ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 23, 2012

Serikali yapata kigugumizi usajili namba magari


ACP Johansen Kahatano
Wakati siku zaidi ya saba zikiwa zimepita baada ya muda uliotangazwa na serikali kwa watumishi wa umma kuacha kutumia namba za kiraia kwenye magari yake, serikali inasuasua kutoa taarifa kuhusiana na maendeleo ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Mwezi uliopita, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, aliagiza kuwa Novemba 15 mwaka huu itakuwa siku ya mwisho kwa watumishi wa umma kuendelea kutumia namba za kiraia.

Baada ya muda huo kumalizika, Jumatatu wiki hii, Kamshna Msaidizi wa Polisi na Afisa Mnadhimu Kikosi cha Usalama Barabarani, ACP Johansen Kahatano, aliliambia NIPASHE kuwa zoezi linaratibiwa na wizara yenyewe na ndiyo inayojua maendeleo ya utekelezaji.
Mkuu wa Kitengo cha Mwasiliano wizarani hapo, Martin Ntemo, alisema kuwa zoezi la usajili linaendelea, lakini taarifa kuhusu idadi ya magari yaliyosajiliwa na kupewa namba mpya na mambo mengine, itatolewa wakati wowote.
Juzi gazeti hili liliwasili tena wizarani hapo na kuwasiliana na Ntemo kwa njia ya simu, naye alisema:
Hata hivyo, habari zaidi zinaeleza kuwa zoezi hilo linakwenda vizuri huku mamia ya magari yakiwa yameshaanza kubadili namba.
Hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, John Ndunguru, alisema serikali iliweka utaratibu unaozuia matumizi ya namba za kiraia kwenye magari yake isipokuwa kwa kibali maalumu kutokana na kubaini kuwa, kupitia namba hizo, magari ya umma yalikuwa yakitumiwa vibaya na baadhi kupotea.
Magari ya serikali na taasisi zake, baada ya zoezi hilo kukamilika, yatapaswa kusajiliwa kwa utaratibu uliowekwa na serikali unaotaka magari ya Serikali Kuu kuwa na mamba za ST, Serikali za Mitaa SM, mashirika ya umma SU na yaliyotolewa na washirika wa maendeleo kwa ajili ya miradi wanayoitoa, DFP. Ya Jeshi (JW), Polisi (PT), na Magereza wataanza kutumia namba mpya za MT.
Ndunguru alisema baada ya agizo hilo, serikali itaendesha msakao wa kukamata magari ambayo yatakuwa bado hayajasajiliwa kwa namba za serikali.
Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 kifungu Na. 30 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004 inaipa mamlaka Wizara ya Ujenzi kusajili na kutunza kumbukumbu za magari yote ya serikali ambayo yatapewa namba zitakazotanguliwa na JW, PT, ST (sheria na 62), na DFP (GN. No.517 ya Novemba 29, 2002.
CHANZO: NIPASHE

No comments: