Mtuhumiwa huyo ambaye amekuwa akisafiri huku na kule nchini kukwepa mkono wa sheria, amejulikana baada ya Jeshi la Polisi nchini kumtangaza na kuweka picha zake hadharani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Juma Abdul, mkazi wa Vingunguti.
“Sasa imegundulika kuwa mtuhumiwa tajwa hapo juu ndiye anayeimiliki isivyo halali. Kuna dalili kuwa mtuhumiwa huyo amegundua kwamba anatafutwa hivyo anakwepa kukamatwa na anajificha maeneo tofautitofauti ya jiji ikiwa ni pamoja na kusafiri sehemu mbalimbali hapa nchini kukwepa mkono wa sheria,” alisema Kova.
Wakati polisi wakihaha kumsaka mtuhumiwa huyo mwenye laptop ya marehemu Dk. Mvungi, pia wanaendelea kuisaka simu yake ya mkononi pamoja na wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kusababisha kifo cha Dk. Mvungi.
Hadi sasa watuhumiwa waliokwishakamatwa ni 10 ambao tayari majina yao yalishatolewa mapema na Polisi Kanda Maalumu inaendea kufanya jitihada kubwa kwa lengo la kuipata laptop hiyo pamoja na simu moja ya marehemu.
Watuhumiwa waliokwishakamatwa ni Msigwa Mpopela na
Chabago Magozi ambao wanadaiwa kuwa vinara wa uhalifu huo.
Wengine ni Ahemed Ally (40), Zakaria Rafael Masesa (25) na Longushi Semaliko Losingo (29), Paul Yamusi (29), Juma Hamisi (29) Mnanda Saluwa (40).
“Laptop hiyo ni muhimu sana katika kukamilisha upelelezi wa shauri hilo na katika taratibu za kipolisi mtuhumiwa wa aina hiyo anatakiwa kutafutwa kwa mujibu wa PGO No 238.”
Katika mazingira yaliyopo sasa chini ya kifungu No: 238 kifungu kidogo cha 5(a) cha sheria na taratibu za polisi katika suala la upelelezi la watu wanaotafutwa (wanted persons), sasa hivi mtu huyo ameingia katika sifa ya watu wanaotafutwa bila kificho ‘WANTED PERSON(S)’. (Sheria hii pia inatumika kimataifa).
Kamanda Kova alisema picha ya mtuhumiwa huyo imeonyeshwa katika vyombo vya habari ili mtu yeyote atakayemwona na kumtambua alijulishe Jeshi la Polisi kwa madhumini ya kumkamata na kupata laptop hiyo muhimu.
“Pamoja na hayo mtuhumiwa mwenyewe ni busara zaidi angejisalimisha kwani sasa kasi ya kumkamata itaongezeka na itakuwa inamhusu kila raia mwema wa Tanzania au nje ya nchi kutokana na urahisi uliopo kupitia mitandao ya habari,” alisema Kova.
Kwa mujibu wa Kova, polisi inawaomba raia wema wasisite kutoa taarifa zitakazosaidia kumkamata mtuhumiwa huyu kwani tukio la kuuawa kwa Dk. Sengondo Mvungi limeleta huzuni kubwa kwa wapenda amani na Watanzania wote kwa jumla.
Tayari bastola iliyoporwa nyumbani kwa marehemu Mvungi, imekutwa nyumbani kwa mkazi wa Kiwalani, Dar es Salaam.
Sambamba na bastola hiyo, vifaa vya kutengenezea milipuko navyo vimekutwa nyumbani kwa mkazi huyo, John Mayunga ‘Ngosha’ (56).
Hivi sasa Ngosha anashikiliwa na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kukutwa na silaha na vifaa hivyo.
Kova alisema kumbukumbu zinaonyesha kwamba Mayunga ni mhalifu mzoefu na hivi karibuni alimaliza kifungo cha miaka saba jela kwa makosa ya ujambazi.
Ngosha ni mtuhumiwa wa 10 kukamatwa kwa tukio hilo na polisi inaendelea na msako ili yeyote aliyehusika akamatwe pamoja na vielelezo vilivyobaki ili sheria ichukue mkondo wake.
“Kwa sasa tutakuwa tumebakiza kukamata wawili au mmoja ambao watakuwa wamebaki na simu na kompyuta ya marehemu, hivyo tunaomba wananchi na wadau waendelee kutoa ushirikiano kwa polisi ili kufanikisha,” alisema.
Dk. Mvungi ambaye alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na mwanasheria mkongwe alifariki Novemba 12 nchini Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa kutokana na kujeruhiwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi nyumbani kwake Kibamba, Novemba 3.
Hadi sasa kuna hofu miongoni mwa wadau wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa huenda taarifa muhimu na nyeti kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya zikawa mikononi mwa watu wasiostahili kupitia laptop ya Dk. Mvungi.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment