Dodoma/Zanzibar. Wabunge mashabiki wa klabu ya Simba wanaoshiriki vikao vya Bunge vinavyoendelea jijini Dodoma, jana walifanya kikao Msalato, nje kidogo ya mji lengo likiwa ni kupanga mikakati ya kuhakikisha timu inapata ushindi kwenye mechi ya kufunga msimu dhidi ya Yanga Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa.
Timu hizo zinakutana kufunga msimu, huku Yanga ikiwa tayari imeshatawazwa ubingwa kabla hata ya mechi kumalizika na Simba ikijihakikishia nafasi ya tatu kutegemea matokeo ya mchezo huo.
Juzi jioni Naibu Spika Job Ndugai, alitangaza bungeni wakati akisoma ujumbe wa maandishi wa Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani, aliouandika akitaka Ndugai kuwatangazia wabunge wanaoishabikia timu hiyo kukutana.
“Kuna mambo muhimu sana lazima niyatangaze sasa hivi, Mheshimiwa Ngonyani anawatangazia wabunge wote mashabiki wa Simba kesho (jana) wakutane kule wanakokutana Msalato kwa ajili ya kupanga mikakati,” alisema Ndugai.
“Hapa nimekaa na mwenyekiti wa Simba, Aden Rage na yeye kaniambia wale wote (Waziri wa Ujenzi John Magufuli) na Naibu wake (Gerson Lwenge) ni Simba pia,” alisema Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba (CCM) wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Ujenzi.
Juzi, Mbunge wa Urambo Magharibi, Juma Kapuya, alimshauri Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage kuwataka yosso wa Simba kuwafunga ‘babu’ zao wa Yanga.
Wabunge mashabiki wa Simba ni Rage (Mwenyekiti wa Simba), Ndugai (Kongwa), Ngonyani, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (Urambo Mashariki), Kapuya, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).
Idd Azzan (Kinondoni), Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Amos Makala (Mvomero), Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini) Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge, ( Njombe Magharibi), Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, (Mkuranga) na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli.
Wakati huohuo, mashabiki wa Simba wametakiwa wasiwe na hofu na wajazane uwanjani kuona timu yao ikiwaadhiri watani wao wa jadi, Yanga.
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Liewig na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ walitamba jana mjini Zanziba kuwa Simba iko imara na itaibwaga Yanga.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment