ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 15, 2013

Mkuu wa Upelelezi afariki ajalini

NA RENATUS MASUGULIKO
Jeshi la Polisi mkoani hapa limepata pigo baada ya kifo cha Mkuu wa Upelelezi (RCO), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Maginus Mng'ong'o, kufariki kwa ajali ya gari.

Ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa 2:30 usiku katika Thidingo, wilayani Geita akiwa kwenye safari ya kikazi baada ya gari alilokuwa akiendesha kugongana uso kwa uso na gari aina fa Fuso T 467 ANG, lililokuwa likiendeshwa na Said Khalfan (38), mkazi wa jijini Mwanza.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishana Msaidizi wa Polisi, Japhet Rusingu, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba marehemu alikuwa kwenye safari ya kikazi akitokea kijiji cha Buseresere kuja Geita mjini na alikuwa akiendesha gari ndogo aina ya Toyota Corolla, lililokuwa na namba za usajili, T 429 BMN.

Alisema jeshi la polisi linamshikilia dereva wa fuso kwa uchunguzi zaidi. Aidha, hakuna abiria aliyejeruhiwa kwenye Fuso hilo akiwamo dereva.Kwa mujibu wa Kamanda Rusingu, mwili wa marehemu umesafirishwa jana mchana kwenda Iringa ambako maziko yatafanyika.

Alisema marehemu alikuwa mchapakazi na mwadilifu na kwamba kifo chake ni pigo kubwa. Alisema Jeshi la Polisi litamuenzi kwa mazuri aliyoacha.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochire, akizungumza kwa niaba ya Serikali, alisema kwa muda ambao marehemu amekuwa wilayani hapa amejenga mahusiano ya jamii kupitia mfumo wa polisi jamii na ulinzi shirikishi na hivyo kusaidia kupunguza uhalifu na jamii kujiona ni sehemu ya ulinzi.

Marehemu aliteuliwa kushika wadhifa huo Juni mwaka jana akitokea Kawe ambako alikuwa OCD. Ameacha watoto saba na mke mmoja
CHANZO: NIPASHE

No comments: