ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 20, 2013

Okwi: Nitaichezea Yanga kwa mapenzi makubwa

Dar es Salaam. Mshambuliaji mpya wa Yanga, Emmanuel Okwi kutoka Uganda ametua nchini kuja kuitumikia klabu hiyo na kusema ataichezea kwa mapenzi makubwa.
Mchezaji huyo wa zamani wa Simba alitua jana saa 9:30 na kulakiwa na viongozi wa Yanga na mashabiki wachache wa klabu hiyo waliojitokeza kumpokea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Okwi aliyesajiliwa Yanga kwa mkataba wa miaka miwili na nusu alitua nchini na ndege ya Shirika la Rwanda na kupokewa na Abdallah Binkleb, Musa Katabalo na Seif Ahmed ‘Magari’.
Akizungumza mara baada ya kutua uwanjani hapo, Okwi ambaye alizaliwa Desemba 25, 1992 alisema: “Mimi ni mchezaji na mpira ni kazi yangu, nimekuja kuichezea Yanga na nitaitumikia kwa mapenzi yangu yote. Nimekuja kufanya kazi na si kuiangalia Simba. Mkataba wangu na Simba ulishaisha.”
Kuhusu utata wa usajili wake Yanga, Okwi alisema: “Mimi hayo mambo siyajui, nimeyaacha mikononi mwa viongozi wa Yanga ndio watakaomaliza hilo suala.”
Akizungumzia mechi ya Yanga na Simba itakayofanyika Jumamosi alisema: “Mimi nipo fiti. Nipo tayari kucheza mechi ya Simba. Nimejiandaa kikamilifu, ila mwenye uamuzi wa mwisho wa mimi kucheza au kutocheza ni kocha, kama atanipanga nitafurahi zaidi.”
Okwi amejiunga kambini na wenzake jana jioni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya Nani Mtani Jembe, Jumamosi.
Simba ilimuuza Okwi kwa Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia kwa dola 300,000 za Marekani ambazo klabu hiyo ya Msimbazi haijalipwa hadi sasa.
Simba walikubaliana na klabu hiyo walipwe hadi Septemba mwaka huu, lakini haikuwa hivyo na kufungua kesi kwa Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa) ikidai fedha hizo.
Wakati Simba ikidai fedha hizo, Okwi aliikacha Sahel akidai hajalipwa mishahara yake na Fifa ikaamua kumpeleka SC Villa ya Uganda ili acheze kwa miezi sita kulinda kiwango chake baada ya Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa) kuomba kwa Fifa.
Villa imemuuza kwa Yanga na Fufa kubariki lakini imeandika barua Fifa kuulizia uhalali wa usajili wa mshambuliaji huyo.
Mwananchi

No comments: