Tuesday, March 26, 2013

TAIFA HATARINI

Ujumbe mfupi wa maneno (SMS) wenye mlengo wa ubaguzi wa kidini dhidi ya serikali, umekuwa ukitawanywa kwa fujo, ule wenye sura ya Kiislam ukisindikizwa na maneno “watumie Waislam wenzako” na wa Kikristo ukielekeza “watumie Wakristo wenzako.”
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa baadhi ya watu ambao tunaamini wakisakwa watapatikana, wamekuwa wakitunga na kusambaza ujumbe mfupi kwa watu mbalimbali, wakiwahamasisha kuhusu jambo fulani kwa masilahi ya dini zao.

SMS hizo , zimekuwa zikikosoa serikali kwamba muundo wake upo kiupendeleo, zile zenye sura ya Kikristo zikidai Waislam wanapendelewa, vilevile za Kiislam zikidai Wakristo wanapendelewa.
Baadhi ya waandishi wetu ni miongoni mwa waliotumiwa ujumbe na watu hao ambao wanaweza kulitia doa taifa letu ikiwa hatua za dharura hazitachukuliwa.
Ujumbe unaosambazwa na watu hao una lengo la kuigawa nchi katika misingi ya kidini, hali ambayo kwa mpenda amani yeyote hawezi kukubali au kufurahia kwani wanaofanya hivyo wanahatarisha usalama na umoja wetu wa kitaifa.

Uchunguzi wetu umebaini kuwa baadhi ya wananchi waliotumiwa ujumbe wa aina hiyo wameonesha wasiwasi wao kwa vyombo vya usalama hasa polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kama wana habari hizo na kuchukua hatua.

“Siku za hivi karibuni kila mara ujumbe mfupi wa uchochezi husambazwa kwenye simu na watu wasiofahamika, mbaya zaidi vyombo vya dola havijasema chochote, ina maana hawana habari?” alihoji kijana mmoja aliyeomba jina lake kuhifadhiwa.

Mwananchi mwingine mkazi wa Mwenge Mlalakua jijini Dar es Salaam alikiri kupokea ujumbe wenye maneno ya uchochezi lakini akasema hajafanya kama alivyoelekezwa na mtumaji.
“Mtumaji ameandika aliyotaka kuandika kisha akanitaka nitume kwa watu wa dini yangu kumi, sikufanya hivyo maana niliona kuwa huu ni uchochezi,” alisema.

SMS hizo, zinataja asilimia ya viongozi waliopo madarakani kwamba ni wa dini fulani kisha ujumbe wenyewe unaonya kwamba muundo wa serikali ni hatari kwa usalama wa taifa bila kutaja sababu za hatari hiyo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela ametoa wito kwa yeyote ambaye atatumiwa ujumbe wa uchochezi kutoa taarifa kwake ili watu hao washughulikiwe.
“Kusambaza ujumbe wa uchochezi kwa kutumia simu au kitu chochote ni uhalifu na mhusika akikamatwa anashitakiwa, hivyo yeyote atakayetumiwa ujumbe wa uchochezi namkaribisha ofisini kwangu ili wahalifu hao washughulikiwe,” alisema Kenyela.
GPL

No comments: