Thursday, July 18, 2013

MAPENZI SAWA ILA JARIBU KUIHESHIMU IMANI YA MWENZAKO!

NDUGU zangu, licha ya kwamba baadhi yetu tuko kwenye swaumu, bado tunalo jukumu la kukumbushana yale ambayo yanagusa maisha yetu ya kimapenzi kwani mapenzi yataendelea kuchukua nafasi kubwa katika maisha yetu ya kila siku.

Katika ulimwengu wa sasa ukifuatilia utabaini kuwa, dini, kabila na rangi si vigezo vya kuangalia pale mtu anapotafuta mwenza wa maisha. Kutokana na hilo ndiyo maana leo hii unakuta Waislam wengi wako kwenye uhusiano wa kimapenzi na Wakristo.
Si suala la uhusiano wa kawaida tu bali pia wapo ambao wanafikia hatua ya kubadilisha dini ili waishi kama mke na mume. Hilo si jambo baya kwani dini zote ni sawa kwa kuwa zinaamini uwepo wa Mungu.
Ninachotaka kukizungumza hapa kinawagusa wale ambao ni Wakristo na wako kwenye uhusiano na Waislam. Kwa mfano, kama wewe ni mwanaume Mkristo na una mpenzi wako ambaye ni Muislam, unatakiwa kumuunga mkono ili aweze kutimiza kipengele hicho muhimu cha dini yake.
Lakini wakati usahihi ukiwa hivyo, nimeshaanza kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanawake wakieleza namna wapenzi wao wanavyowatibulia swaumu zao.
Malalamiko yamekuwa mengi ila huyu aliyejitambulisha kwa jina la Husna wa Magomeni jijini Dar anaweza kuwasilisha kile ambacho wengi wamenilalamikia na hatimaye akanisukuma kuandika mada hii. Hebu msikie:
Mimi naitwa Husna, dini yangu ni Muislam. Hivi karibuni nilibahatika kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanaume ambaye nilimpenda sana naye akaonesha kunipenda kwa dhati.
Yeye ni Mkristo lakini alisema baadaye tutaangalia ni nani abadili dini ili tuweze kuoana. Kwa kuwa nilimpenda, nilikubaliana naye. Kinachonifanya niombe ushauri kwako ni kwamba, juzi baada ya mimi kuanza kufunga, huyu mpenzi wangu amekuwa akinilazimisha jioni niende kufanya naye mapenzi.
Hili ni kinyume na imani yangu lakini mwenzangu naona hanielewi. Inafika wakati tukikutana mchana ananishikashika, nikimwambia aniache kwa kuwa nimefunga, anakasirika. Kwa kifupi naona uhusiano wangu unaelekea kusiko.
Ndugu zangu, yawezekana Husna ni mmoja tu kati ya wale ambao wanakutana na mazingira haya. Ninachoweza kusema ni kwamba, kama umetokea kumpenda mtu ambaye ana imani tofauti, iheshimu imani yake. Kama mpenzi wako ni Muislam, mpe uhuru wa kufanya ibada.
Usifikie hatua ya kumkataza mpenzi wako asifunge eti ili muwe huru kukutana na kufanya yale ambayo dini yake inakataza. Kwa kufanya hivyo kwanza utaonesha kutoiheshimu imani ya mwenzako lakini pia mapenzi yako yataonekana ni feki.
Ni vyema kipindi hiki ikiwezekana mkawa mbalimbali kama hamjaoana. Wasilianeni, shaurianeni, saidianeni na pale inapobidi kutaneni lakini kila mmoja ahakikishe anayaepuka yale ambayo yanaweza kutibua swaumu.
Wewe msichana ambaye una mpenzi wako Muislam unatakiwa kumsaidia mwenzako amalize kipindi hiki bila kumharibia. Usimvalie vivazi vya kimitego, usimtumie sms za kimapenzi zinazoweza kuamsha hisia za mapenzi na usilazimishe kufanyiwa yale ambayo huenda yakaharibu swaumu ya mwenzako.
Nasema hivyo kwa kuwa, wapo wasichana micharuko, wengine ni Waislam majina ambao licha ya kwamba huu ni mwezi mtukufu wao wala hawajali. Wanawavalia wapenzi wao kihasara, hawakawii hata kulazimisha wapewe penzi wakati wanajua ni dhambi kubwa katika kipindi hiki.
Nawasihi ndugu zangu tumuogope Mungu, yale yote yanayogusa imani zetu tuwe nayo makini kwani bila hivyo Mungu anaweza kutuadhibu na kujikuta tunayaona mapenzi ni machungu.

Global Publishers

No comments: