ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, January 12, 2014

NINENO FUPI LA LEO, JAMBA LA WAZANZIBARI NI LETU WATANGANYIKA


Ndugu zangu,

LEO Januari 12 ndugu zetu wa Zanzibar wanatimiza miaka 50 ya Mapinduzi yao.
Naam, jambo la waZanzibar ni letu waTanganyika. Na hakika, Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa mapinduzi yetu pia. Na leo hii Waunguja na Bara tumo kwenye mchakato wa Katiba Mpya ambapo pia, kuna mapendekezo ya uwepo wa Serikali Tatu, mapendekezo yalitokana na wananchi wa pande hizi mbili.
Naam, inahusu maridhiano ya kindugu yasiyotokana na uhasama na yenye lengo la kubaki kuwa wanandugu                                                                                                                                            .Na tunasoma, kuwa Mfalme Suleiman aliambiwa ndotoni aombe kitu chochote kwa Mola wake, naye akajibu; " Ewe Mola wangu, nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili ili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya, maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?" Hivyo basi, Mfalme Suleiman aliichagua hekima. Maana, ni Mfalme Suleiman huyo anayekaririwa na vitabu vya dini akitamka, ; " Watu wangu wanaangamia kwa kukosa hekima".
Naam, hekima ndilo jambo lililo bora kabisa kwa mwanadamu kuwa nalo. Mwanadamu aliyepunguwa hekima ana hasara kubwa maishani. Hekima ni tunu na kipaji ambacho Mwenyezi Mungu amewajalia waja wake, ili nao waweze kupambanua na kuamua kati ya yalo mema na maovu. Duniani hakuna shule ya hekima.
Ndio, furaha ya waZanzibar ni yetu, na huzuni yao ni yetu pia, sisi waTanganyika. Binafsi nilifika Zanzibar kwa mara ya kwanza mwaka 1988 ( pichani). Nilikuwa kijana mdogo sana. Zanzibar ndio kisiwa cha kwanza kupata kukitembelea.
Tangu hapo niliipenda Zanzibar, nimefika Zanzibar mara kadhaa. Ningelipenda sana niwe Zanzibar katika siku ya kesho kushuhudia waZanzibar wakitimiza miaka 50 ya Mapinduzi.
Naam, ningependa kushiriki sherehe hizo nikiwa na ndugu zangu waZanzibar. Maana, bado naukumbuka ukarimu wa wenyeji wangu wa Zanzibar tangu safari yangu ya kwanza Unguja, Desemba, 1988.
Nakumbuka pia kushiriki sherehe za Mapinduzi Zanzibar, Januari 12, 1989.
Naam, Wazanzibar hata katika Serikali Tatu, kama zitapitishwa, watabaki kuwa ndugu zetu. Na kwamba, jambo la waZanzibar litabaki kuwa letu pia waTanganyika, iwe la furaha au huzuni.
Happy Mapinduzi Day!
Ni Neno Fupi La Usiku.

Maggid Mjengwa

No comments: