Tuesday, March 26, 2013

Wajane wawili ndugu wauawa kikatili Geita

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Leonard Paulo.
Wajane wawili ndugu wakazi wa kijiji cha Ilirika, kata ya Nyarugusu wilayani Geita, wameuawa kikatili kwa kukatwa katwa mapanga mbele ya watoto wao wadogo na watu wasiojulikana.

Tukio hilo lilitokea saa 7:00 usiku wa kuamkia jana ambapo mmoja kati ya wajane hao, alitenganishwa mkono na kiwiliwili chake na mwingine kuchinjwa shingoni.

Kabla ya watu hao kufanya mauaji hayo, walivunja milango ya nyumba mbili tofauti kwa kutumia mawe makubwa maarufu kama `fatuma' walizokuwa wamelala.Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ilirika, Fabian Mugetha, amewataja waliouawa kuwa ni Chausiku Lukombe (60), aliyekatwa katwa sehemu kadhaa za mwili na kuchinjwa shingoni na kuachwa kichwa chake kikishikiliwa na ngozi nyembamba.

Mwingine ni Zuhura Lukombe (55), ambaye licha ya kukatwa katwa sehemu kadhaa za mwili, pia mkono wake wa kulia ulitenganishwa na kiwiliwili chake.
Mugetha alifafanua kuwa wakati wakitekeleza ukatili huo kwa mujibu wa maelezo ya watoto watatu walioshuhudia, wauaji hao walikuwa wameficha nyuso zao kwa vitambaa.

Mmoja wa watoto hao ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema baada ya watu hao kuvunja mlango na kuingia ndani, waliwaamuru kukaa kimya na kulala kifudifudi pamoja na mama yao.

Watoto waliokuwa wamelala na marehemu Chausiku wametajwa kuwa ni Mihambo Zakaria (9), mwanafunzi wa darasa la tatu, Chausiku Hamza (8), anayesoma darasa la pili na Kibibi Zakaria (14), mwanafunzi wa darasa la sita wote katika Shule ya Msingi ya Ilirika.

Marehemu wote hao ni wajane waliofiwa na waume wao kwa nyakati tofauti.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Leonard Paulo, alithibitisha kwa njia ya simu kuwapo kwa tukio hilo.
CHANZO: NIPASHE

Miili ya marehemu hao ilitarajiwa kuzikwa jana.
CHANZO: NIPASHE

No comments: