ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 20, 2013

Mzimu wa mabomu ya Arusha watikisa tena

  Aliyebambikiwa kesi atinga bungeni
  Pinda asema siyo rahisi kutoa majibu
Mzimu wa milipuko ya mabomu yaliyotokea kwa nyakati tofauti Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olasiti na mkutano wa Chadema viwanja vya Soweto jijini Arusha, umemuibua mkazi wa Nzega kutinga bungeni akilalamikia kuteswa na kubambikiwa kesi ya kuhusika na matukio hayo.

Mkazi huyo, Almas Apolo Mangapi, alidai wakati akizungumza na waandishi wa habari bungeni jana kuwa wakati akiteswa na polisi kikosi kazi kutoka Rorya, mkoani Mara, alikuwa akilazimishwa kumtaja Mbunge wa Arusha, Godbless Lema (Chadema), kuwa anahusika na milipuko hiyo.

Mlipuko wa bomu la kanisani ulitokea Mei 5, mwaka huu, wakati Balozi wa Vatican nchini na mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francis, Askofu Mkuu Francisco Padilla, akiongoza misa ya uzinduzi wa parokia hiyo akishirikiana na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu.

Katika mlipuko huo watu watatu walifariki dunia na zaidi ya 70 walijeruhiwa kati yao vibaya.

Aidha, mlipuko wa Soweto ulitokea Juni 14 mwaka huu na kuua watu wanne na wengine karibu 100 kujeruhiwa kati yao vibaya.

Mlipuko huo ulitokea wakati Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyekuwa akimalizia hotuba yake ya kufunga kampeni za chama chake na huku wanachama wakijiandaa kufanya harambee.

Mkutano wa Chadema ulikuwa wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani kwa kata za Themi, Elerai, Kaloleni na Kimandolu.

AELEZA YA MOYONI
Mangapi aliyesema alizaliwa, kukua na kusoma Nzega, awali alikamatwa kushtakiwa na kisha mwaka 2010 kufungwa jela miaka 30 kwa wizi wa kutumia silaha, aliweza kushinda kesi yake baada ya kukata rufaa Mahakama Kuu na kuachiwa huru. Aliruhusiwa kutoka gerezani Mei 23 mwaka huu.

Alisema Oktoba mwaka 2010, alikamatwa Dar es Salaam kwa tuhuma za kupora dhahabu kwa kutumia silaha katika mgodi wa Buzwagi na kisha akapelekwa Mwanza akiwa chini ya ulinzi na baadaye alipelekwa Geita kujibu mashtaka.

Alisema baada ya kutoka gerezani alikwenda kuripoti kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Nzega, aliyemtaja kwa jina moja la Sarungi, na kueleza: “Nimeachana na wizi na sasa mimi ni raia mwema.”

Hata hivyo, alisema Agosti 5, mwaka huu, akiwa nyumbani kwa mwenzake aliyemtaja kuwa Bernard John, walikamata na polisi wa kikosi kazi kutoka Rorya ambao baada ya kupekua nyumba hiyo walimbambikia mabomu mawili ya kutupwa kwa mkono.

“Baadaye polisi hao walinitaka twende nyumbani kwangu kufanua ukaguzi na tulipofika kwa kuwa niliona walivyombambikia mwenzangu mabomu nyumbani kwake, nilishtuka na kuwaomba kuwakague kwanza,” alisema.

Aliongeza: “Polisi mmoja alikataa akisema hawezi kukaguliwa na hivyo akatoka nje, lakini wenzake walikubali. “Nilifanya hivyo kwa lengo la kujiridhisha na kisha waliingia ndani ya nyumba kufanya kukaguzi na baadaye wakanipeleka kituo cha polisi cha Nzega.”

Alisema akiwa kituoni hapo hakupigwa, lakini alipopelekwa Kahama na kukaa mahabusu kwa siku saba alipigwa sana.
Alisema baadaye alipelekwa mkoani Arusha na kuwa shtaka lake lilikuwa ni kuhusika na milipuko ya mabomu yaliyotokea kanisani Olasiti na kwenye mkutano wa Chadema.

SITASAHAU KIPIGO, MATESO
Alisema ameumizwa sehemu za siri kwa kubanwa hali ambayo imemfanya apate majeraha na mguu wake kuumizwa na hivyo anashindwa kutembea vizuri.

Alisema alipata kipigo na mateso hayo akishinikizwa akubali kumhusisha Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), kuhusika na matukio ya milipuko hiyo.

ASAINDIKIZWA KWENDA ARUSHA
Alisema alipofikishwa maeneo ya Minjingu mkoani Manyara, polisi walimwingiza porini na kuendelea kumpa kipigo wakimshinikiza chini ya mtutu wa bunduki akubali kusema Lema amehusika na hapo ndipo itakuwa salama yake, lakini alikataa na kukubali kufa.

“Nilitakiwa kumtaja Lema na raia mmoja wa Kenya aitwaye Kamau kuwa alihusika na milipuko hiyo,” alisema.

Alisema alipofika Arusha pamoja na Bernard waliwekwa rumande maeneo tofauti na baada ya siku nne yeye alipelekwa kwa kikosi kazi cha hapo kuhojiwa na makamishna wa polisi.

Alisema aliwaeleza kuwa wakati matukio hayo yakitokea yeye alikuwa gerezani, hivyo asingeweza kuhusika nayo na kwamba Lema hamfahamu kwa sura licha ya kumuona kwenye picha.

“Baada ya hapo nilipelekwa tena rumande kwa siku mbili kisha nilitolewa na kusarishwa Nzega hapo ndipo nilipoweza kuonana tena na Bernard, lakini baadaye mimi nilipelekwa Kahama na kisha Shinyanga na Septemba 8, nikapelekwa Mwanza.

“Lakini hata hivyo, nilirudishwa tena Nzega ambako sasa nilifunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kupatikana na mabomu.

“Desemba 16 nilipelekwa mahakamani ambako nimepata dhamana,” alisema na kuongeza, zaidi ya miezi minne amekuwa rumande.

MBUNGE NASSARI ANENA
Akizungumzia tukio hilo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), alisema wanatarajia kulifikisha suala hilo kwa wananchi na pia kwa mabalozi wa nchi za nje ambao ofisi zao zipo nchini.

“Ikibidi tutatembea naye mahali popote nchini na kuelezea hali ilivyokuwa kuhusu tukio la kijana huyo na la milipuko ya mabomu yaliyotokea Arusha.

MBUNGE LEMA ANENA
Mbunge Lema alisema tangu kutokea kwa milipuko ya mabomu hayo kumekuwa na propaganda nyingi zinazotolewa na serikali kukishusisha chama hicho na viongozi wake.

“Tukio hili la kuteswa kwa Apolo, kubambikiwa kesi na kumlazimisha anitaje linaonyesha dhahiri jinsi polisi walivyokuwa na nia ya kunibambikia kesi na kuniua.
“Mabomu yote hayo mawili na kadiri siku inavyokwenda, waliopiga lile bomu Olasiti ni maelekezo.

“Sasa hivi walikuwa wakimtaka huyu Apolo anitaje kuwa nimehusika na milipuko ile nibambikiwe kesi…ninamshukuru Mungu na ninasali sana, kama huyo asingekuwa amefungwa gerezani leo hii asingekuwa na ushahidi wa kutosha na hivyo mimi ningebambikiwa kesi hii,” alisema.

Lema alisisitiza kwamba chama kina ushahidi kuwa aliyelipua mabomu hayo ni polisi na njia pekee ya kutafuta ufumbuzi ni kwa Rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya uchunguzi.

Swali la Nassari kwa Waziri Mkuu
Katika swali lake la papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Nassari alitaka kujua nia ya serikali ya kubambikiza watu.

“Masuala ya ulinzi na usalama ni jukumu namba moja la serikali, masuala ya ulinzi kwa wananchi na mali zao ni jukumu la serikali, masuala ya utoaji na upatikanaji wa haki kwa wanachi suala la serikali.

“Sasa sisi tuliokuwa wahudhuriaji wakubwa wa magerezani tumeshuhudia malalamiko mengi ya watu ambao wamebambikiwa kesi na kwamba malalamiko hayo yamekuwa yakifishwa ofisi za wabunge ili wayafanyie kazi.

“Sasa ni nia ya serikali kutumia vyombo vya dola kuwabambikia watu kesi,” alihoji.

Katika jibu lake Waziri Mkuu Pinda alisema: “Sio nia ya serikali kuwambikia watu kesi, inategemea kesi na kesi…sasa kama una mfano maalum ambao unaomba serikali iutazame unaweza kufanya hivyo, lakini sio kweli kwamba wote waliomo magerezani basi wamefikishwa humo kwa kesi za kubambikizwa siyo kweli.”

Alitamka Nassari kama ana kitu au jambo maalum basi awalisilishe ili aone namna gani kama serikali inaweza kufanya.

Jibu la Pinda lilimlazimisha Nassari aanze kuelezea tukio la kijana Apolo bungeni na akahoji kama huo ndio mkakati wa serikali wa kuwanyamazisha viongozi wa Chadema kwa staili hiyo ya kuwabambia kesi.

Waziri Mkuu walijibu: “Mheshimiwa Spika, kwanza siyo rahisi kujibu swali la Mheshimiwa Nassari kama alivyouliza. Wewe una taarifa zote alikamatwa wapi, alipelekwa wapi alifanywa nini na sasa unataka Waziri Mkuu asema anasema nini hapo.”

“Lakini jambo moja nataka nisema, suala lile bomu la Olasiti na baadae pale Soweto halikuwa rahisi hata kidogo…kuna msukumo mkubwa watu wanataka wajue nani alilipua na kwa nini alilipua…sasa juhudi za serikali bado zinaendelelea katika kuona nani alilipua…sasa haya mambo ambayo unanieleza hapa unatakiwa uandike, unipe nami nitawapa wizara husika ili wajue kama kuna maeneo ambayo tumekosea hapo tunaweza kusema,” alisema.

Majibu hayo yalimfanya Lema kusimama na kuomba kuulizwa swali na alianza kwa kusema: “Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kabisa lile bomu la Olasiti na pale Soweto, lilifanywa na …..”

Hata hivyo, Spika Makinda baadaye alimzuia Lema kuuliza swali hilo akimweleza kuwa kanuni haziruhusu kuendeleza swali lililokwishaulizwa.

Majibu hayo yalimfanya Lema kusema: “Mlitaka kuniua na kunitengenezea kesi kwa hiyo Mheshimiwa sitakuwa na swali lingine tena kwa siku ya leo.”

Spika Makinda aliwataka Nasarri na Lema kumwandikia Pinda kwa maandishi.

Wakati huo huo huo, kijana Apolo baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari alichukuliwa na polisi na maofisa wa Idara ya usalama wa Taifa kwenda kujiridhisha kama alipata dhamana katika kesi yake ya kukamatwa na mabomu.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Unknown said...

Sometimes i dont recognize my own country