ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 13, 2014

MKWAWA SHUJUA!! KWA WALE WAPENDA HADITH

KAMA UNAKUMBUKA DARASA LA TANO WALE WENYE UMRI KAMA WANGU BASI UTAKUMBUKI UKURASA HUU WA KITABU HIKI CHA TUJIFUNZE LUGHA YETU! KITABU CHA SITA(6) KARIBU UKUMBUSHIE ENZI HIZOOOO

Hapo zamani palikuwa na mzee aliitwa Muyugumba. Mzee huyo alikuwa mtemi wa Wahehe. Alikuwa akipendwa sana na watu wake.

Mtemi Muyugumba alikuwa na watoto wengi. Wawili kati yao walikuwa Mkwawa na Muhenga. Siku moja aliwaita watoto hao wawili ili kuzungumza nao. Walipofika aliwaambia, "Wanangu, nimewaiteni usiku huu huu wa leo niwaeleze habari muhimu sana. Kwanza, mnajua kwamba mimi nimekuwa mtemi wa nchi hii kwa muda mrefu. Nimeweza kuwaunganisha watu wangu mpaka tumekuwa na kauli moja. Kwa ajili ya umoja wetu, tumeweza kuwashinda maaduni wetu. Tumeweza kuhifadhi uhuru wetu. Sasa mimi ni mzee. Nguvu zinaanza kumalizika taratibu. Nimetazama katika watoto wangu wote sikumwona ambaye ataweza kuendesha kazi yangu ila ninyi. Hivyo leo nimewaita kuwapeni usia wangu.

"Mimi karibuni nitakufa. Nitakapokufa nanyi mtaitawala nchi hii. Kwa hiyo, wewe Mkwawa utakuwa mtemi wa Kaskazini; nawe Muhenga utakuwa mtemi wa Kusini ya Iringa. Ninaigawa nchi sehemu mbili ili kazi yenu iwe rahisi. Jambo kubwa ninalotaka mlikumbuke wakati wotw ni kudumisha uhuru, heshima na umoja katika nchi ya Uhehe. Msiposhirikiana hamtaweza kufanikiwa; na kazi yenu itakuwa ngumu sana." Mkwawa na Muhenga wakajibu wote kwa pamoja, "Asante baba. Tutafanya kama ulivyotuagiza."

Haukupita muda mrefu, Mtemi Muyugumba akashikwa na ugonjwa, akafa. Wahehe wakawa na huzuni sana kwani walimpenda sana kiongozi wao. Matanga yalipokwisha Mkwawa aliwekwa kuwa mtemi wa kaskazini ya Iringa na Muhenga kusini kama walivyousiwa na baba yao. Kwa bahati mbaya Muhenga alikuwa mchoyo. Hakuridhika na sehemu yake ya utawala. Hivyo aliyaamrisha majeshi yake yamvamie Mkwawa; nayo yakamvamia. Lakini Mkwawa hakukubali. Alipigana kiume, mwisho akamshinda nduguye akawa mtemi wa nchi yote ya Iringa kama ilivyokuwa wakati wa marahemu baba yake.

Wakati wa utawala wa Mkwawa, kulitokea wageni weupe kutoka Ulaya. Wageni hao walikuwa ni Wajerumani. Walifika katika nchi yetu ili kuondoa utawala wetu wa jadi na kuweka utawala wao wa kigeni. Kwa kweli wageni hao walikuwa katili sana. Waliwaua babu zetu bila kosa lolote. Waliwapiga bakora kama wanyama. Walifanya kazi katika mashamba yao, wakatengeneza mabarabara na kujenga majumba yao makubwa makubwa. Yote haya yalikuwa kwa ajili ya manufaa yao. Jambo lililokuwa baya zaidi ni kuwa waliwafanya babu zetu kuwa si binadamu kamili kama wao. Walitunyangánya nchi yetu kushibisha matumbo yao.

Mkwawa hakuweza kuvumilia ukatili wa Wajerumani. Hakupenda watu wake watawaliwe na wageni. Kwa hiyo, hakuwa na njia nyingine ya kufanya ili kuyakabili majeshi ya Wajerumani. Jamboo la kwanza alilofanya ni kuimarisha majeshi yake. Vijana wa Kihehe walijiandikisha kuwa askari kwa wingi sana. Ili Mkwawa awape askari wake mafunzo bora ya kivita, alijenga kambi kubwa mahali pamoja panapoitwa Kalenga. kambi hii ilizungukwa na ngome kubwa sana. Katikati ya ngome hiyo palijengwa nyumba kubwa. Hiyo ndiyo ilikuwa makao makuu ya Mkwawa. Pia mlikuwemo nyumbo za askari, mifugo na mashamba ya vyakula. Ngome hiyo ililindwa barabara na askari wa zamu usiku na mchana. Ilikuwa ikiitwa "Liringa", yaani "ngome kuu ya Vita." Kila kijiji kilikuwa na ngome za aina hii ili kuwalinda wananchi.

Baada ya kupigana kwa muda mrefu, na Wajerumani wengi kuuwawa, Mtemi Mkwawa aliweza kushinda Wajerumani. Lakini majeshi yake yalianza kudhoofika kwa sababu askari wake wengu waliuwawa. Wajerumani walipowashika viongozi wa Wahehe waliwanyonga hadharani!

Mkwawa alipoona kwamba Wajerumani wanazidi kuimarisha majeshi yao, na kwamba walikuwa wanamtafuta ili wamuue, alitoroka na kwenda msituni. Alitoroka na askari wake wawili ambao walikuwa wamekula kiapo cha uaminifu cha pamoja naye. Mara siku moja Mkwawa akajiona amezungukwa na majeshi ya Wajerumani. Alikuwa mtu shujua ambaye hakupenda kukamatwa mateka wala kuacha mwili wake uguswe na mzungu . Hivyo alijiua mwenyewe kwa bunduki kabla Wajerumani hawajawahi kumgusa.

Kweli Mkwawa alikuwa shujua. Anatukumbusha kuwa babu zetu hawakupenda kutawaliwa na wageni. Hawakupenda kupuuzwa. Hivyo walikuwa tayari kufa kuliko kutawaliwa 

KWA HISANI YA MAISHA NA MAFANIKIO BLG

No comments: