Dar es Salaam. Wanafunzi wa vyuo vikuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wameishangaa Tume ya Kurekebisha Katiba kwa kuyaondoa Maziwa Tanganyika, Victoria na Nyasa kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano kwenye rasimu ya Katiba.
Mwanasheria na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kilimanjaro, Evod Mmanda alisema katika rasimu hiyo haitaji maziwa hayo kama sehemu ya Muungano.Mmanda alisema hayo kwenye kongamano lililoandaliwa na Vyuo Vikuu mkoa wa CCM.
Rasimu hiyo iliyopo ibara ya pili inasema, “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya bahari,” alisema Mmanda.
“Rasimu hii inaondoa maziwa tuliyonayo nadhani yataenda katika nchi jirani kwa sababu hayajaonyeshwa kama sehemu ya Muungano,” alisema.
Alisema watanzania wanatakiwa kupitia vipengele vyote vilivyopo kwenye rasimu hiyo ili kuweza kupata katiba inayofaa. Wanafunzi wengi waliohudhuria kongamano hilo walipendekeza Muungano wa Serikali mbili tofauti na rasimu hiyo inayopendekeza Muungano wa serikali tatu.
“Hakuna haja ya kuwa na Serikali tatu wakati tumeshindwa kuisimamia serikali mbili, sasa hivi tujikite kuwa na muungano wa Serikali moja,” alisema John Magoti, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere.
Alipendekeza wagombea wa ubunge kuwa na umri wa miaka 18 badala ya 25 kama inavyopendekezwa na rasimu hiyo.
“Kama mwenye miaka 18 anaruhusiwa kupiga kura, iweje kugombea iwe miaka 25, huku ni kuwanyima haki vijana,” alisema.
Naye Justine Mkude wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, alisema kwa kuwa na serikali tatu kutakuwa na gharama kubwa za uendeshaji.
“Tutatue kero zilizopo katika muungano na si kuongeza mzigo mwingine,” alisema.
Mlezi wa Mkoa wa Vyuo Vikuu wa CCM, Januari Makamba alitaka vijana wasomi kugombea nafasi mbalimbali ya uongozi na kwamba wasiwaachie wababaishaji.
“Ni lazima nchi hii iongozwe na vijana wasomi tusiwaachie wababaishaji hatutafika kule tunakokwenda,” alisema Makamba.
mfumo wa sera nchini haufai
Mhadhiri kutoka shule ya elimu, Chuo kikuu cha Dar es Salaam (DUCE),Frateline Kashaga ameukosoa mfumo wa sera zinazoandaliwa hapa nchini akidai kukosa vipaumbele muhimu vya kumsaidia kijana wa Kitanzania katika kunufaika na uwekezaji wa rasirimali zake.
Kashaga alisema serikali imekuwa na utaratibu wa kuandaa sera za kumvutia mwekezaji bila kujali hatima ya ajira kwa vijana.
“Kwa mfano miaka ya 1998 vijana wengi wa Kanda ya ziwa Victoria walikuwa wanategemea ajira katika uvuvi lakini baada ya serikali kuwekeza makampuni vijana wengi wameingia kwenye maisha magumu, wanaitwa wavuvi haramu, ajira ni kidogo na serikali haina mwelekeo wowote wa kuwasaidia,”alisema Kashaga.
Kashaga aliongeza kuwa taifa haliwezi kuleta maendeleo kwa utegemzi wawekezaji kutoka nje ya nchi. “Ukiangalia mataifa tunayoyategemea yanaendesha uchumi wake kwa madeni Marekani kwa sasa ina deni la dola 6 trilioni,hali hiyo haiashirii jambo zuri kwa nchi zinazoendelea,”alisema Kashaga.
Akizungumzia matarajio ya nishati katika uchumi wa taifa, Waziri wa Nishati na madini Profesa Sospeter Muhongo alisema Watanzania wanatakiwa kuunga mkono harakati za uwekezaji katika sekta hiyo.
“Dunia kwa sasa inatazama niashati ya gesi kama mkombozi wa ukuanji wa uchumi kwa hivyo tunapaswa kujiandaa kwa miaka kadhaa ijayo kuingia katika ushindani wa soko la kuuza nishati, nchi itakuza uchumi, ajira zitapanuka na wataalamu tutakuwa nao,”alisema Profesa Muhongo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment