Wednesday, December 5, 2012

WAZIRI WA HABARI UTAMADUNI UTALII NA MICHEZO AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI JUU YA MATENGENEZO YA BEIT EL AJAB

Waziri wa habari utamaduni utalii na michezo Said Ali Mbarou akizungumza na waandishi wa habari juu ya kulifanyia matengenezo jengo la Beit El Ajab lililoanguka moja ya sehemu zake. Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar

NA RAMADHANI ALI.
Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba maharibiko ya kuanguka sehemu ya jengo la Makumbusho ya Taifa Beit El Ajab yanarekebishwa na matengenezo ya jumla ya jengo hilo na majengo yote ya kihistoria yanasimamiwa ipasavyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makumbusho ya Mnazimmoja, Waziri Mbarouk amesema kutokana na heshima na hadhi ya jengo la Beit El Ajab kwa historia ya Zanzibar, kuanguka kwa jengo hilo kumeathiri shughuli za utalii kwani ni miongoni mwa vivutio vikuu vya Utalii ZANZIBAR.

“Asilimia 70 ya wageni wanaotembelea sehemu za kihistoria huwa wanafika makumbusho ya Beit El Ajab’’, alisema Waziri Said Ali Mbarouk.

Amesema uamuzi wa kuyahifadhi maeneo ya Historia ikiwemo jengo la Beit El Ajab utaendelea kupewa umuhimu mkubwa kwani ni sehemu ya urithi wa Utamaduni wa Zanzibar na yanahitaji kudumu kwa miaka mingi zaidi.

“Jengo hili lililojengwa mwaka 1883 na Mfalme Barghash bin Said ni moja kati ya majengo yenye hadhi kubwa kihistoria, kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa Zanzibar” alisisitiza Waziri Mbarouk.

Amesema umaarufu wa jengo la Beit El Ajab unatokana na kuwa ni la kwanza Zanzibar kuwekewa huduma za kijamii kama vile umeme, simu, lifti na maji ya mfereji kabla ya huduma hizo hazijaanzishwa kwenye nchi nyingi za Afrika Mashariki.

Ameongeza kuwa kutokana na maharibiko yaliyotokea Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe inachukua hatua ya kuiarifu UNESCO kuhusu tukio hilo na kuomba msaada wa kitaalamu na fedha kulinusuru.

Aidha amesema Idara ya Makumbusho na Mambo ya kale inafanya mawasiliano na watalaalamu wa majengo ya kale ili kupata tathmini ya hali ya jengo hilo na Kasri ya Kifalme na aina ya matengenezo ya kudumu na gharama zinazohitajika.

Jengo la Makumbusho kuu ya Jumba la Ajab lilianguka usiku wa Jumamosi iliyopita wakati likiendelea kufanyiwa matengenezo na MACEMP na limewahi kutumika kwa sherehe na shughuli za utawala wakati wa ufalme, Makumbusho ya Chama cha ASP, Chuo cha Itikadi ya Chama na kuanzia mwaka 2002 likapewa hadhi ya kuwa makumbusho inayohusu Utamaduni wa Mswahili na Historia ya Zanzibar.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments: