ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 23, 2013

MANCHESTER UNITED NDIO MABIGWA WA LIGI KUU UINGEREZA



MANCHESTER, ENGLAND
MANCHESTER UNITED imetwaa ubingwa mara ya 20, huku mchezaji wake, Robin van Persie anayevaa jezi namba 20 akifunga mabao yote matatu dhidi ya Aston Villa katika Uwanja wa Old Trafford.
Katika mchezo huo uliochezwa jana Jumatatu usiku, Manchester United ilipata bao la kwanza dakika ya kwanza na sekunde 23, kupitia kwa Robin van Persie aliyepokea pasi maridadi kutoka kwa Ryan Giggs.
Mpira ulianzia kwa Wayne Rooney, aliyetoa pasi kwa Antonia Valencia ambaye akiwa katika wingi ya kulia alimpa pasi Rafael ambaye alitoa pasi ndefu kwa Giggs aliyempasia van Persie.
Dakika ya 13, Van Persie alifunga bao la pili baada ya kupokea pasi ndefu kutoka kwa Rooney. Baada ya kupokea mpira huo, Van Persie aliunganisha moja kwa moja na kulifanya bao hilo kuwa miongoni mwa mabao bora msimu huu.
Dakika ya 33, Van Persie alifunga bao la tatu baada ya Shinji Kagawa kumtengenezea pasi Giggs aliyekimbia na mpira katika wingi ya kushoto na hakutaka kufunga mwenyewe, badala yake akampa pasi Van Persie aliyemaliza kazi.
Si tu kwamba, Van Persie alifunga 'hat trick' hiyo, lakini alifikisha mabao 24 katika Ligi Kuu England.
Mholanzi huyo, ambaye huvaa jezi namba 20 ameifanya Manchester United kutwaa ubingwa wa 20. Huo ni ubingwa wa 13 kwa Alex Ferguson ambaye alianza kuifundisha timu hiyo tangu mwaka 1986.
Kwa matokeo hayo, Manchester United imefikisha pointi 84 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote.
Katika mechi ya Jumapili ijayo, Arsenal watatakiwa kujipanga katika mistari miwili wakati Manchester United wakiwa wanaingia uwanjani kabla ya kuanza kwa mchezo ikiwa ni utamaduni wa England kuifanyia hivyo timu iliyotwaa ubingwa.
Man United wameivua ubingwa Manchester City huku zikiwa zimebaki mechi nne kumalizika kwa msimu wa ligi.

No comments: