Lubumbashi, DR Congo. Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea TP Mazembe ya DR Congo, Mbwana Samata amesema viongozi wa klabu za Tanzania hawana malengo ya kutwaa ubingwa wa Afrika ila wanapigania kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu tu.
Samata alisema hayo wakati alipokuwa akihojiwa na waandishi wa mtandao wa klabu ya TP Mazembe wakati timu hiyo ilipokuwa imeweka kambi mjini Ndola, Zambia kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Alisema,”Viongozi wa klabu kubwa za Tanzania, Simba na Yanga hawana malengo ya kutaka kushinda ubingwa wa Afrika na kucheza mashindano ya FIFA ya klabu bingwa ya dunia, viongozi wanapigania kushinda Ligi Kuu tu.”
Samata alisema,”Viongozi wa TP Mazembe wana malengo ya juu, wapo tofauti na viongozi wa klabu kubwa za Tanzania, ndiyo maana TP Mazembe inakuwa klabu kubwa.
“TP Mazembe haionei wivu klabu nyingine za Afrika, ila zipo klabu nyingi za Afrika zinazoionea wivu, TP Mazembe ina vifaa vyote muhimu vya kuwaandaa wachezaji, ina miundombinu ya soka, ina wafanyakazi wanaoijua soka na ina wachezaji wenye kiwango cha juu,”alisema Samata.
Alisema, “TP Mazembe ina wachezaji nyota kutoka DR Congo, Ghana, Zambia, Tanzania na Uganda, naona faraja kuchezea klabu hii, nataka mwaka huu nitwae ubingwa wa Afrika nikiwa na klabu yangu ya TP Mazembe.
Nataka nicheze mashindano ya FIFA ya Klabu Bingwa ya Dunia, ambapo naweza kucheza dhidi ya Barcelona na kuonyesha uwezo wangu.”
Mwanacnhi
No comments:
Post a Comment