishia lugha ya Kiswahili kama video na kutumia vitabu mbali mbali ambavyo vitaweza kuwaelewesha wenye kujifunza.

“Tunahitaji tuwe na vifaa vya kisasa vya kufundisia lugha ya Kiswahili lakini pia tuwe na utumiaji wa kisasa kama kutumia video kwa kufundishia vitabu na mitandao mbali mbali mfano kumuonesha mwanafunzi namna anavyozungumza lugha ya Kiswahili anapokwenda sokono, anapokuwa nyumbani, anapokwena kuchota maji na kadhalika” alisema.


Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo imefufuliwa miaka 10 iliyopita imo katika juhudi za kujiunganisha katika masuala ya uchumi, siasa, na kijamii ikiwa na lengo la kupanua lugha ya kiswahili katika nchi hizo.

Ukanda wa Afrika Mashariki unakadiriwa kuwa na watu milioni 150 na asilimia 80 kati ya hao inaaminika mawasiliano yao yanafanyika kwa Kiswahili, Zanzibar na Tanzania bara ikiwa inaongoza, ikifuatiwa na Kenya na Burundi.  

Kuhusu ya manufaa ya kamisheni hiyo kuwa Zanzibar, Profesa Mwansoko alisema ajira za taasisi hiyo ambazo haziitaji utaalamu wa hali ya juu, kama vile udereva, ukatibu muhtasi na usafi wa ofisi na uhudumu zitatolewa kwa Wazanzibari. 


No comments: