Wednesday, May 15, 2013

UMOJA WA MATAIFA WAJARIBU TENA KUISAIDIA SYRIA

Ubao wa matangazo ukionyesha namna ambavyo kila Nchi ilivyopiga Kura yake Azimio Kuhusu hali ya Syria, upigaji kura huo ulifanyika wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokutana siku ya Jumatano. Azimio hilo lilipitishwa kwa kura za ndiyo 107, za hapana 12 na 59 za kutofungamana na upande wowote. Madhumuni ya Azimio hilo ni kuchagiza usitishaji wa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchi humo. Ingawa Azimio hilo limepita lakini limelalamikiwa kwamba mchakato wake haukuwa wazi, shirikishi, halikuzingatia ushauri wa wajumbe wengine na lilikuwa limeegema upande mmoja.

Na Mwandishi Maalum
Wakati milipuko ya risasi na mabomu ikiendelea kurindima nchi Syria, huku mamia kwa maelfu ya raia wa nchi hiyo wakiendelea kuwa wahanga wa milipuko hiyo. Kwa mara ya tano Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limepitisha Azimio kuhusu hali ilivyo nchini humo likichagiza pande zinazohusika kusitisha mapigano.

Jana (Jumatano ) Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipigia kura Azimio nambari A/67/L. 63 kuhusu Hali nchini Syria. Azimio hilo liliwasilishwa mbele ya wajumbe wa Baraza na Qatar kwa niaba ya Umoja wa Falme za Kiarabu likiungwa mkono na nchi kadhaa yakiwamo baadhi ya mataifa makubwa isipokuwa China na Urusi.

Azimio hilo lilipitishwa kwa kura za ndiyo 107, hapana 12, na 59 za kutofungamana na upande wowote. Kati ya nchi zilizopiga kura ya hapana ni Urusi na Uchina, wakati Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa kati ya nchi 59 zilizopiga kura ya kutofungamana na upande wowote.

Pamoja na kwamba Azimio hilo limepitishwa bado nchi nyingi zikiwamo hata baadhi ya zile zilizopiga kura ya ndiyo, zimeelezea kutoridhishwa na baadhi ya vipengele vilivyomo ndani ya Azimio na namna mchakato mzima wa maandalizi yake ulivyofanyika.

Wawakilishi wa Nchi zilizopiga kura ya kutofungamana na upande wowote akiwamo Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, walipata fursa ya kuelezea sababu zilizowafanya wakafikia uamuzi huo.

Baadhi ya sababu kubwa zilizoelezwa na wawakilishi hao ni pamoja na, kwamba,mkachato wa majadiliano ya Azimio hilo haukuwa wazi, shirikishi na haukuzingatia hoja zilizotolewa na wajumbe wengine ikiwamo hoja iliyotolewa na Kundi la Nchi za Afrika ya kutaka uwasilishwaji wa Azimio hilo uahirishwe ili kutoa nafasi ya kulijadili zaidi.

Kwamba, Azimio hilo lilikuwa limeegemea upande mmoja na kuelekeza lawama na shutuma dhidi ya serikali ya rais Al- Assad kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa , huku likiwa kimya kuhusu ukatili na ukiukwaji unaofaywa na makundi yenye silaha yanayopigana nchi humo.

Kwamba, Azimio hilo lilikuwa linakaribisha uanzishwaji uliofanyika mwezi Novemba 2012 wa Muungano wa Kitaifa kwajili ya Mapinduzi nchini Syria na Makundi ya Upinzani(National Coalition for Syrian Revolution and Opposition Forces) kama chombo halali cha kusimamia na kushiriki majadiliano kuelekea mabadiliko ya kisiasa na serikali ya mpito.

Ukaribishwa wa muungano huo ndani ya Azimio, unaelezwa na baadhi ya wanadiplomasia hao kwamba kwanza haikuwa kazi ya Baraza Kuu ya kuutambua Muungano huo likini ilikuwa ni hatua inayoashiria mwelekeo wa kuiondoa kinyemela serikali iliyoko madarakani hatua ambayo siyo tu ni kinyume na sheria za kimataifa lakini pia ni uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi nyingine na ni jambo baya.

Kwamba, Azimio hilo halikuwa na chochote kipya ambacho kinaweza kuleta matumaini kwa raia wa Syria na kwamba lilikuwa halitoi usuluhisi wa kisiasa .

Kwamba, Azimio hilo halikuwa na mashiko kuletwa wakati huu ili hali ni siku chache tu zilizopita , Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na Urusi John Kerry na Bw. Sergey Lavrov walikuwa wametangaza nia ya kuitisha mkutano wa Kimataifa kuzungumzia hali ya Syria. Tangazo ambalo lilipokelewa vema na jumuiya ya kimataifa.

Pamoja na hoja hizo na nyingine nyingi wawakilishi wa nchi zilizopiga kura ya kutofungamana na upande wowote walieleza bayana kwamba kutounga mkono azimio hilo hakumaanishi kwamba walikuwa wanaunga mkono ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na machafuko yanayoendelea nchini humo.

Kwa upande wa wawakilishi waliopiga kura ya ndiyo kuunga mkono, hoja kubwa kwao ilikuwa ni kwamba kwa kupitisha azimio hilo, ili kuwa ni kujaribu kwa mara nyingine kwamba Jumuiya ya Kimataifa haijawasahau wananchi wa Syria.

1 comment:

Anonymous said...

DANGANYA TOTO WANAWACHAFULIA NCHI ZA WATU HALAFU ETI WANAJARIBU DANGANYA TOTO NDO MAANA NASEMA UKIENDA SHULE BWANA UNAJUA KUCHAMBUA HABARI ZA KILA AINA UNAPO ZISOMA SHULE INALIPA NENDENI SHULE WADAU MJUE MAMBO