Bwana Vuaa Mwadini Mcha wa Kijiji cha Chwaka akifafanua kero zinazowakabili za mgogoro wa uvuvi kati ya Kijiji hicho na Marumbi ambazo wamedai kuchangiwa na baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Kati.
Bwana Nuru Muhammad wa Kijiji cha Chwaka akionyesha kusikitishwa kwake na Mradi wa Macemp kumalizika muda wake bila ya kuwanufaisha Wavuvi wa Ghuba ya Chwaka.
Picha no:- 504 ni:- Wananchi wa Kijiji cha Chwaka wakiongozwa na Bwana Vuaa Mwadini Mcha wakimtakia safari njema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya kupokea Kero na Changamoto zinazowakabili Wananchi wa Kijiji hicho.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kufikiria muundo wa Miradi mbadala ya Kiuchumi itakayosaidia kutoa ajira, kulinda Mazingira ya Bahari pamoja na kupunguza msongamano wa wavuvi katika Ghuba ya Chwaka na Marumbi.
Muundo huo wa miradi Mbadala kwa njia nyengine pia utakuwa suluhisho la kudumu la mgogoro wa muda mrefu wa uvuvi unaokaribia miaka 35 sasa kati ya Vijiji jirani vya Chwaka na Marumbi viliopo Wilaya ya Kati.
Ombi hilo limetolewa na Wananchi wa Kijiji cha Chwaka wakati wakitoa kero pamoja na changamoto zinazowakabili mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika uwanja wa soka wa Chwaka Wilaya ya Kati.
Mkutano huo wa Balozi Seif ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati alipokutana na Wananchi wa Marumbi kupokea kero na Matatizo yao miezi michache iliyopita ambayo yanavihusu Vijiji hivyo kwa pamoja kubwa hasa ni suala la Uvuvi.
Bwana Vuaa Mwadini Mcha alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba idadi kubwa ya Wavuvi wanaofanya shughuli zao za Uvuvi katika ghuba ya Chwaka imekuwa kubwa kulinganisha na uwezo wa ghuba yenyewe.
Hata hivyo Bwana Vuaa alisema Wananchi wa Chwaka wako tayari wakati wowote kumeguka kwa asilimia kubwa kutoka katika shughuli za Uvuvi kama Serikali itaanzisha miradi ya Kiuchumi itakayowawezesha Wananchi hao kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku.
“ Tunakumbukumbu nzuri tusiyoisahau ya Rais wa Awamu ya Pili Mzee Aboud Jumbe Mwinyi wakati ule alipotutaka tuachane na uvuvi wa juwa. Kwanza alituwezesha kwa kutuletea nyavu na baadaye taaluma ya matumizi bora ya Bahari mpango ambao ulifanikiwa kwa kiwango kikubwa sana”. Alifafanua Bwana Vuaa Mwadini.
Alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Wananchi na Wavuvi wa Chwaka hawana ugomvi na Wananchi wa Marumbi lakini kinachojitokeza ni Baadhi ya Viongozi wa Serikali na Polisi Wilaya ya Kati kuwa na kigugumizi cha kuchukuwa hatua za kisheria wakati yanapotokea matatizo hasa ya Uvuvi baina ya pande hizo mbili.
“ Chwaka haiko tayari Mwananchi ye yote afariki kutokana na ugomvi wa Uvuvi. Lakini tumefikia wakati kukosa imani dhidi ya uongozi wa Polisi na Serikali wa Wilaya ya Kati kwa kushindwa kuchukuwa hatua za kisherika kwa watu wanaokiuka sheria hizo.
Naye Bwana Nuru Muhammad alielezea masikitiko yao kutokana na Mradi mkubwa ulioanzishwa chini ya uhadhili wa Benki ya Dunia wa kuwawezesha wavuvi wa Ghuba hiyo { Macemp } kutowanufaisha Wavuvi hao ambao ndio walengwa wa mradi huo.
Bwana Nuru alifahamisha kwamba licha ya juhudi zilizochukuliwa na Wawakilishi wa Mradi huo kupitia wasimamizi wa Benki ya dunia wa kukutana na Wananchi hao kwa kupanga malengo ya mradi huo kiutekelezaji kwa vile mfuko wa mradi huo haukuwa na mashaka lakini kilichojichomoza zaidi kwa mfuko huo ni kuendelezwa kwa semina na vikao.
“ Inasikitisha kuona Vikao mbali mbali vilifanywa kwa kushirikishwa wavuvi husika lakini nguvu za mradi huo zikaelekezwa sehemu nyengine bila ya kuwanufaisha walengwa ambao ni sisi Wavuvi”. Alisisitiza Bwana Nuru.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wajibu wa Serikali wakati wote ni kufuatilia na kujua kero zinazowakabili Wananchi na kuzitafutia ufumbuzi unaostahiki.
Balozi Seif alielezea kusikitishwa kwake na mgogoro wa uvuvi unaotia doa mfumo wa amani na utulivu Nchini unaovikumba Vijiji vya Chwaka na Marumbi kwa karibu miaka 35 sasa.
“ Sisi tunataka amani na utulivu, watu waishi pamoja, wafanye kazi pamoja, haya mambo ya Ukafu na uccm hayana nafasi tena katika Jamii. Tunachokizingatia zaidi kwetu sisi kama Serikali ni kuona wananachi wanaishi kwaamani na kushirikiana pamoja”. Alisisitiza Balozi Seif.
Katika Mkutano huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliahidi kutoa Mabomba 800 pungufu yaliyooelezwa ndani ya risala ya Wananchi hao wa Chwaka kukamilisha Mabomba 1200 yaliyokisiwa kutumika katika mradi wa Maji safi na Salama katika Shehia hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban aliahidi kugharamia ujenzi wa Tangi la Maji ili kukamilisha mradi huo muhimu.
Hata hivyo Waziri Shaaban aliwanasihi Wananchi hao wa Chwaka kuwa na stahamala kidogo kwa vile kazi hiyo inahitaji gharama ambayo kwa hivi sasa itahitajika kutafutiwa bajeti yake.
Aliwataka Wananchi hao wa Chwaka kuwa tayari wakati utapowadia kuitekeleza kazi hiyo kwa ushirikiano na Watendaji wa Taasisi za Wizara hiyo kwa njia ya mpango wa ujenzi wa Taifa.
No comments:
Post a Comment