ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 6, 2013

Mkewe Slaa akwama kumtambua mwizi wake kortini

Mke wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, Josephine Mshumbushi

Mke wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, Josephine Mshumbushi, Ijumaa iliyopita alishindwa kumtambua kijana anayedaiwa kumpora vitu vyake kwenye gari katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea kabla ya kuanza kutoa ushahidi wa kesi ya wizi wa vitu hivyo inayowakabili Getisi Mturi, Gake Mwita, Salum Raphael na Charles Steven.

Baada ya Hakimu Hakimu Hellen Liwa kutamka Mshumbushi kumuonyesha kwa kidole mtu anayedaiwa kumuibia vitu hivyo, alifanya hivyo mshtakiwa mwingine ambaye hausiani na kesi hiyo, raia wa Malawi wakati akisubiri kupatiwa dhamana.

Raia huyo alitaharuki na kuieleza Mahakama kuwa mwaka 2011 alikuwa Malawi na wala hajawahi kuiba maishani mwake.

“Mnataka kunidondoshea jumba bovu mimi, mheshimwa naomba mnipe dhamana nikapumzike," alilalamika .
Baada ya kutoa maelezo hayo, Mshumbushi aliendelea kudai kuwa miaka miwili ni mingi hivyo inawezekana amemfananisha kijana huyo na yule aliyemwona wakati akimpora vitu vyake.

Mushumbushi alidai kuwa Julai 13, mwaka 2011, akiwa mjauzito alivamiwa na vijana na kuporwa simu ya mkononi, pochi, leseni ya udereva, kadi za benki, kamera na fedha taslimu Sh. 50,000 wakati akienda nyumbani kwake Boko.

Alidai akiendesha gari lake aina ya Toyota Harrier jeusi T932 ASH kwenye barabara ya Lugalo, akiwa katika foleni alimuona kijana anapita karibu na mlango wa gari lake mkono wa kushoto na ghafla alirudi nyuma na kuvunja kioo cha dirisha.

Alidai alihamisha gari lake kutoka upande wa kushoto hadi wa kulia karibu jirani na geti la Suma JKT ambako alisikia tena mlio wa risasi lakini alipotaka kujiokoa alishindwa kutokana na gari hilo kupinduka kwenye mtaro.


"Nilijaribu kufungua mlango ili niweze kukimbia lakini nilikutana na mtu mwingine aliyekuwa ameshika bastola nilimuomba asinidhuru bali achukue kitu chochote anachotaka," alidai.

Mshumbushi alidai mtu huyo alichukua vitu vyake hivyo na kutokomea.

Alipotakiwa tena na Hakimu kumtambua mtu huyo mahakamani hapo, aligoma kwa madai hataki kusema tena uongo.
Hakimu Liwa aliiahirisha keshi hiyo hadi Agosti 15, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: