Mabingwa hao wa soka Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), ambao waliweka kambi yao kwenye hoteli inayotajwa kuwa ya kifahari ya Fame Residence iliyopo katika mji wa ‘matanuzi’ wa Antalya, walitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam saa 9:28 usiku wa kuamkia juzi.
Wakiwa Uturuki, Yanga walifaidi ‘maraha’ ya Ulaya kwenye viwanja safi vya michezo, vyumba vya kisasa vya mazoezi ya viungo (gym), vifaa vya kutosha vya mazoezi, mabwawa mazuri kwa ajili ya kuogelea, mazingira ya kupumzikia, ulinzi, huduma safi za afya, hali nzuri ya hewa na miundombinu ya kisasa ya hoteli hiyo na mji wa Antalya kwa ujumla.
Tofauti na kusafiri katika barabara za 'juu na chini' za Uturuki, vinara hao wa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (Yanga), pia walipata fursa ya kujipima uwezo kwa kucheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya timu Arminia Bielefeld iliyowahi kukipiga katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga),
Denizlispor ya Ligi Daraja la Kwanza Uturuki na
Emmen FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Uholanzi.
Hata hivyo, taarifa zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako, zimeeleza kuwa timu hiyo itaanza rasmi mazoezi yao nyumbani leo kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama jijini Dar es Salaam; mahala ambako pana kiwango cha chini mno kwa ubora kulinganisha na eneo walilokuwa ‘wakijifua’ nchini Uturuki.
Yanga watafafanya mazoezi hayo kwenye uwanja ambao umejaa ‘vipara’ katika baadhi ya maeneo, huduma za afya ziko mbali huku uwanja huo ukiwa na kumbukumbu ya kumtoa vidonda aliyekuwa kocha wao, Mbelgiji Tom Saintfiet, hali iliyomlazimu daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani kumzuia kocha asifanya mazoezi na wachezaji.
Kwenye uwanja huo wa Bora uliojaa kokoto, Yanga walikuwa wamekuwa wakikumbana na vituko vingi vya maisha halisi ya ‘uswazi’ vikiwamo vya kuibwa kwa baadhi ya vifaa vyao na vibaka wanaowavamia kirahisi kwavile uwanja huo hauna ulinzi wa kutosha.
Kiungo wa Yanga, Athumani Iddi ‘Chuji’ ni shahidi wa vituko vya uwanja wao wa ‘uswazi’ Bora kwani Julai 4, 2012 alilazimika kufanya kazi ya ziada kumuokoa kibaka aliyekuwa akila kipigo baada ya kuiba mpira wao na kufanya mazoezi yasite kwa zaidi ya dakika 10, huku kocha wao Saintfiet akishangaa na kutoamini kutokana na yale aliyokuwa akiyashuhudia.
Kwa kawaida, wasipofanya mazoezi kwenye Uwanja wa Bora, Yanga hukimbilia kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Mabibo jijini Dar es Salaam ambao pia umejaa vipara na tofauti yake kwa ubora na Uturuki ni kama mbingu na ardhi.
Cha kusikitisha, uwanja wa Yanga wa Kaunda uliopo katika mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam nd’o una hali mbaya zaidi kiasi cha wao wenyewe kuukimbia.
KUWAVAA WASAUZI J'MOSI
Katika hatua nyingine, ‘Wanajangwani’ watapima makali yao waliyoyapata Uturuki wakati watakapocheza dhidi ya timu ya Black Leopards kutoka Afrika Kusini ‘Sauzi’ kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Yanga jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako alisema kuwa mechi hiyo ambayo awali ilipangwa ichezwe Jumapili imesogezwa mbele kwa siku moja ili isiingiliane na Mkutano Mkuu wa klabu hiyo utakaofanyika Jumapili Januari 20.
“Timu yetu itaanza mazoezi kesho (leo) baada ya kupata mapumziko ya siku mbili kutokana na uchovu wa safari. Tutacheza dhidi ya Black Leopards FC ya Afrika Kusini Jumamosi, mechi hiyo ni muhimu kujua hali ya timu yetu baada ya kuweka kambi ya Uturuki,” alisema Mwalusako ambaye alikuwa amefuatana na kocha wao Mholanzi Ernie Brandts.
Katika hatua nyingine, Mwalusako pia alisema kuwa sakata la Sufiani kutoenda na timu yao Uturuki litajadiliwa na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo leo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment