Thursday, May 16, 2013

Ripoti ya Elimu bungeni yaibua utata

Dar es Salaam. Kauli ya Serikali iliyotolewa bungeni juu ya kufutwa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne na sababu za kufeli kwa wanafunzi wengi, imeibua utata baada ya taarifa kadhaa kuonyesha kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilibariki mabadiliko ya mfumo mpya wa kupanga madaraja.
Taarifa ya Serikali iliyosomwa bungeni Mei 3, mwaka huu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi ilisema Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), lilifanya mabadiliko ya mfumo bila kushirikisha wadau.
“Baraza la Taifa la Mitihani lilikuwa linachakata alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika kwa kutegemeana na hali ya ufaulu wa mwanafunzi... lakini mwaka 2012 lilitumia mfumo mpya wa kuwa na viwango maalumu vya kutunuku (fixed grade ranges).”
“Tume imebaini kwamba, pamoja na mfumo huo kuandaliwa kwa nia nzuri, utaratibu huo mpya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika.
“Baraza la Taifa la Mitihani limeelekezwa kuzingatia kuwa pamoja na kwamba sheria ya kuanzishwa kwake inawaruhusu kufanya marekebisho ya mchakato wa mtihani, lakini marekebisho yoyote ya kubadilisha utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya mtihani lazima yahusishe wadau wote wanaohusika na mitalaa, ufundishaji na mitihani.”
Kwa mujibu wa vielelezo vilivyochapishwa na Gazeti la Wiki la Jamhuri, mfumo huo ulipitishwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa, kikao kilichokutana na kujadili mapendekezo ya Necta ya kubadili mfumo huo kiliongozwa na Waziri wa Elimu, Dk Shukuru Kawambwa na Katibu wake alikuwa Naibu Waziri wa Elimu, Philip Mulugo.
Muhtasari wa kikao hicho unaonyesha wajumbe wa mkutano huo walikuwa ni pamoja na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Selestine Gesimba, Kamishna wa Elimu,  Profesa Eustell Bhalalusesa, Paulina K Mkonongo, Marystella Wassena, T.E. Temu, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), Dk Primus Nkwera, Bunyanzu Ntmabi, H.A Lihawa wote wakiwa wajumbe kwa upande wa Wizara.
Kutoka Necta wajumbe walikuwa ni Dk C.E Msonde, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk Joyce Ndalichako, Mwenyekiti wa Bodi ya Necta, Profesa Rwekaza Mukandara pamoja na Profesa Sifuni Mchome, ambaye ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
Aidha, Gesimba alimwandikia barua Katibu Mtendaji wa Necta yenye kumbukumbu namba CAC.109/437/01N Desemba 12 mwaka jana akiliagiza kutumia mfumo mpya wa kukokotoa alama za mitihani ya kidato cha nne na sita.
“Tafadhali rejea kikao kilichofanyika tarehe 10/12/2012 katika ukumbi wa mikutano wa wizara kuhusu somo tajwa hapo juu (Maagizo ya kuhusu utaratibu wa matumizi ya viwango vya ufaulu katika mitihani ya kidato cha nne na sita).
“Viwango vya ufaulu vilivyopendekezwa na Baraza la Mitihani la Tanzania vitumike kwa mitihani ya Kidato cha Nne 2012 na Kidato cha Sita kwa mwaka 2012 tu.
“Viwango vya kutunuku (grade rage) vifanyiwe kazi zaidi ili kupunguza au kuondoa mrundikano (bunching) wa alama katika kundi moja.”
“Necta ifanye utafiti kuhusu matumizi ya alama za maendeleo kwa O level (kidato cha kwanza mpaka cha sita) na A Level (kidato cha tano na sita) na kutoa mapendekezo mapya ya matumizi ya alama za maendeleo (continuous assessment).”
“Utekelezaji wa maagizo haya ufanyike mapema ili mapendekezo yaliyowasilishwa yaweze kuanza kutumika katika Mwaka wa Fedha 2013/2014.”
Mbali na barua hiyo, Profesa Bhalalusesa aliandika barua kwa Katibu Mtendaji wa Necta, Novemba 14, mwaka huu kuhusu utaratibu wa matumizi ya alama za maendeleo ya mtihani na viwango vya ufaulu katika mitihani ya taifa.
“Rejea kichwa cha habari hapo juu na barua yako yenye kumbu Na. MTS. 1/29/VOL.XII/61 ya tarehe 20/09/2012. Kutokana na maelezo ya barua yako, Wizara imeridhia mapendekezo ya uwiano wa alama za maendeleo ya wanafunzi (CA) na alama za mtihani wa mwisho kubadilishwa kutoka alama 50:50 na kuwa 30:70.”
“Wizara inaridhia pia alama 15 zitokane na mtihani wa kidato cha pili kwa wanafunzi wa kidato cha nne.”
“Aidha, wizara inataka mlete mchanganuo wa jinsi alama 15 zilizobakia zitakavyopatikana ili kuleta uelewa wa pamoja. Vivyo hivyo, mchanganue utaratibu wa mgawanyo wa alama za maendeleo ya mwanafunzi wa kidato cha sita,” ilisema.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Dk Kawambwa alisema hawezi kuzungumza chochote na badala yake atafutwe Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha Ufaulu wa Mtihani huo, Profesa Sifuni Mchome kwa kuwa kwa sasa masuala yote yapo chini yake.
“Naomba nisi-comment (nisizungumze) chochote kwa sasa, muulizeni Profesa Mchome kwa kuwa sasa hivi mambo yote yapo chini ya tume, nikizungumza nitawaudhi,” alisema.
Hata hivyo, jana Profesa Mchome ambaye pia alikuwa mjumbe wa kikao kilichopitisha mapendekezo hayo ya awali, hakupatikana kuzungumzia madai hayo lakini juzi akizungumza na mwandishi wetu alisema tume yake ilibaini kuwa Necta na wizara walikubaliana mwaka jana kuanza kutumia kanuni hiyo na utekelezaji wake ukaanza mwaka jana jambo ambalo halikuwa sawa.
Alisema mabadiliko makubwa kama hayo yalipaswa kuchukua angalau miaka minne ili watoto waandaliwe kuanzia kidato cha kwanza na waje wapimwe wanapofika kidato cha nne.
“Vyote hivi ni vyombo vya Serikali (Necta na Wizara ya Elimu) kwa hiyo kujikosoa siyo tatizo, sisi tumeona hilo ni tatizo na tukapendekeza hivyo na Serikali ikaamua kujikosoa,” alisema.
Alisema kuwa baada ya mabadiliko yanayoweza kufanyika bila kushirikisha wataalamu wengi lakini suala la alama za mtihani kwa kuwa tayari matokeo yake yameonekana baada ya kujaribiwa, ni vyema wadau wakashirikishwa zaidi.
Mwananchi

No comments: