Tuesday, March 26, 2013

MAPENZI NI KUHAMA ULIMWENGU WA KAWAIDA NA KUZAMA KWENYE ‘MALAVIDAVI’ -2

MPENZI msomaji, leo naendelea kuelezea ‘topiki’ ya mapenzi ni kuhama katika ulimwengu wa kawaida na kuzama katika ‘malavidavi’. Tuwe pamoja...

WEWE NI RAFIKI MKUBWA (You’re my best friend)
Mwanamke wako anakupenda sana. Siyo tu kwamba anataka kuwa mpenzi wako bali pia anahitaji awe rafiki yako mkubwa. Mwambie kuwa huna rafiki mkubwa kama yeye chini ya jua. Mchombeze kwamba huna mtu mwingine wa kuchangia naye siri zako zaidi yake.
Hii inamaanisha kuwa mwanamke hapendi kuwa kimbilio lako la pili, daima hutaka kuwa wa kwanza ndani yako.

WEWE NI MUHIMU KWANGU (You’re the most important thing to me)
Inawezekana ukawa ‘bize’ mno na kazi. Unatumia muda wa wikiendi kuponda maisha na marafiki. Angalizo ni kuwa, usithubutu kumfanya mwanamke wako akahisi humuoni ni umuhimu kwako.
Pamoja na ‘ubize’ wako, tumia muda mchache unaoutumia na yeye kumuonesha jinsi alivyo muhimu kwako. Isiishie hapo, mtamkie kwa herufi kubwa: “Wewe ni muhimu kwangu kuliko kitu kingine chochote duniani.”
SIKUDANGANYI (I would never lie to you)
Mwanamke hujiamini pale anapobaini kuwa mwenzi wake ni mkweli. Anapokosea, hukiri na kuomba msamaha. Humchukia yule ambaye hujifanya kauzu, macho makavu anadanganya.
Mwambie humdanganyi na umaanishe unachosema. Hayo yakijaa kwenye ubongo wake, utakuwa umempatia kwa kiwango kikubwa.

SIJAWAHI KUKUSALITI (I have never cheated on you)
Jaribu kuanzisha mazungumzo kuhusu namna ambavyo unachukia usaliti. Mbele ya mazungumzo yako, mueleze kuwa unaridhika kuwa naye, kwa hiyo huwajawahi kumsaliti hata mara moja.
Ni kawaida ya wivu kukua muda baada ya muda lakini wewe unayo nafasi ya kumfanya asiwe na chembe yoyote ya kukuhisi unamsaliti.

NINGEPOTEA BILA WEWE (I’d be lost without you)
Ni katika kumfanya ajione yeye ni taa ya maisha yako. Mueleze kuwa kama si yeye, ungeshapoteza muelekeo wa kimaisha.
Kwa kawaida, mwanamke hataki tu kujua kuwa unampenda na kumtaka, ila unamhitaji kwa dhati, kwa hiyo ukimwambia ni yeye ndiye amekuweka kwenye mstari, atajiamini kuwa unamhitaji sana.

WEWE NI MCHESHI (You’re funny)
Daima tembea na kanuni hii. Wawili wanaopendana na kucheka pamoja ndiyo hudumu. Mpe uhuru akuchekeshe kisha uruhusu mbavu zako zivunjike kwa kicheko. Mwisho wa kicheko, gonganisha naye viganja halafu mwambie “wewe ni mcheshi sana mpenzi wangu.”

NAKUPENDA (I love you)
Ni neno la kawaida lakini kwa mwanamke huwa lina maana kubwa endapo litatamkwa na mtu anayempenda. Ni hatari kwa wanaume wengi wanapowazoea wapenzi wao, hushindwa kutamka neno hili lakini mwanamke hupenda kusikia akiambiwa hivyo.
Mwambie mpenzi wako jinsi unavyompenda, mthibitishie kuwa mapenzi yako kwake ni makubwa kupita kiasi.

VIPI KUHUSU WANAUME?
Wanawake wengi hulalamika kuwa wanaume ni watata kwenye mapenzi. Hulaumu kwamba ni ngumu kubaini vitu ambavyo wanaume huhitaji kutoka kwa wanawake.
Wanadai kuwa wakati mwingine hujitahidi kadiri ya uwezo wao kuhakikisha wanawapa furaha lakini wanaume huwa hawana hata msisimko.
Hapa chini, nimekuandalia vitu ambavyo wanaume huhitaji kwa wanawake wao. Moja kwa moja, mambo yakienda chanya huwa ni zaidi ya chombezo na hupagawa.

MAPENZI (Love)
Siku zote wanaume huangalia mapenzi kwa wenzi wao. Mara nyingi wanaume huwa wepesi kuonesha mapenzi kwa wanawake wao lakini ndani ya nafsi zao, hutegemea mambo mengi kama malipo (return) ya upendo waliotoa kabla.
Wanapenda, kwa hiyo nao huhitaji kupendwa ili waone mambo yanakwenda sawa.
Wanawake wengi huwa wanaficha hisia za kupenda, hili huwaumiza wenzi wao.

Itaendelea wiki ijayo.
GPL

No comments: