NaAhmed Rajab
JAJI mstaafu Joseph Warioba na Tume yake ya Mabadiliko ya Katiba wametamka na wananchi wamewasikia. Jumatatu walimkabidhi Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal rasimu ya kwanza ya katiba mpya ya Tanzania waliyoipendekeza na Bilal akaizindua.
Wazanzibari walikuwa wakiisubiri kwa hamu na ghamu rasimu hiyo wakitaka kujua nini Tume itapendekeza kuhusu muundo wa Muungano. Kwa muda mrefu tumekuwa tukisema kwamba mchakato wa kulitafutia taifa la Tanzania katiba mpya lazima utaibadili sura ya Muungano na hautokuwa kama ulivyokuwa tangu uasisiwe.
Kwa mfano, tukisema kwamba haielekei ya kuwa Tume ya Warioba itapendekeza kuendelezwa kwa mfamo wa sasa uliopo wa serikali mbili za Muungano na Zanzibar.
Wala Tume isingelithubutu kupendekeza kuwako kwa mfumo wa serikali moja tu, mfumo ambao lazima ungeleta mpasuko mkubwa nchini humo. Pangalitolewa pendekezo hilo basi nina hakika kwamba pasingelikalika.
Tumekuwa tukisema kwamba wengi wa Wazanzibari wamechoshwa na mfumo uliopo wa Muungano na wakitaka ubadilishwe na pawe na Muungano wa mkataba badala ya huu uliopo wa Katiba.
Kuna wengine ambao wanasema wamechoshwa kabisa na Muungano wenyewe na wanataka Zanzibar iachiwe ijitoe. Hisia kama hizo pia wanazo baadhi ya watu wa Bara ingawa si zenye hamasa nyingi kama za Wazanzibari.
Wazanzibari, si wote lakini wengi wao, wamekuwa wakiupigia debe muundo wa Muungano utaoirejeshea Zanzibar mamlaka yake kamili ya kidola. Wamekuwa pia wakidai ifufuliwe rasmi ile iliyokuwa Tanganyika na ipewe nayo serikali yake na mamlaka yake kamili ya kidola.
Wazanzibari hao wamekuwa wakishikilia kwamba Muungano mpya uwe ni Muungano wa mataifa mawili yaliyo sawa kila moja likiwa linashughulikia mambo yake yenyewe kwa ukamilifu.
Kwa mfumo huu wa Muungano Zanzibar bado itapunjika. Muungano ulikuwa na nguvu zaidi ya hizo kwa muda wa takriban miaka 50 na Zanzibar haikupata natija ya maendeleo kama inavyostahiki.
Sijui kwa nini rasimu hii ya katiba inaziita nchi hizi mbili Tanzania/Bara na Tanzania/Zanzibar badala ya Tanganyika na Zanzibar. Kwa nini ionekane jambo la aibu kulifufua jina Tanganyikana kulipa hadhi yake na taifa hilo kupewa haki yake ya kuwa na serikali yake na utaifa wake?
Kabla ya kuja dhana ya Muungano wa Mkataba wengi wa Wazanzibari walikuwa wakipendekeza kuwa Muungano uwe na muundo wa serikali tatu. Pendekezo hili liliwahi kutolewa na Rais wa pili wa Zanzibar Sheikh Aboud Jumbe na wakati mmoja hiyo ndiyo iliyokuwa sera ya Chama cha Wananchi (CUF).
Rasimu hii ya kwanza iliyozinduliwa Jumatatu imependekeza kuwa Muungano wa Tanzania uwe na muundo wa serikali tatu. Pawepo na Serikali ya Tanzania/Bara, serikali ya Tanzania/Zanzibar na serikali ya shirikisho.
Aidha yale yaitwayo ‘mambo ya Muungano’ yamepunguzwa kutoka 22 na sasa kuwa saba. Hayo saba ni:
- Katiba ya Jamhuri ya Muungano
- Sarafu na Benki Kuu
- Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa
- Ushuru
- Ulinzi na Usalama
- Usajili wa vyama vya siasa na
- Uraia na uhamiaji.
Mambo haya saba ya Muungano yaliyopendekezwa kwa hakika ni mambo ambayo kwa jumla unaweza kuyaita kuwa ndiyo mambo yenye ‘nguvu za mamlaka.’ Kwa mantiki hiyo iwapo mambo hayo na nguvu hizo saba zitabakia katika Muungano, Zanzibar bado haitokuwa na mamlaka yake kamili.
Kinachofanyika hapo ni sawa na kile kilichofanywa na serikali ya kikoloni ya Uingereza ilipoipa Zanzibar serikali ya ‘madaraka ya ndani.’ Na tunaweza kuhoji kwamba serikali hiyo ya madaraka ya ndani ilikuwa na nguvu zaidi na hiyo inayopendekezwa na Tume ya Katiba kwa vile ilikuwa na wizara ya mambo ya ndani ya nchi.
Nimejaribu kutafuta maoni ya Wazanzibari kuhusu rasimu hii ya kwanza ya katiba na ninavyoona ni kwamba wengi wao wanasema kwamba mabadiliko hayo yaliyopendekezwa hayatoshi. Wanasema kwamba hayatoshi kwa sababu hayakidhi madai ya Wazanzibari wengi.
Hawasemi kwamba mabadiliko hayo hayana maanalakini wanachosema ni kwamba mabadiliko hayo bado yataufanya Muungano uidhibiti Zanzibari ilhali wanachotaka wao ni kupumua.
Mbali na ya Muungano kuna mengi yenye maana katika rasimu hii yanayopaswa kuungwa mkono. Kwa mfano, Tume ya Katiba imependekezwa kwamba Katiba itoe haki ya kuyahoji matokeo ya uchaguzi wa urais katika mahakama ya juu zaidi.
Tume imependekeza pia kwamba mshindi wa urais atangazwe iwapo atapata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa.
Jengine la kihistoria lililopendekezwa na Tume ni kwamba wagombea binafsi waruhusiwe kuwania viti vya toka ngazi za chini hadi cha urais. Pendekezo hili likikubalika litaitanua demokrasia nchini.
Jengine lenye maana lililopendekezwa na Tume ni kwamba idadi ya mawaziri wa Muungano isizidi 15 na mawaziri hao kabla ya kuzishika nyadhifa zao lazima kwanza waidhinishwe na Bunge la Muungano.
Kwa upande mwingine, mapendekezo yaliomo kwenye rasimu hii ya katiba yanaonyesha wazi kwamba sera ya CCM imeshindwa ya kutaka uendelezwe muundo wa Muungano wa serikali mbili.
Hivyo ni wazi pia kwamba msimamo wa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein na ule wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, umepitwa na wakati. Warioba na Tume yake wameling’amua hilo.
Kuna tofauti kubwa kati ya Tume hii ya Warioba na zile za Nyalali na Kisanga. Katika mchakato huu wa sasa kuna mabaraza ya katiba ambayo hayakuwepo wakati wa tume zilizotangulia. Jambo jingine muhimu ambalo limo katika mchakato wa sasa na ambalo halikuwepo kabla ni rasimu ya mwisho ya katiba itapigiwa kura na wananchi ili waamue iwapo wanaikubali au la.
Kwa hivyo, uamuzi wa mwisho hautokuwa tena katika mikono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kama ilivyokuwa wakati wa enzi za Mwalimu Julius Nyerere na Benjamin Mkapa.
Wala CCM hakitokuwa na uamuzi. Sasa uamuzi utakuwa wa wananchi. Wao ndio watakaoamua hatima ya Muungano na muundo wake.
Hatua itayofuata sasa katika mchakato wa kupata katiba mpya ya Tanzania ni kwamba rasimu hii ya kwanza ya katiba itabidi ijadiliwe na wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya.
Mijadala hiyo itafanyika baadaye mwezi huu bado mwezi wa Agosti mwaka huu.
Baada ya kupata maoni ya mabaraza hayo, Tume itakaa tena kuyatafakari maoni hayo na kuyaingiza katika rasimu ya mwisho ya katiba ambayo itawasilishwa mbele ya Bunge la Katiba. Baada ya hapo ndipo wananchi watapotakiwa waipigie kura rasimu hiyo katika kura za maoni zitazopigwa mwakani 2014.
Ikiwa rasimu hii ya sasa ya katiba ndiyo itayoibuka na kuwa ya mwisho ya kupigiwa kura na wananchi na kukubaliwa basi nina hakika kwamba huo utakuwa mfumo wa mpito tu.
Bado pataendelea kuwako na manung’uniko Zanzibar kwa vile wengi wa wananchi wa huko hawatoridhishwa na muundo huo wa serikali tatu uliopendekezwa katika rasimu hiyo. Lengo lao ni kutaka pawe na Muungano wa Mkataba.
1 comment:
Bw. Ahmed.
Inasikitisha kuona kwamba ni Wazanzibari zaidi ndio wanao nung'unika kuhusu muungano.
Mimi sio mwandishi wa habari hivyo sina utaalamu wa kuandika makala ndeeeefu.
Lakini kwa ufupi tu, Watanganyika nasi tumechoshwa na mwenendo wa Zanzibar kuona Tanganyika imeneemeka sana kutokana na muungano.
Hakuna faida yeyote tuliyoipata ila ni hasara tupu. Katika kuuchukulia muungano kama ni ufugu, Wazanzibari wamenufaika kwa mengi mno. Mnapata fursa ya kuishi Bara. Kumiliki mali na biashara kwa uhuru kabisa (Bakhrea na Wapemba lukuki) . Mnamiliki mali, ardhi, fursa za elimu, na ajira kwenye idara zote serikalini hata zile zisizohusu muungano. Mbona hukuzungumzia kuhusu Wazinzibar hawa? Tuwafanyeje sidi wa Bara katika huo muungano wa Mkataba?? Kwanza huo muungano wa mkataba ni upi? Wa aina gani? Yapi yatajiri humo?
Mimi binafsi nimechoshwa kuona Wazanzibar wanao nung'unikia muungano lakini hawaji na wazo la KUUVUNJA!
Hilo ndio suluhisho la matatizo yote. Halafu Wazanzibar wote mhame bara mrudi kisiwani kwenu. Hapo ndio mtakapo ona nini ilkuwa faida ya muungano.
Yaani mmekuwa kama watoto wasiotaka ku share chochote kile na wenzao. Inakera sana.
You guys want to have your cake and eat it too..
Hatutofika kokote kwa mwenendo huo.
Mimi fikra zangu zilikuwa ......
Iweko Serikali MOJA tu ya Muungano.
Hakuna cha Zanzibar wala Tanganyika. Ami sivyo, basi MUUNGANO UFE!!!
Ni mie Mbara Mkereketwa.
Post a Comment