Tuesday, March 26, 2013

Kim Poulsen apewe mkataba mrefu Stars


Kocha Mkuu wa Taifa Stars Kim Poulsen

Kuna taarifa kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemuandikia barua ya kutaka kumpa mkataba mpya kocha Kim Poulsen wa timu ya taifa (Taifa Stars). Hatua hiyo imefikiwa baada ya kurugenzi ya ufundi ya TFF kuridhishwa na maendeleo ya Stars tangu ianze kuwa chini ya Poulsen katika kipindi cha mkataba wake wa mwaka mmoja unaomalizika miezi miwili ijayo.

Katibu Mkuu wa TFF amekaririwa akisema kuwa tayari wameshamtaarifu Poulsen kusudio lao la kumpa mkataba mpya na kwamba, kinachosubiriwa ni majibu yake kuhusiana na 'ofa' hiyo.

Sisi tunaipongeza TFF kwa kufanya uamuzi huo wa busara. Hii ni kutokana na ukweli kwamba Poulsen huyu aliyepewa kuiongoza Stars baada ya kuondoka kwa mtangulizi wake, Mdenmark mwenzie Jan Poulsen, ameleta mabadiliko makubwa kikosini na sasa walau timu yetu inacheza soka la kueleweka.

Hata hivyo, NIPASHE tunaamini kwamba jambo moja kubwa linalopaswa kuzingatiwa na TFF ni umuhimu wa kumpatia kocha huyo mkataba mrefu zaidi ya ule uliopita. Walau wamsainishe mkataba wa kuanzia miaka mitatu.


Inawezekana kuwa masharti mapya ya Poulsen kabla ya kusaini mkataba mpya yakawa na mahitaji ya ziada kulinganisha na mkataba wa awali. Hata hivyo, tunatambua vilevile kwamba hakutakuwa na kikwazo kuhusiana na rasilimali fedha kwani tayari serikali imeshaahidi kupitia kwa naibu waziri wake wa Habari, Vijana, utamaduni na Michezo kuwa iko tayari kuendelea kulipa mshahara wa kocha huyo na marupurupu yake baada ya kuridhishwa na mwenendo wa Stars na kwamba inachosubiri ni maelekezo tu kutoka kwa TFF.

Kutokana na ahadi ya serikali, TFF haina tena sababu ya kuogopa kumpatia mkataba mrefu Poulsen.

Awali, wakati wakimsainisha mkataba uliompa nafasi ya kumrithi mtangulizi wake, TFF ilikuwa na sababu za kutosha za kiufundi za kumpa mkataba wa mwaka mmoja tu. Kamwe isingekuwa busara kwao kumpa mkataba mrefu kocha huyo aliyekuwa akikinoa kikosi cha timu ya taifa ya vijana kwasababu hawakuwa na uhakika kama ataweza kuongoza vyema timu ya taifa ya wakubwa.

Hata hivyo, tangu Poulsen aanze kazi yake mwaka jana, Stars ya sasa imeonekana kuimarika zaidi.

Kocha huyo amewajumuisha kikosini wachezaji kadhaa aliokuwa nao katika timu yake ya taifa ya vijana na sasa, kasi ya Stars uwanjani imeongezeka.

Wanacheza kwa malengo ya kushinda, wakijitahidi kucheza pasi za kuvutia na kushambulia mara kwa mara kulinganisha na enzi za Jan Poulsen. Ushindani wa Stars dhidi ya wapinzani umeongezeka.

Matokeo ya mechi mbili zilizopita kabla ya mechi ya jana ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco yalidhihirisha kuanza kukomaa kwa Stars.

Walicheza dhidi ya waliokuwa mabingwa wa Afrika, Zambia na kuonyesha soka la kuvutia kabla ya kupata ushindi waliostahili wa goli 1-0. Wakashinda pia kwa idadi hiyo ya magoli katika mechi nyingine ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa zamani wa Afrika, Cameroon, ambao kikosi chao kinaundwa na nyota wengi wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya akiwamo beki Essou-Ekotto wa klabu ya Tottenham inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Hata hivyo, ieleweke kuwa NIPASHE hatuishauri TFF kumpa mkataba mrefu Poulsen kwa sababu ya ushindi wa Stars katika mechi hizo za kirafiki dhidi ya Zambia na Cameroon.
Bali tunaridhishwa na mtindo wake wa kuwapa nafasi zaidi vijana wenye vipaji na kuwapa mbinu zinazowafanya wacheze vizuri kulinganisha na Stars iliyopita.

Ikiwa Poulsen atapewa mkataba mrefu, ni wazi kwamba wachezaji watapata nafasi zaidi ya kujifunza mbinu zake na mwishowe Stars itaondoka kutoka katika kundi la timu dhaifu sana duniani na kuwa miongoni mwa timu za kuheshimiwa.

Tunaamini vilevile kuwa Poulsen akibaki na timu yake hii iliyojaa vijana kwa walau miaka mitatu, ipo siku Stars itatimiza ndoto ya kufuzu kwa fainali za michuano mikubwa kama ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ambayo kwa mara ya mwisho ilikuwa ni miaka 33 iliyopita; enzi za nahodha Leodegar Tenga ambaye hivi sasa ndiye rais wa TFF.

Tunaamini kwamba TFF itafanya kosa kubwa ikiwa haitompa Poulsen mkataba mrefu kwani akiachwa aondoke ndani ya muda mfupi ujao, Stars inaweza kurudi kulekule ilikotoka. Kocha mpya atakuwa na kazi kubwa ya kuwajua wachezaji wake na kuingiza mbinu nyingine za ufundishaji ambazo ni dhahiri zitawavuruga wachezaji.

Chonde chonde TFF. Mpeni Poulsen mkataba mrefu ili Stars iendelee kuimarika na mwishowe iwape raha Watanzania.


 
CHANZO: NIPASHE

No comments: