Thursday, May 16, 2013

Tanzania hatihati kwenda COSAFA


Kocha wa timu ya soka ya taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen

Kocha wa timu ya soka ya taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen, amesema kwamba Tanzania iko katika hatihati ya kushiriki mashindano ya Ukanda wa Nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA) kama ilivyotarajiwa kutokana na ratiba ya michuano hiyo kuwa karibu na mechi ya kusaka nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Tanzania imepangwa kucheza ugenini dhidi ya Uganda kati ya Juni 21 na 23 mwaka huu jijini Kampala na zitarudiana kati ya Julai 5 na 7 jijini Dar es Salam wakati na michuano ya COSAFA ambapo Taifa Stars ni timu mwalikwa mwaka huu itaanza Julai 2 hadi 16 huko Zambia.


Inatarajia kuanza dhidi ya Shelisheli Julai 6.

Akizungumza na gazeti hili jana, Poulsen alisema kwamba Shirikisho la Soka Nchini (TFF) lilifanya mawasiliano na Chama cha Soka cha Uganda (FUFA) ili kusogeza mbele tarehe za mechi hiyo lakini wapinzani wao wameonyesha nia ya kukataa kufanya mabadiliko yoyote.

Alisema kwamba alikubali Stars ishiriki mashindano hayo mwaka huu ili kuiandaa na mechi hiyo dhidi ya Uganda Cranes, lakini inaonekana kwamba nafasi haitapatikana.

"Sidhani kama tunaweza kwenda kushiriki kama tulivyotarajia, nilitaka kutumia mashindano hayo kujiandaa na mechi za CHAN lakini Uganda hawataki kusogeza mbele au kufanya mabadiliko yoyote tofauti na tarehe zilizopangwa awali," alisema kocha huyo raia wa Denmark.

Aliongeza kwamba bado anaamini mazungumzo kati ya TFF na FUFA yanaweza kuzaa matunda na watakapofanikiwa itasaidia kuijenga Stars.

"Hatujakata tamaa, bado tunasubiri majibu ya Uganda, nitasikitika endapo tutakosa nafasi ya kushiriki mashindano ya COSAFA, ni muhimu kwa ajili ya kujenga timu kama ilivyokuwa mwaka juzi tulipopeleka wachezaji vijana," aliongeza kocha huyo.

Tanzania ilifuzu kushiriki fainali za CHAN za mwaka 2009 zilizofanyika Ivory Coast baada ya kuwaondoa Kenya na Uganda iliyokuwa chini ya Bobby Williamson.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: