Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
WAKATI hatua zaidi zikisubiriwa kuchukuliwa kwa watendaji waliohusika na ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa Operesheni Tokomeza, Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kutangaza kuanza kwa awamu ya pili ya Operesheni hiyo wakati wowote kuanzia sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema wakati wowote Rais Kikwete atatangaza kuanza kwa Awamu ya Pili ya Operesheni Tokomeza na itazingatia haki zote ikiwemo haki za binadamu.
Nyalandu alisema ingawa awamu ya kwanza kulikuwa na kasoro zilizojitokeza, awamu hii ya pili kasoro hizo zitafanyiwa kazi ili kuhakikisha rasilimali za Taifa zinalindwa.
Kusitishwa kwa operesheni hiyo kulikosababisha uteuzi wa mawaziri watatu kutenguliwa na waziri mmoja, kujiuzulu kwa mujibu wa Nyalandu, kulisababisha pia tembo 60 kuuliwa.
Mawaziri ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais Kikwete mwishoni mwa mwaka jana ni Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo) huku Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), akijiuzulu.
Katika hatua nyingine, Nyalandu amemsimamisha kazi Ofisa Wanyamapori Mwandamizi wa Pori la Akiba la Maswa, Lawrence Kileo, ambaye anatuhumiwa kupokea rushwa na kuwatoza faini wafugaji wanaoingiza mifugo ndani ya pori la akiba bila kuwapa risiti halali ya Serikali.
Pia, ameamuru mamlaka husika kukamilisha uchunguzi na kuchukua hatua za kinidhamu haraka dhidi ya Ofisa Wanyamapori wilayani Kasulu mkoani Kigoma, Benjamin Mkasamali. Ofisa huyo anatuhumiwa kuwatorosha majangili ambao waliwinda wanyamapori wasioruhusiwa kuwindwa katika kibali kinachotolewa na Serikali.
Nyalandu alisema Kileo amesimamishwa kazi, kutokana na makosa ya kupokea rushwa na kuwatoza faini wafugaji wanaoingiza mifugo ndani ya pori la akiba bila kuwapa stakabadhi ya Serikali, kinyume na Kifungu 116(2) (c) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Namba 5 ya 2009.
Mkasamali anachunguzwa baada ya Wizara kutumia njia za kiintelijensia na kubaini kuwa aliingilia kati na kuwaachia huru majangili, waliokamatwa na kikosi cha doria cha Kampuni ya Friedkin Conservation Fund.
Majangili hao wanadaiwa kuwinda wanyama aina ya tohe 12, madume watano na majike saba, ambao hawakuwepo katika orodha ya leseni yao ya uwindaji namba B59921, iliyotolewa na ofisa huyo Novemba 29 /2013. Pia majangili hao waliua wanyamapori wengine wanne aina ya oribi.
Alisema baada ya Mkasamali kuwaruhusu majangili hao kuondoka, ambao tayari walishakamatwa na kikosi cha doria, kiongozi wa kikosi hicho aliwasiliana na RPC Kigoma, Freiza Kashai.
Inadaiwa Kamanda Kashai alitoa ushirikiano kwa kumwagiza OC CID Kasulu, Athuman Namba ambaye alishirikiana na Ofisa Usalama Taifa Kasulu, ambao kwa pamoja waliweka kizuizi sehemu ya Kibagwe njia ya kwenda Kigoma na kukamata majangili hao na kurudishwa Kasulu, ambako wamefunguliwa kesi.
CHANZO HABARI LEO
1 comment:
Huyu naibu waziri inabidi awajibichwe pia kwenye hicho cheo alikuwa wapi wakati wote huyo?anajitoa sana magazitine kwa sasa kutafuta vyeo kinguvu naibu waziri mzigo huyu.
Post a Comment