Tuesday, March 26, 2013

Al Kharoosi kuwajengea yatima makazi ya kudumu




Kutolewa kwa msaada huo inaonyesha kama ukombozi kwa kituo hicho, ambacho kina watoto 70  
Dar es Salaam. Watoto yatima wanaolelewa Kituo cha Umra kilichopo Magomeni Makuti Dar es Salaam, wamepata faraja zaidi baada ya Mjumbe wa Kamati ya Ushindi ya Klabu ya Simba, Rahma al Kharoosi kuwajengea kituo cha kisasa maeneo ya Mbezi Msakuzi.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kharoosi alisema amechukua uamuzi huo kwa sababu amekuwa karibu na yatima wengi na kutoa kile alichonacho kuwasaidia ambao  wanahitaji huruma ya jamii.
“Huwa ninaguswa na watoto yatima, ndiyo maana siku zote ninajiona nina deni nao, sasa nimeamua kuwajengea watoto wa kituo hiki cha Umra kituo chao cha kisasa kabisa, ambacho watakuwa hawalipi tena kodi,” alisema al Kharoosi na kuongeza:
“Hapa Magomeni wanalipa kodi, hawana sehemu ya michezo, kule kutakuwa na nafasi ya michezo na hawatalipa tena kodi, kitakachokuwapo ni kuwasaidia tu mahitaji ya chakula kwa kuwa hawa ni binadamu.”
Al Kharoosi ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafuta na Madini ya RBP Oil.
Akizungumza baada ya ahadi hiyo, mlezi wa watoto hao wapatao 70, Rahma Juma alimpongeza Alh Kharoosi kwa uamuzi wake huo.
“Mungu atamlipa. Hawa watoto wanahitaji huruma ya jamii kama Al Kharoosi... kikubwa ninamshukuru kwa kuwakumbuka yatima hawa na kuwapa hifadhi nzuri,” alisema Juma.
Juma alisema watoto yatima wamekuwa wakiishi maisha magumu hasa wasichana ambao wakati mwingine hupata vishawishi vya kujiingiza kwenye vitendo viovu.
“Bila kuwa na makazi imara ni vigumu kwa watoto hawa kukua kwa maadili ambayo tunataka, lakini kutokea msaada huu utawajengea msingi wa maisha bora,” alisema Juma.
Pia, aliwataka watu wengine kujitokeza kusaidia watoto hao.
Al Kharoosi alikutana na watoto hao na kuwataka kusoma kwa bidii. Pia, aliwapa zawadi mbalimbali ikiwamo jezi, mipira, mifuko ya unga, sukari, mchele na katoni za juisi na maji.
Mwananchi

No comments: