ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 5, 2012

Wakili: Korti ilikosea kumvua Lema ubunge

Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (wapili kulia) akiambatana na wafuasi wa Chadema wakitoka nje ya Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam jana, baada ya kusikilizwa rufaa yake ya kupinga kuvuliwa ubunge wake. Picha na Michael Jamson 

WAKILI wa Serikali Mkuu Timon amedai kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilikosea kutengua ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, kwa madai ya kutumia lugha za matusi kwa kuwa Bunge limeruhusu wanasiasa kutukanana kwenye kampeni.

Wakili Vitalis alitoa madai hayo jana, wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya Lema, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),katika Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.
Wakati wakili huyo wa serikali akitoa madai hayo, Wakili wa wajibu rufaa, ambao walishinda katika kesi ya msingi, Alute Mughway, naye alidai kuwa Mahakama Kuu, Arusha ilikosea katika uamuzi wake, pamoja na mambo mengine, kwa kukataa baadhi ya madai yao.

Lema alivuliwa ubunge April 5, 2012, katika hukumu iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalia, kufuatia kesi iliuyofunguliwa makada watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Lema kupitia kwa Wakili wake Method Kimomogoro alikata rufaa Mahakama ya Rufani, lakini Novemba 8, 2012 mahakama ilitupilia mbali rufaa hiyo baada ya kuini kuwepo kwa dosari za kisheria, kutokana na pingamizi lililowekwa na upande wa wajibu rufaa.

Hata hivyo mahakama hiyo ilimpa nafasi nyingine ya kukata rufaa tena baada ya kumpa siku 14 kufanya marekebisho ya dosari hizo za kisheria na kuiwasilisha mahakamani ndani ya muda huo, amri ambayo aliitekeleaza.

Wakati Lema akikata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kumvua ubunge, wajibu rufaa nao walikata rufaa (Cross Appeal) kupinga uamuzi wa mahakama hiyo, huku wakibainisha hoja nne.

Katika hoja ya kwanza hadi ya tatu walidai kuwa Jaji alikosea katika hukumu yake kwa kuchanganya vituo vilivyotolewa ushahidi na mashahidi wanne na hatimaye akakataa ushahidi wapo, pamoja na tarehe za ratiba ya kampeni ya CCM nay a Chadema.

Hoja ya nne walidai kuwa Jaji alikosea kwa kuamua kuwa hata kama Lema kwenye kampeni zake alidai kuwa Dk. Buriani ni mkazi wa Zanzibar hatafaa, wakidai kuwa ukazi si sifa ya kuchaguliwa kuwa mbunge.

Hatimaye rufaa hizo zilisikilizwa jana na jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, lililoundwa na Jaji Salum Massati, Jaji Bernard Luanda, chini ya uongozi wa Jaji Nathalia Kimaro.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, mawakili wawili ambao ni ndugu, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu na kaka yake Mghway, walipambana vikali kwa hoja za kisheria.

Lisu, Kada wa Chadema ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alikuwa akimtetea Lema mrufani (Lema), akisaidiana na Wakili Method Kimomogolo, huku Mughway akiwatetea wajibu rufani ambao ni makada wa CCM.

Hata hivyo Wakili Vitalis, aliyemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye pia alikuwa upande wa Lema, alidai kuwa wajibu rufaa hawakuwa na haki ya kufungua kesi kupinga ushindi wa mrufani (Lema) kwa kasoro zilizotokea wakati wa kampeni.

Wakili Vitalisi alidai kuwa wajibu rufani hao hawakuwa wahusika katika katika mchakato huo kampeni na kwamba hata kama kulikuwa na lugha ya matusi kama walivyodia katika ushahidi wao mahakama haikuwastahili kumvua ubunge kwa kuwa Bunge liliruhusu matusi kwenye kampeni.

Akifafanua zaidi Wakili Vitalis alidai kuwa anayepaswa kufungua kesi mahakamani kwa madai ya lugha ya matusi ni yule aliyetukana kwa kuwa hayo ni maumivu ya mtu binafsi na kwamba hata anapokufa, madai yake nayo hufa wala hayawezi kuendelezwa na mtu mwingine.

“Sasa iweje kwa mtu ambaye yuko hai lakini watu wengine ndio waje mahakamani kufungua kesi?”, alihoji Wakili wa Serikali Vitalisi.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 108 cha Sheria ya Uchaguzi Sura ya 313 ya mwaka 2010, matusi si miongoni mwa mambo ambayo yanaweza kutengua matokeo ya uchaguzi.

Hata hivyo Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa Bunge liliruhusu kutukana na baada ya kufanya marekebisho katika sheria ya uchaguzi, mwaka 1995 kufuatia hukumu ya kesi kati ya AG na Aman Waridi Kaburu.

Alidai awali sharia ilikuwa inaruhusu matokeo ya uchaguzi kutenguliwa kutokana na lugha za matusi, lakini baada ya hukumu ya kesi ya Kaburu Januari , 1995, mwezi Julai mwaka huo Bunge lilifanya marekebisho na kuondoa suala la matusi katika mambo yanayoweza kutengua uchaguzi.

“Hapa Bunge liliifunga mikono mahakama, hakuna kutengua matokeo ya uchaguzi kwa mambo amabayo hayajatajwa. Kwa uamuzi huu waliamua kutukanana, kwa hiyo nasi hatuwezi kuwakatalia.”, alidai Wakili Vitalisi.

Pia alidai kuwa kifungu cha 108 (2) cha Sheria ya Uchaguzi kinaeleza aina ya za ubaguzi zinazokatazwa ni pamoja na wa kidini na kikabila na kwamba aina nyingine kama makazi (Uzanzibar, Ubara) hazijatajwa.

Awali Wakili wa Lema Kimomogoro aliainisha sababu 18 za rufaa hiyo kuwa ni pamoja na Jaji kuamua kuwa Sheria zinazotumika katika Nchi za Jumuiya ya Madola (hususan Uingereza), hazitumiki katika kesi za uchaguzi nchini.

Sababu nyingine alidai kuwa ni Jaji kutokujieleza vyema kama wajibu rufaa waliwajibika katika hati yao ya madai kwa kutaja maneno dhahiri ya ubaguzi dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batlida Burian.

Sababu nyingine alidai kuwa Jaji alikosea kuamua kuwa mtu yeyote aliyejiandikisha kupiga kura ana haki isiyo na mpaka ya kufungua kesi kupinga matokeo.

Alidai kuwa hoja yao ni kwamba mtu anakuwa na haki hiyo pale ambapo haki yake imevunjwa au inaelekea kuvunjwa na si pale aliyeathirika na ukikwaji wa haki hiyo ni mtu mwingine.

Sababu nyingine alidai kuwa Jaji hakutolea uamuzi baadhi ya hoja ambazo zilitakiwa kujibiwa na kwamba hakujielekeza vyema kwenye wajibu wa kuthibitisha madai kwa kueleza kama walalamikaji walithibitisha madai yao bila kuacha mashaka yoyote.

Sababu nyingine ni kwamba Jaji alitumia ushahidi wa mdomo bila kungwa mkono na ushahidi mwingine, na kwamba Jaji alijielekeza vibaya katika kupima ushahidi wa pande zote na badala yake akaegemea ushahidi wa walalamikaji na mashahidi wao tu.

Pia alidai Jaji alikose kusema kuhusu hoja ya vitendo vya kijinai na kwamba hakuvitaja hivyo vitendo vilivyofanywa na mrufani, huku akisisitiza kuwa hukumu hiyo haikukidhi vigezo vya kisheria.

Hata hivyo akijibu hoja hizo, Wakili Mughwa alidai kuwa hukumu hiyo imekidhi vigezo vya kuwa hukumu kwa kuwa inaeleza mambo yote yanayopaswa kuwepo.

Wakili Mughwa alidai kuwa walalamikaji katika kesi ya msingi kwenye ushahidi wao walieleza maneno yaliyokuwa yakilalamikiwa huku akidai kuwa mawakili wa utetezi wanaipotosha mahakama kwa kuwa mambo mengine aliyopinga yako kwenye kumbukumbu za mahakama.

Kuhusu matumizi ya Sheria za Nchi za Madola, huku akitoa orodha ya kesai mbalimbali, alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 2 (3) cha Sheria ya Uchaguzi kesi za uchaguzi zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi na kwamba Jaji alikuwa sahihi kuamua hivyo.

Akizungumzia haki ya mpiga kura kufungua kesi, Wakili Mughway alidai kuwa haki hiyo inaelezwa katika kifungu cha 111 (1) (A) cha Sheria ya Uchaguzi (2010) pamoja na katiba.

Mwananchi

No comments: