ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 28, 2013

Minziro: Nainoa Yanga kwa mapenzi

Dar es Salaam. Kocha msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro amesema hana wasiwasi kuhusu hatima ya kibarua chake kwani amefanya kazi muda wote bila ya mkataba wowote.
Kauli hiyo ya Minziro imekuja wakati kumekuwa na taarifa kwamba uongozi wa Yanga upo kwenye mazungumzo na kocha wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa kuhusu kuchukua nafasi ya nahodha huyo wa zamani wa Yanga.
Akizungumza na gazeti hili,  Minziro alisema amejiunga na timu hiyo kwa muda mrefu, lakini kwa kipindi chote hicho hajasaini mkataba wowote na klabu hiyo.
Minziro alisema amekuwa akifanya mazoezi na timu hiyo kwa muda wote kwa mapenzi yote japokuwa ukocha ndio kazi yake.
“Nilikuwa nafundisha JKT Ruvu, walinifuata na kuniomba nije kufanya kazi hapa,  nimefanya na makocha wengi, japokuwa sikuwa na mkataba wowote yote hiyo ni kutokana na mapenzi yangu kwa timu hii, lakini kama wameamua kunifukuza, nipo tayari kuondoka kwa sababu hizo ndizo changamoto za maisha,” alisema Minziro.
Alisema viongozi wa klabu hiyo bado hawajamfuata kumweleza suala hilo ila amekuwa akisikia tetesi hizo kupitia vyombo vya habari kwamba Mkwasa amechukua nafasi yake.
Minziro alisema kufukuzwa ni jambo la kawaida katika kazi hii na hawezi kumlaumu yeyote kwa uamuzi huo.
“Mimi ni kocha wa kiwango cha juu, nina uhakika wa kupata kazi sehemu nyingine na kufanya kwa mafanikio kama niilivyokuwa JKT Ruvu,” alisema.
Wakati huohuo; nyota kadhaa wa Yanga pamoja na kocha Ernie Brandts jana walikacha mazoezi ya timu hiyo kwenye uwanja wa Bora Kijitonyama.
Brandts alipewa notisi ya siku 30 na kutakiwa kuendelea kuinoa timu hiyo hadi pale uongozi utakapopata kocha mwingine, na tayari makocha mbalimbali wameshajitokeza kuomba ajira ndani ya klabu hiyo.
Lakini jana gazeti hili liliishuhudia kocha Minziro aliyekuwa akisimamia mazoezi naye alionyesha kushangazwa kwa kutofika kwa Brandts katika mazoezi hayo huku Meneja wa timu hiyo Hafidh Saleh akisema: “Katika kikao alikubali kuendelea kufundisha mpaka siku 30 zipite, Jumatatu kaja kawapa mapumziko wachezaji hadi leo sisi tumefika hajatokea sasa sijui kinachoendelea labda kesho (leo) atakuja.”
Taarifa ambazo gazeti hili ilizipata baadaye jana zilisema Brandts amegoma kuendelea kuinoa timu hiyo kwa siku 30 mpaka kwanza amalizane na viongozi wa klabu hiyo na jana jioni alikuwa akutane na viongozi wa klabu hiyo ambao walikuwa safari, Makamu Mwenyekiti Clement Sanga alikuwa Iringa wakati Seif Magari alikuwa nje ya nchi na alitarajiwa kurudi nchini jana.
Kwa upande wa wachezaji wengi hawakuonekana katika mazoezi hayo ya jana ambayo muda mwingi walitumia kukimbia kitu ambacho kilipondwa na baadhi ya mashabiki waliofika kushuhudia.
“Tulivyofungwa na Simba sawa sawa tu, mazoezi gani haya, wachezaji wanakimbia tu, hebu ona wachezaji wamechoka, hamna kitu hapa. Kwa mazoezi haya hata ubingwa tunaweza kuusikia kwenye bomba, hebu ona muda huu wameshamaliza mazoezi, wanaenda kufanya starehe tu, mpaka kesho tena. Mazoezi yenyewe si lolote si chochote,” alilalama mmoja wa mashabiki aliyefika kwenye uwanja wa Bora.
Wachezaji waliokacha mazoezi hayo ni Hamis Thabit, Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima, Emannuel Okwi, Hamis Kiiza, Juma Kaseja na Athuman Idd Chuji ambaye hata hivyo kocha Minziro alimkingia kifua Chuji kwamba ni mgonjwa.
“Wachezaji wote hawa wana matatizo ya kifamilia, wanaumwa malaria,” alisema Minziro huku akiangua kicheko.
Hata hivyo, nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub alionyesha kushangazwa na tabia ya baadhi ya wachezaji wenzake ambao wanaamua kukacha kufika mazoezini bila ya taarifa.
Mwnanchi

No comments: