Thursday, May 16, 2013

Mtoni Mwenda Madafu wakataa kuuza nyumba zao

Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi, Anna Tibajuka.

Wakazi wa Mtoni  Mwembe Madafu  Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, wamesema hawawezi kuuza nyumba zao kwa fedha kidogo wanazoshurutishwa na madalali wa nyumba.

Wamesema watakuwa tayari kiziuza kwa bei inayolingana na thamani yake, lakini hawatakuwa tayari kuuza kwa bei ya kuburuzwa na madalali ya Sh. milioni 80.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa kamati ya wananchi hao wanaolalamikia kuuza nyumba zao kwa bei ndogo, Bakari Serungi.

Alisema Sh. milioni 80 ni hasara kubwa ukilinganisha na kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi, mchakato wa kupata kiwanja kingine kwa ajili ya makazi mapya.


“Lazima uuze kitu kwa malengo ya baadaye, unapokosea kufanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi majuto huwa mjukuu, tunahitaji kuuza, lakini kwa Sh.milioni 300,” alisema.

Alisema madalali waliwafuata wao, hivyo lazima wafuate bei yao na kwamba maamuzi ya kukurupuka yaliwagharimu wakazi  waliokuwa wakiishi Kurasini Shimo la Udongo kwa kuuza nyumba zao kwa bei ndogo.

Mmoja wa wakazi hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema baada ya kuona kuna ubabaishaji wa malipo, waliamua kumfuata mwekezaji anayeyahitaji maeneo hayo, Anwarali Dharamsi, kupata taarifa sahihi.

Alisema Dharamsi aliwaeleza kuwa anatafuta eneo, lakini kazi hiyo aliwapa madalali, hivyo halipo kwake, lakini yupo tayari kununua ekari moja kwa Sh. milioni 500.

Alisema Dharamsi aligundua kuwa madalali hao ndiyo wanaoshusha thamani ya nyumba zao kwa maslahi yao.

Alisema madalali hao walisababisha mgawanyiko wa waliokubali bei ya Sh. milioni 80 na wengine kuzikataa.  Walikubali kulipwa fedha hizo wengi wao ni wenye nyumba za urithi.

Meneja wa kampuni ya Usafirishaji ya TRH, ambayo inamilikiwa na  Dharamsi, Daud  Mlezi, akizungumza na NIPASHE  kuhusu malalamiko ya malalamiko ya wananchi kuwa anafanya udalali wa nyumba zao, alisema yeye ni Meneja  wa kampuni hivyo hawezi kugeuka na kuwa dalali.

“Siwezi kufanya udalali, mimi ni meneja, lakini  kuwa meneja hainizuii kuzungumza na madalali, kama yapo malalamiko kutoka kwa wenye nyumba wajitokeze hadharani,sijawahi kufika Mwenbe Madafu hata mara moja,” alisema.

Diwani  wa Kata ya Mtoni, Ally Kinyaka, alisema zoezi la kuuza na kununua ni haki ya muuzaji wenyewe, hivyo hakuna atayeshurutishwa kwa kuwa serikali haihusiki katika majadiliano ya kuuza mali ya mtu.

Alitoa kauli hiyo baada ya wakazi wa Mtoni Madafu kumlalamikia kuwa anawashawishi kuuza nyumba zao kwa Sh. milioni 80 ili kumpisha mtu binafsi kuendeleza eneo hilo.

Alisema kama diwani wa eneo hilo hakushirikishwa katika mchakato wa kupatikana kwa mwekezaji huyo na kuwa aliitwa katika kikao cha mtaa baada ya wananchi kukataa kuuza nyumba zao.

Kinyaka alisema ikiwa wenye nyumba watakubali kuuza nyumba zao, serikali ya mtaa itakuwa na wajibu wa kusimamia malipo na kuthibisha kuwa mwekezaji amewalipa wananchi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: