Christina Newa akisimulia mkasa mzima wa tukio la mauaji hayo yalitokea Novemba 19 Ilala Bungoni jijini Dar es Salaam baada ya mpenzi wake Gabriel Munisi kuwashambulia kwa risasi ndugu wa familia moja na kuwaua watu wawili na kisha yeye mwenyewe kujiua. (Picha na Francis Dande)
Christina Newa.
Dada wa Christina Newa, Carolyne Newa ambaye alimpoteza mume wake Capt. Francis Shumila katika tukio hilo, akisimulia maisha ya Christina Newa na mpenzi wake, Gabriel Munisi.
Katika tukio hilo Gabriel Munisi aliwashambulia ndugu wa familia moja na kuwaua watu wawili, Alpha Newa 'Nando' na shemeji yake Capt. Francis Shumila kabla ya yeye mwenyewe kujiua.
Christina alifafanua kuwa licha ya kutoa
taarifa za kutishiwa maisha katika kituo cha Polisi Kirumba jijini Mwanza na
Pangani jijini Dar es Salaam, polisi walipuuza tishio hilo huku
wakiwadhalilisha kwa kauli za kebehi.
Alisema uhusiano wake na Munisi haukuwa wa muda mrefu na
kwamba baada ya kubaini kuwa kijana huyo ana tabia ya ukatili alifanya kila
njia kuachana naye ikiwa ni pamoja na kwenda nchini Cyprus kwa ajili ya masomo.
Aliongeza kuwa akiwa nchini Cyprus Munisi alimpigia simu na
kumuomba atakaporejea kwa likizo asiijulishe familia yake ili apate nafasi ya kumpokea
akiwa peke yake.
“Ni kweli niliporudi likizo Munisi alinipokea na alionekana
kuwa mtu aliyebadilika kitabia na hata tukapanga safari ya kwenda Mwanza
tuliongozana katika gari dogo lakini tukiwa sehemu moja ya Singida alinishusha
na kunitolea bastola huku akiniambia nimueleze sababu ya kwenda kusoma nje bila
kumtaarifu,” alisema Christina.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo alimuomba msamaha na
hali ikawa ya utulivu mpaka walipofika Mwanza huku Munisi akiwa amezuia kila
kitu alichotoka nacho Cyprus ikiwemo Laptop.
Christina alisema kuwa hata hivyo hakuwa na wasiwasi na Munisi
baada ya kuona amebadilika na kwamba katika hali hiyo alimuomba ruhusa ya
kurejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya mambo kabla ya kurejea jijini Mwanza.
Alisema akiwa jijini Dar es Salaam, Munisi alipeleka Laptop
kwa mafundi kwa ajili ya kuondoa namba za siri na akaweza kuona picha
zinazomuonyesha Christina akiwa ufukweni na wanafunzi wenzake jambo aliloeleza
kuwa lilimkera na kuwa mwanzo wa mgogoro.
Huku akiushika mguu wake uliojeruhiwa kwa risasi Chrstina
alisema, baada ya hali hiyo Munisi alianza kumpiga kila wakati huku akimfungia
mlango asitoke nje mpaka atakaporudi na
kwamba hali hiyo ilidumu kwa muda mrefu mpaka alipopata msaada wa majirani
walioweza kuwataarifu polisi na kumuokoa
Baba wa Munisi awatimua
Chrstina alisema baada
ya kipigo cha mara kwa mara alilazimika kufikisha malalamiko yake kwa mzazi wa
Munisi ambaye hakutaka kuwasikiliza na kumtaka aondoke nyumbani kwake.
Alisema kutokana na
hali hiyo hakuwa na jinsi zaidi ya kurudi kwa Munisi na kuendelea kupokea
manyanayaso mpaka siku alipopata msaada kutoka kwa mpita njia aliyewasiliana kupitia
dirisha la nyumba yao.
Christina alisema alimpa namba za mama yake
mpita njia huyo ambaye aliwasiliana na mama wa Christina ambao walifika jijini
Mwanza na kufanya mawasilino na Polisi wa Mwanza na kufanikiwa kumuokoa.
“Siku Polisi
walipokuja nyumbani, Munisi hakuamini kama wanamfuata kwa heri akanilazimisha
tutoke pamoja nilikuwa na kanga tu mwilini na hapo ndipo tulipoanza safari ya kituoni kwa ajili ya kuandikisha taarifa,” alisema Christina.
Aliongeza kuwa wakiwa njiani kuelekea kituoni Munisi alipigia
simu kwa ndugu wa Christina na kumtaka awaambie Polisi kwamba hakuna tatizo, jambo alilosema alilitekeleza kutokana na hofu aliyokuwa nayo.
Chrstina aliongeza kuwa baada ya kufikishwa kituoni alikataa
kurudi kwa Munisi na ndipo akarejea jijini Dar es Salaam baada ya kutumiwa tiketi na ndugu zake.
Munisi amuwinda Dar
Alisema baada ya kurejea jijini Dar es Salaam, Munisi alianza
harakati za kutaka kupata msaada wa Polisi kutokana na vitisho vya Munisi
ambapo alifika katika kituo cha Polisi Pangani na kutoa taarifa pasipo kupewa msaada wowote.
“Pale Pangani tulimkuta mpelelezi mmoja, huyu bwana alitusaidia mwanzo mpaka ndugu yetu aliporudi lakini kuhusu vitisho vya bastola, alisema hayo ni mambo ya mapenzi na hayawahusu,”. Chrstina anasema baada ya kauli hiyo ya Polisi hawakuwa na njia ya kufanya na kuamua kutulia nyumbani kabla ya kubaini uwepo wa Munisi katika jiji la Dar es Salaam, aliyekuwa akifuatilia nyendo ya familia yao kila
siku.
Alisema mara kwa mara Munisi alikuwa akimtumia ujumbe wa simu
na wakati mwingine kwenda kugonga katika nyumba yao na kumueleza kuwa hawezi
kumuacha na kwamba ikitokea amemuacha atafanya mauaji katika nyumba zote tatu
za familia hiyo
Siku moja kabla ya Mauaji.
Christina alisema siku moja kabla ya mauaji kutokea alipokea
ujumbe wa simu kutoka kwa Munisi ukimsifia kuwa amependeza hali iliyozidi
kumtia hofu na kuamua kumueleza shemeji yake Kapten Francis Shumila ambaye aliahidi
kumlinda.
“Nilimwambia Shemeji juu ya ujumbe wa Munisi naye akaniambia
atanilinda na kama kufa ataanza yeye kabla ya kifo changu kumbe ndivyo
alivyomaanisha,”alisema Chrstina kwa hisia kali.
Wakati wa Mauaji
Akisimulia hali ilivyokuwa muda mfupi kabla ya mauaji Christina alisema wakiwa wanatoka getini walimuona Munisi akiwafuata kwa kasi na kisha kutoa bastola hali iliyomfanya shemeji yake Kapten Shumila ashuke katika gari kwa ajili ya kutaka kumtuliza.
Alisema wakati Shumila akishuka katika gari Munisi alimfyatulia risasi ya kichwa na kisha risasi zingine akizielekeza katika gari na kumuua Dada wa Chrstina aitwae Alpha pamoja na kumjeruhi mama yao mzazi sehemu ya begani.
“Alikuwa kama Mnyama na katika hali hiyo niliweza kumsukumiza mama chini kwa ajili ya kumuokoa huku tukiwa tayari tumejeruhiwa na wengine wameshauawa Munisi kuona wote tumelala chini ndipo akajimaliza na bastola akidhani kwamba wote alishatumaliza,”alisema Chrstina.
Mama mzazi wa Christina Newa ambaye alijeruhiwa na risasi begani akisaidiwa na mtoto wake, Carolyne Newa alipokuwa akirudi nyumbani baada ya kuruhusiwa na madaktari kutoka hospitali ya taifa Muhimbili alipokuwa akipata matibabu.
Pole mama....
Waombolezaji msibani.
Christina Newa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la mauaji lililofanywa na Gabriel Munisi kuwashambulia ndugu wa familia moja na kuwaua watu wawili kisha mwenyewe kujiua, katika eneo la Bungoni jijini Dar es Salaam.
Marehemu Captain Francis Shumila enzi za uhai wake.
Marehemu Captain Francis Shumila enzi za uhai wake.
MICHUZI BLOG
No comments:
Post a Comment