Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, imefuta tuhuma za ugaidi zilizokuwa zikiwakabili makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku ikitoa tahadhari kwa wanasiasa kuepuka kulifanya suala hilo kuwa ni kitu cha kawaida katika jamii, la sivyo linaweza kusababisha madhara bila sababu.
Mbali ya kufuta shitaka hilo, Mahakama Kuu pia imesema kuwa washtakiwa Henry Kilewo na wenzake wanne, Evodius Justian, Oscar Kaijage, Seif Kabuta na Rajab Kihawa, wamebakiwa na shitaka moja ambalo ni kosa la kawaida la jinai, la kushambulia na kudhuru mwili. Mahakama hiyo imeamuru kwamba kesi hiyo irejeshwe na kusikilizwa Mahakama ya Wilaya Igunga, ikielezwa kuwa dhamana itakuwa wazi kwa washtakiwa.
Katika shitaka la kwanza la kesi hiyo ya marejeo Mahakama Kuu, namba 54/2013, Kilewo na wenzake, chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi, walidaiwa kumteka kwa nia ya ugaidi Mussa Tesha, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
Shitaka la pili ilidaiwa kuwa chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu, washtakiwa walimdhuru Tesha kwa kummwagia tindikali.
Washtakiwa hao walidaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2011, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga.
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua takriban dakika 45 jana mbele ya mahakama iliyofurika watu, Jaji Mfawidhi Simon Lukelelwa, alisema suala la ugaidi siyo kitu cha mzaha au kidogo kama linavyotaka kuonyeshwa na baadhi ya watu, akionya kuwa hali hiyo ikiachwa inaweza kusababisha madhara makubwa katika jamii bila sababu za msingi.
"Suala hili la ugaidi kwa siku za hivi karibuni limeshika kasi, linazungumzwa kwa mapana ndani na nje ya nchi, lakini inavyoonyesha mazungumzo hayo hayajaelewa undani wa madhara yake. Nchi ikiwa imekithiri kwa ugaidi kama inavyodaiwa, vitu vingi vingeathirika, uchumi, utalii na mambo mengine," alisema.
"Ni vizuri mambo haya yakapewa nafasi yake na kwa umakini mkubwa, yasije yakaleta madhara makubwa kwa nchi pasipo ulazima wowote. Hata neno ugaidi tafsiri yake haijajulikana vizuri, kila mtu anatafsiri zake. Mtu unayemuona wewe ni gaidi, anaweza kuwa mpigania uhuru kwa mwingine," alisema Jaji Lukelelwa akisoma hukumu hiyo.
Huku akirejea maamuzi ya kesi nyingine, Jaji Lukelelwa alisema ameridhika kuwa washtakiwa hawana hatia katika kosa la kwanza la ugaidi, huku akiwaonya waendesha mashitaka kuwa makini katika kuandaa mashitaka kwa kufuata sheria zilizopo na nyaraka za Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), zinazowaelekeza namna ya kufanya kazi zao, kwani siyo kila kosa la jinai ni ugaidi.
Katika uamuzi wake huo, Jaji Mfawidhi Lukelelwa pia alisema pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora kutokuwa na uwezo wa kusikiliza hoja za upande wa utetezi, kama zilivyoelezwa kwenye kesi namba 75/2013, kitendo cha Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Tabora, Issa Magori, kuchukua jalada la kesi hiyo ambayo haikuwa yake na kufanya uamuzi, kilikuwa ni kinyume cha sheria na taratibu za Mahakama.
Kwa mara ya kwanza watuhumiwa hao walisomewa shitaka la ugaidi Juni 24, mwaka huu, wakidaiwa walimteka na kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011.
Upande wa serikali uliwakilishwa na Wakili Juma Massanja na Ildefons Mukandara.
Awali, watuhumiwa hao waliposomewa shitaka, jopo la mawakili wa utetezi, Abdallah Safari na Peter Kibatala, liliomba mahakama hiyo iyafute mashitaka hayo kwa sababu ya kutokuwa na uhai.
Mawakili hao wa utetezi walidai kuwa mashitaka hayo hayana uhai kwa sababu yamefunguliwa bila ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Pia mawakili hao walidai kuwa sheria za uendeshaji wa makosa kama hayo hapa nchini zinadai kuwa mashitaka kama hayo yanapofunguliwa ni lazima ridhaa ya DPP iwepo, lakini ridhaa hiyo haipo, hivyo yatupwe.
Waliongeza sababu ya pili kuwa maelezo hayaonyeshi kosa husika ni la kigaidi, tofauti na makosa mengine ya kawaida kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hivyo waliomba yafutwe au yafunguliwe kama kosa la kawaida.
Upande huo wa utetezi pia ulidai kwa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya jinai, inaelekeza kuwa mshtakiwa ashtakiwe katika mahakama yenye mamlaka na hadhi kama ile waliyopelekwa katika maeneo yale walikokamatwa.
Hivyo mawakili waliiomba mahakama itupilie mbali shitaka kwani washtakiwa kama walikuwa na hatia walipaswa kushtakiwa katika maeneo yao walipokamatwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment