Tuesday, March 26, 2013

MAREKANI YAFURAHISHWA NA MSIMAMO WA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano Zanzibar Dk. Juma Akil (wa pili kushoto) akiwa na  ujumbe wake Mhe.Said Hassan, Naibu Mwanasheria Mkuu wa SMZ(wa kwanza Kulia) na Bw.Abdi Maalim, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Meli Zanzibar (wa pili Kulia) na Bw. Suleiman Saleh(wa Kwanza Kushoto) Afisa wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Washington DC, walipowasili katika Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani tayari kwa mkutano na Viongozi na Maofisa wa Serikali ya Marekani.
Mhe. Peter E. Harrel(katikati), Naibu Waziri katika Wizara ya Nje ya Marekani anaeshughulikia Uchumi ,Biashara na Vikwazo katika picha ya pamoja na Mhe.Dk. Juma Akil,Katibu Mkuu,Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi (SMZ) (wa tatu kushoto), na Bw.Suleiman Saleh,Afisa wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Washington DC (kushoto) mara baada ya mazungumzo baina yao.
Mhe.Dk.Juma Akil,Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi wa SMZ (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mhe.Lily Munanka,(katikati)Kaimu Balozi wa Tanzania Washington DC wakazi alipofanya ziara katika Ubalozi huo( Tanzania House) na kumweleza kwa muhtasari yaliyojiri katika mkutano wake na Viongozi wa Serikali Marekani kuhusu msimamo wa SMZ kuvunja mkataba wake na Kampuni ya kusajili Meli ya Philtex iliyoko Dubai,UAE.Wengine kushoto ni Mhe.Said Hassan,Naibu Mwanasheria Mkuu wa SMZ (kushoto) na Bw. Abdi Maalim, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Meli la Zanzibar(wa pili kulia)na Bw.Suleiman Saleh,(kulia)Afisa wa Ubalozi wa Tanzania Washington,DC.

Serikali ya Marekani imefurahishwa na msimamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) wa kuvunja mkataba wake na kampuni ya Philtex ya Dubai,UAE ambayo ni wakala wa SMZ katika kusajili meli kimataifa. Msimamo huo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar uliwasilishwa rasmi na Mhe.Dk. Juma Akil,Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi wa SMZ katika mkutano wake na Viongozi na Maofisa wa Serikali ya Marekani uliofanyika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani,Washington DC, Ijumaa,Machi 22,2013, saa 6.30-hadi saa 8.30 mchana. Katika mkutano huo Dk.Akil aliambatana na Mhe.Said Hassan Said,Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bw. Abdi Maalim, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Meli la Zanzibar na Bw.Suleiman Saleh,Afisa kutoka Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Washington DC. Katika kikao hicho ambacho kilidumu karibu masaa mawili, Mhe. Peter Harrel ambaye ni Naibu Waziri katika Wizara ya Nje ya Marekani katika Idara ya Uchumi na Biashara inayoshughulikia vikwazo vya kiuchumi aliongoza upande wa Marekani katika mazungumzo hayo. Kwa ujumla Serikali ya Marekani ilifarijika sana na habari nzuri kwamba SMZ imepitisha uamuzi wa kuvunja mkataba wake kampuni ya Philtex na kilichobaki sasa ni utekelezaji tu wa azma hiyo na hivyo Serikali ya Marekani imeonyesha utayari wake wa kuona ni namna gani itaisaidia Zanzibar katika kipindi cha mpito itakapoachana na kampuni ya Philtex ili kuendelea na biashara na meli ambazo hazina utata na vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran. Aidha Serikali ya Marekani imependekeza mambo kadhaa kwa SMZ katika azma yake ya kupata wakala mbadala.

No comments: