Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekanusha tuhuma dhidi ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, kwamba alihongwa na Nimrod Mkono pamoja na Rostam Azizi, kikieleza kwamba ni uzushi na uongo uliopangwa kukichafua na kuilaghai jamii.
Pia kimesema, Mbowe amekwishawasiliana na mawakili walifanyie kazi suala hili kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.
Taarifa ya Chadema iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam na Ofisa wake Mwandamizi wa Habari, Tumaini Makene, ilieleza kuwa uzushi huo unalenga kukichafua chama hicho ili kionekane hakina tofauti na chama kilichoko madarakani.
“Matokeo ya uongo huo ni kutaka kuisaidia CCM na kugeuza mjadala.
Kwa uhakika tunapenda kuiambia jamii ya Watanzania wote kwamba; chama wala Mwenyekiti wa Chama Taifa, mahali popote na wakati wowote, hajawahi kupokea msaada wa fedha hizo kutoka kwa waliotajwa kwa malengo yaliyosemwa.”
“Tungependa kuwaambia waliozusha tuhuma hizo, ni vyema kama wanapenda kutunza heshima kidogo waliyobakiza katika jamii kutokana na kuelemewa na mzigo wa tuhuma za utovu wa maadili na usaliti dhidi ya Chadema, badala ya kugeuka kuwa mabingwa wa kupika uongo, wajibu masuala ya msingi yanayowaandama kuhusu mikakati yao ya kuhujumu Chadema na viongozi wake,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kuwa waliozusha uongo huo walikuwa na nia ovu ya kuua ndoto na matumaini ya Watanzania kufanya mabadiliko ya kimfumo na kiutawala, kwa kuiondoa CCM madarakani, kama chama kisingebaini usaliti huo na kuchukua hatua dhidi yao.
Chadema kimekuwa kwenye msukosuko baada ya mwishoni mwa mwaka jana, Kamati Kuu ya chama hicho kuwavua madaraka makada wake watatu; aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Arusha, Samson Mwigamba na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, baada ya kudaiwa kukisaliti chama.
Baada ya kuvuliwa nyadhifa zao, makada hao waliandikiwa tuhuma zinazowakabili na kutakiwa kujibu kwa maandishi lakini Zitto alikimbilia Mahakamani kuzuia Kamati Kuu isimjadili kwa kuwa alikuwa amekata rufaa Baraza Kuu.
Katika ukurasa wake wa Facebook, Zitto alimtuhumu Mbowe kwamba mwaka 2005 alichukua fedha kutoka kwa Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono kiasi cha Sh. milioni 40 ili asifanye kampeni katika jimbo hilo.
Kadhalika, alimtuhumu kwamba mwaka 2008, Mkono alimpatia Mbowe Sh. milioni 20 kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Tarime, kisha akazitoa kwenye chama kama mkopo na akalipwa na pia mwaka 2010, wakati wa uchaguzi mkuu Mkono alimpatia Mbowe Sh. milioni 200 kwa ajili ya kampeni za mgombea urais.
Pia alimtuhumu kwamba mwaka huo huo wa 2010, wakati wa uchaguzi mkuu, Mbowe alipokea Sh. milioni 100 kutoka kwa Rostam Aziz kwa ajili ya kampeni.
SOURCE: NIPASHE
1 comment:
kwanini asijitetee mbowe mwenyewe chama kimsemee.. na suala la kuzini.? (kutoka nje ya ndoa.?)
Post a Comment