ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 5, 2013

SADC, AU, EU watofautiana ushindi wa Mugabe

Wafuasi wa Chama cha Zanu-PF kinachoongozwa na Robert Mugabe ambaye juzi alitangazwa kwa mara ya saba kuliongoza Taifa la Zimbabwe wakifurahia baada ya kutolewa kwa matokeo hayo.Picha na AFP
Harare. Baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Zimbabwe huku Rais Robert Mugabe akiibuka kidedea kwa mara ya saba, waangalizi wa Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU), na Jumuiya ya Kiuchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC), wametofautiana kuhusu matokeo hayo.
Wakati waangalizi AU na SADC wakisema uchaguzi huo ulikuwa huru na haki, wenzao wa EU wamesema kulikuwa na kasoro kadhaa.
Hata hivyo, AU na SADC walisema kulikuwa na hitilafu katika daftari la wapigakura kwani baadhi hawakuruhusiwa kupiga kura wakati walikuwa na haki ya kufanya hivyo.
Waangalizi wa EU wameeleza wasiwasi wao juu ya kutokukamilika kwa ushiriki wa wapigakura na kwamba kulikuwa na udhaifu kwenye mchakato wa upigaji kura pamoja na ukosefu wa uwazi.
Kwa upande wake, Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC), ilisema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, licha ya hitilafu mbalimbali zilizojitokeza.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Solomon Zwana, alisema iwapo kuna chama ambacho hakijaridhishwa na matokeo, kinaweza kufuata njia za kisheria.
“Tuna imani vyama vitaheshimu ahadi walizoweka kwamba watafuata njia za kisheria na si kuanzisha vurugu. Hilo ndilo tumaini letu na ujumbe wetu kwa wadau wa kisiasa,” alisema Zwana.
Zuma wa kwanza kumpongeza Mugabe
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amempongeza Rais mteule wa Zimbabwe, Robert Mugabe kwa kuchaguliwa tena kuliongoza taifa hilo la Kusini mwa Afrika.
Katika salamu zake, Rais Zuma aliwataka wapinzani kukubaliana na matokeo hayo kwa ajili ya kudumisha amani nchini humo.”
Zuma anaonekana kutofautiana na misimamo ya Marekani, Uingereza na Australia, zilizokataa kukubaliana na ushindi wa Mugabe.
Uchaguzi wa Zimbabwe umemrudisha madarakani Mugabe kwa ushindi wa asilimia 61 dhidi ya aliyekuwa Waziri wake Mkuu, Morgan Tsvangirai aliyeambulia asilimia 34.
Tsvangirai alisema kulikuwa na rafu na wizi wa kura na anapanga kwenda mahakamani kupinga uchaguzi huo.
Tsvangirai alifahamu mapema
Tangu kuanza kwa mchakato wa kura, Mgombea wa MDC, Morgan Tsvangirai aliapa kupinga matokeo hayo mahakamani na kusema chama chake kitasusia taasisi za Serikali.
“Hatutajihusisha na masuala yoyote ya Serikali... tutakwenda mahakamani kupinga matokeo haya,” alisema Tsvangirai aliyekuwa akiwania kiti hicho kwa mara ya tatu. Mugabe mwenye umri wa miaka 89, ameiongoza Zimbabwe tangu taifa hilo lilipopata uhuru wake kutoka kwa Waingereza 1980.
Baada ya ZEC kumtangaza Mugabe kuwa ndiye mshindi, Tsvangirai alisema uamuzi huo wa tume utaiyumbisha nchi hiyo.
Alisema kutokana na kitendo cha udanganyifu na kuiba kura katika uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita, Zimbabwe itaingia katika mzozo wa kikatiba, kisiasa na uchumi.
Mgombea huyo alitetea uamuzi wa MDC wa kuingia katika Serikali ya kugawana madaraka na Mugabe, ambaye alitoa amri ya kukamatwa kwake, kupigwa na kufikishwa mahakamani kwa madai ya uhaini.
“Kushiriki kwetu kumeiokoa nchi hii, kwani shule, hospitali zilifungwa. Tulikuwa tunatumia sarafu ya Zimbabwe ambayo haikuwa na thamani, hakukuwa na bidhaa katika maduka, kila mtu alikuwa katika mtafaruku,” alisema.
Akiwa mwenye hasira, Tsvangirai alisema: “Siku za kuishi kwa kudanganywa zimekwisha na Jumatano (keshokutwa) MDC itawasilisha ushahidi wake wa udanganyifu katika Mahakama Kuu.”
Tsvangirai alisema atawasilisha waraka wa ‘upungufu wote na hali zote za kuendewa kinyume na sheria’ kwa SADC na kutoa wito wa kuitishwa kikao cha dharura cha jumuiya hiyo. “Haimaanishi kwamba SADC na AU ndivyo vigezo vya kimataifa vya uchaguzi  wa huru na wa haki,” alisema Tsvangirai na kuongeza: “Niseme pia kwamba licha ya vikwazo tulivyokumbana navyo, baadhi yetu tuliamini kwamba uchaguzi huu ungesuluhisha matatizo ya kiuchumi na ya kisiasa hapa Zimbabwe.”
Tsvangirai alisema raia wa Zimbabwe watalazimika kubeba athari za uamuzi wa kisiasa na kiuchumi uliofanywa na Mugabe na Zanu-PF. Waziri wa Ulinzi, Emmerson Munangagwa alisema kwamba  matokeo hayo ni mabadiliko ya mchezo.
“Mataifa ya Magharibi sasa yatabidi kutafuta ngazi na kushuka... uchaguzi wa kidemokrasia umefanyika nchini Zimbabwe,” alisema Munangagwa.
Mwananchi

No comments: