NIKIANZA na tathmini ya kimapenzi, kuhusu kundi la mwisho ambayo nilianza nayo wiki iliyopita, ni kwamba wanaounda kundi hili, nyoyo zao huwa hazisemi uongo kuhusu hisia zao za kupenda.
Hutulia mahali walipo bila kutetereka. Maisha yao siyo ya mitego, kwa maana hutawakuta wakijishughulisha kufuatilia nyendo za wenzi wao ili kujua makosa yao au kubaini kama wanawasaliti.
Wanajua kunyenyekea pale inapostahili wanyenyekee, kadhalika huwa hawachukui uamuzi wa papara hata pale wanapohisi kwamba wenzi wao watakuwa wanafanya usaliti. Umakini wao, huwafanya waonekane kuwa viumbe waliobarikiwa zaidi.
Wanaweza kuhisi kitu kinachokaribiana na ukweli lakini watapuuza kwa vile hawana ushahidi. Ni waangalifu sana kuzungumza au kufanya mambo ambayo yanaweza kuwakera wenzi wao. Siyo wabinafsi, huwekeza furaha zao kwa kuhakikisha wenzi wao ni wenye furaha.
Imani yao ni kwamba wenzi wao wanapokuwa na furaha ndipo nao wanaweza kufurahi. Ukiwafuatilia utagundua kwamba marafiki hawachukui nafasi za wapenzi wao. Hawapo kama wale ambao wanatumia muda mwingi vijiweni au baa na marafiki na kuwaacha wenzi wao wakiwa wapweke.
Ni hodari wa kuzingatia mzani. Maisha yao hayana longolongo. Ikitokea wakatekwa na Shetani, hivyo kutengeneza nyumba dogo, huwa hawahamishi mapenzi yote nje. Huendelea kuwajibika ndani ya familia zao kwa nidhamu na ufanisi wote unaotakiwa.
Kuna wanawake wa pembeni ambao huanzisha uhusiano na wanaume wa watu wenye sifa zinazowafanya waunde kundi hili. Hao huangukia pua pale wanapokosea njia na kuanza kuwarubuni wanaume hao wazitelekeze familia zao ili wao washike mpini.
Kiuhalisia, hawapendi usaliti. Kwa hiyo ukiwaambia waache wake zao, unakuwa kama umewafukuza. Nyumba ndogo zilizofanya jaribio la namna hiyo, ziliambulia kuachwa zenyewe. Hawa ni wanaume makini sana, ndiyo maana nikasema huwa hawakawii kujisahihisha pale wanapotoka nje ya mstari.
BAHATI MBAYA
Wana akili sana lakini kwa tabia yao ya kupuuzia vitu, baadhi ya wanawake hudhani ni mazezeta, hivyo kutaka kuwaendesha kama baiskeli ya miti au gari moshi. Utulivu na umakini wao, hutafsiriwa kama ubwege. Mwisho kabisa wanapokuja kuonesha upande wao wa pili wa sarafu, hutafsiriwa kwamba ndiyo wabaya.
Siyo watu wa mapepe, kwa hiyo huwapa uhuru wa kutosha wapenzi wao. Hii kwa wanawake wengine, hutumia fursa hiyo ndivyo sivyo. Matokeo yake hufanya usaliti, hivyo kuwaumiza wanaume wanaounda kundi hili.
Wakati mwingine, mwanaume wa kundi hili hukutana na wanawake mapepe. Wale ambao mitazamo yao ya kimaisha, inaishia kwenye kipengele cha fedha na starehe. Hapa hupata wakati mgumu, kwani hujitahidi kufundisha lakini wengine hawafundishiki.
Wao ni waaminifu lakini kutokana na misimamo yao na kutoyapa kipaumbele mapenzi ya kitandani, hujikuta wakisalitiwa mara nyingi sana. Maajabu yaliyopo ndani yao ni kuwa inawezekana kabisa akajua kwamba mke wake ni msaliti lakini akawa mtulivu kuchukua uamuzi mpaka apate ushahidi.
Wanaweza kukosa tendo la unyumba kwa muda mrefu kutokana na ‘ubize’ wao. Hili hugeuka fimbo kwao, kwani baadhi ya wanawake wao, hushindwa kuvumilia, hivyo kusaliti ndoa, usaliti ambao mara nyingi baadaye husababisha ndoa kuvunjika.
Wao ni wazalishaji mali, tatizo linalowatesa wanaume wengi wa kundi hili ni kwamba uzalishaji wao, huvunwa na wengine kutokana tamaa, kiburi na ujinga wa wanawake wao.
Itaendelea wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment